7. Visa Vya Mitume

Tumtendee haki Nabii Isa!

Katika muktadha wa dini kuu kwenye ulimwengu wa sasa, na kusema ukweli, kwa nyakati zote tangu kuzaliwa kwake, mtu huyu anayeitwa Isa (Kiarabu), Ishoa (Kiaramaic), Joshua (Kiebrania), Jesus (Kiingereza) na Yesu (Kiswahili), amekuwa mara zote akitukuzwa kama mtu muhimu katika kujenga mtazamo sahihi wa imani. Utata mkubwa umeigubika mada hii na kwa baadhi, kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu nini hasa cha kuamini kumhusu bwana mkubwa huyu, kuanzia kwenye mambo ya msingi kabisa. Alikuwa Mungu? Alikuwa binadamu? Alikuwa Mungu na binadamu? Alikuwa roho? Au alikuwa vyote vitatu: Mungu, binadamu na roho? Au alikuwa mtu bora maalumu, aliyechaguliwa kuwasilisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu, yaani Mtume kama Nuhu, Ibrahim, Mussa na Muhammad (rehema na amani ya Allah imshukie). Mfululizo wa makala hizi unalenga zaidi kujibu swali, huyu Yesu Kristo alikuwa nani hasa, kwa kuchunguza maneno yake mwenyewe yaliyoripotiwa. Ili kufikia lengo hilo, ni muhimu sana kutegemea vyanzo nyenye kuaminika. Kwa kuanzia, inafahamika vyema kwamba kwa asili, Isa (amani ya Allah imshukie) au Yesu kama anavyojulikana kwa upande mwingine, alitokea katika kabila la Kiyahudi (siyo dini ya Uyahudi). Isa alizaliwa na mwanamke bikira aliyekuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu, Maryam (Maria). Hakuna ubishi, ‘Yesu Kristo’ hakuwahi kuzungumza hata neno moja la Kiingereza, au hata kusikia tu jina hili ‘Yesu’ ambalo amenasibishwa nalo leo. Jina hili ‘Yesu’ siyo neno la Kiebrania na limekuja kama matokeo ya tafsiri nyingi tofauti kwa kipindi kirefu. Karibu zaidi na Kiebrania (Joshua) ni Kiarabu (Isa), ambapo kuna tofauti ndogo tu ya matamshi. Leo hii kuna matoleo mbalimbali ya Biblia, ambayo kila dhehebu la Kikristo linadai kwamba toleo lake ndiyo sahihi zaidi. Jambo la kufurahisha ni kwamba kuna toleo moja maalumu la Biblia, linalojulikana kama ‘Red Letter Bible’ ambalo, kwa urahisi wa kufanya rejea, maneno yanayohusishwa moja kwa moja na Isa (Yesu), yameandikwa kwa wino mwekundu. Cha kushangaza na kutia hofu, vitabu vyote vya agano jipya na la kale, vikiwekwa pamoja, ni pungufu ya kurasa ishirini na tano zilizoandikwa kwa wino mwekundu! Hii inaonyesha kuna mafundisho machache mno ya moja kwa moja kutoka kwa mtu huyu mashuhuri, kiasi cha kuigemeza dini nzima kwenye mafundisho hayo. Yaliyobaki ni maneno ya Mark, Mathayo, Luka na Yohana, ikiwemo maoni binafsi ya Paulo, ambaye ndiye anayeaminika kwa wanatheolojia wengi na wanahistoria kama muasisi wa Ukristo wa kisasa. Kipindi cha nyuma, kabla ya Paulo, mataifa (wasiokuwa Mayahudi) hawakuruhusiwa kufuata habari njema aliyokuja nayo Yesu. Hili, kama tulivyoona, ni tatizo jingine la usahihi – waandishi wa Agano Jipya wakiwa hawajulikani, lakini Wakristo wamekubaliana kwamba wote hao hawakuwahi hata kukutana na Yesu. Tunachotaka kujua ni Isa (amani ya Allah imshukie) au Yesu Kristo kama anavyoitwa, amesema nini na siyo tafsiri na maoni ya wengine, ambao hawakuwahi hata kumuona. Kutoka kwenye Biblia Takatifu, sasa tuichunguze Qur’an Tukufu. Hiki ni kitabu ambacho bado kimehifadhiwa katika lugha yake asili ya Kiarabu, ikithibitishwa na ukweli kwamba mamilioni ya watu wamekihifadhi chote kichwani. Kwamba Kitabu hiki ndiyo toleo pekee linalokubalika ndani ya Uislamu ni jambo lisilohitaji mjadala. Bila ya kuzingatia bara, au nchi au hata lugha anayozungumza mtu, Qur’an bado inasomwa katika lugha yake asili ya Kiarabu. Kwa hiyo, kosa au mabadiliko yoyote yakitokea yatabainishwa haraka sana. Methodolojia hii imedumishwa kuanzia zama za Mtume wa mwisho Muhammad (rehema na amani ya Allah imshukie) mpaka leo. Hakuna kitabu kingine au maandiko yoyote matakatifu duniani, yanayoweza kujisifu kuwa na heshima kama hiyo katika uhifadhi wake wa asili. Qur’an imebaki na itaendelea kubaki kuwa chanzo pekee chenye kuaminika, katika kutoa na kufahamu mafundisho sahihi ya Mwenyezi Mungu, yaliyofunuliwa kwa Mitume na Manabii wote. Mafundisho ya Qur’an Tukufu kuhusu mada hii tunayoijadili yako mbali kabisa na hiyana dhidi ya ‘Yesu Kristo’ kama Wakristo wengi wanavyodhani. Isa (amani ya Allah imshukie) ambaye wenzetu wanamwita Yesu, ametajwa mara nyingi zaidi kwa jina ndani ya Qur’an, ikilinganishwa na Muhammad mwenyewe (rehema na amani ya Allah imshukie). Ndani ya Qur’an Tukufu kuna sura maalumu ambayo imeitwa kwa jina mama yake Isa (amani ya Allah imshukie), Surah Maryam (Surah ya Maria). Wakati tunapoanza kuangalia kauli zote ndani ya Qur’an Tukufu zinazomrejea Isa (Yesu) lazima tujiandae kiuadilifu kutafuta ufahamu wa kweli. Kwa ajili ya mfululizo wa mada hii, basi tuanze na: “Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, alimuumba kwa udongo kisha akamwambia, ‘Kuwa!’ Basi akawa” (Qur’an, 3:59). Mbele ya Mwenyezi Mungu, mfano wa Isa (Yesu) ni kama ule wa Adam (amani ya Allah imshukie). Kama yalivyo yote ambayo Mwenyezi Mungu anayataka, akisema ‘Kuwa’ basi yanakuwa. Si jambo gumu wala lenye kutia shaka kwa yule ambaye Yeye peke yake ndiye anayestahili kuabudiwa. Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake. Aya ifuatayo tutakayoangazia inafafanua kwa uwazi kabisa kile kinachodaiwa kuwa Yesu alisulubiwa msalabani. Na ndiyo sababu yangu hasa ya kuandaa mfululizo wa makala hizi, ili zikamilike na sikukuu ya Pasaka, ambayo kimsingi ni maadhimisho ya kumbukumbu ya ‘kusulubiwa’ Yesu Kristo. Waislamu tunaamini kwamba Isa (amani ya Allah imshukie) atarejea tena duniani kabla ya saa ya mwisho. Kwa wakati ule alinusuriwa na Mwenyezi Mungu na njama za maadui na akamnyanyua Kwake. Yesu lazima arudi na atarudi kwa sababu nyingi tu. Mojawapo ni kwamba bado hajafa na binadamu wote lazima waonje mauti katika maisha haya ya dunia. “Na kwa kusema kwao, ‘Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu’ – nao hawakumuua wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka. Hawana ujuzi nayo wowote, ila wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua” (Qur’an, 4:157). Kuna utafiti mwingi unaoonesha kwa njia ya mfuatano wa matukio jinsi madai haya ya kusulubiwa Yesu Kristo yalivyo mbali na ukweli. Qur’an iko wazi sana kuhusu jambo hilo kwamba ‘hawakumuua’ wala ‘hawakumsulubu’ na kile wanachosema Wakristo ni ‘kubahatisha’ tu. Wanajaribu tu kuhalalisha ‘dogma’ iliyobuniwa kitaalamu kwamba Yesu alibeba mzigo wa dhambi za binadamu wote na habari hii inasambazwa dunia nzima kupitia propaganda mbalimbali. Lakini ukweli wake hasa, hakuna mahali popote ndani ya maandiko matakatifu yaliyo sahihi, kwamba Yesu Kristo alitoa madai tata kama hayo. Aya hii inayofuata inawashauri Mayahudi na Wakristo, kwa njia ya mawaidha, kutoruka mipaka katika dini. Mayahudi walimkataa Isa (Yesu) wakisema wao wanamfuata Musa tu. Na Wakristo, kutokana na mahaba, wakamuweka Yesu katika daraja la Mwenyezi Mungu. Nao wakatumbukia kwenye mtego ule ule kama Mayahudi, wa kumkataa Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah imshukie), bila ya ushahidi au hoja za kweli. Wa i s l a m u , k w a u p a n d e mwingine, wanafuata njia ya kweli ya maisha, ile iliyowekwa na Mwenyezi Mungu, wakidumisha njia ya kati na kuwakubali, kuwaheshimu na kuwaamini wote hao watatu kama Mitume Watukufu wa Mwenyezi Mungu na wengine wote. “Enyi Watu wa Kitabu! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli. Masihi Isa bin Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilompelekea Maryam, na ni roho iliyotoka kwake. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme ‘watatu’…Jizuieni na (Itikadi hiyo), Itakuwa bora kwenu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ni mbali na utukufu wake kuwa ana mwana. Ni vyake vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni mlinzi wa kutosha” (Qur’an, 4:171). Aya hii vilevile inaonya vikali dhidi ya kusema ‘watatu’ yaani (Utatu Mtakatifu) kwa sababu Itikadi hiyo inapingana kabisa na imani ya Mungu mmoja. “Masihi (Nabii Isa) hataona unyonge kuwa mja wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika waliokurubishwa (na Mwenyezi Mungu hawataona unyonge kuwa waja wa Mwenyezi Mungu). Na watakaoona unyonge uja wa Mwenyezi Mungu na kutakabari, basi atawakusanya wote Kwake (awatie motoni)” (Qur’an, 4:172). Kwa hiyo, tunaona kupitia Aya hii kwamba kuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu, ni moja kati ya hisani kubwa za Muumba kwa kiumbe wake, na kupata hadhi hiyo siyo unyonge wala udhalilishaji, kwa kuwa hakuna yeyote anayekaribia utukufu wa Mwenyezi Mungu. Isitoshe, hakuna viumbe bora kama Mitume, na katika hili, mitume wote akiwemo Isa (amani ya Allah imshukie) walifahamu ukweli huu, kama walivyoelewa Malaika, ambao wakati wote wako tayari kumtukuza Mwenyezi Mungu bila hata chembe ya kiburi wala kujihisi wanyonge. Lakini Aya nyingine ifuatayo inabainisha nguvu zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu. “Hakika wamekufuru waliosema: “Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryam. Sema, ‘Ni nani mwenye kumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryam, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi?’ Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu” (Qur’an, 5:17). Nukta ya kwanza kuangalia ni swali la nani anayeweza kumzuia Mwenyezi Mungu na njia zake mbalimbali za kuonyesha nguvu zake? Tunaona mifano halisi ya nguvu Zake katika matetemeko ya ardhi na jinsi yanavyoangamiza watu bila kujua, ingawa kuna baadhi wanaendelea kumkana Mwenyezi Mungu. Nukta ya pili ni mwishoni mwa Aya ambapo Mwenyezi Mungu anasema, yeye anaumba anachotaka au anayemtaka. Isitoshe Yeye ndiye aliyemuumba Adam (amani ya Allah imshukie) bila ya mama wala baba. Itakuwa Yesu ambaye alikuwa na mama? Mambo yote hayo yamefanyika kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anafanya uumbaji wake kwa malengo na hekima maalumu na wala hawajibiki kwa yoyote. Suala la kumuinua Yesu mpaka katika hadhi ya Uungu au kusema kwamba ni mwana wa Mungu ni hatari sana na kinyume kabisa na imani ya Mungu mmoja. Aya hizi mbili zifuatazo zinabainisha hilo. “Hakika wamekufuru waliosema, ‘Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryam!’ Na hali Masihi mwenyewe alisema, ‘Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu. Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru’” (Qur’an, 5:72). “Kwa hakika wamekufuru waliosema, ‘Mwenyezi Mungu ni wa tatu katika Utatu’. Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayosema, kwa yakini itawakamata adhabu kali wale wanaokufuru” (Qur’an, 5:73) Isa (amani ya Allah imshukie) anaelekeza, kama Mitume wote waliopita walivyofanya, kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake – “Mungu wangu na Mungu wenu”. Anawakumbusha watu wake kwamba tofauti yake na wao ni kwamba yeye amechaguliwa na Mwenyezi kutangaza imani ya Mungu mmoja. Watu wachache sana wamepata baraka hii ya Mwenyezi Mungu kuwa viongozi wa wanadamu, lakini kwa watu wengine haitoshi Isa (Yesu) kuwa Mjumbe Mtukufu wa Mwenyezi. Wameamua kumfanya Mungu kabisa na hivyo kupotosha dhana nzima ya imani ya Mungu mmoja na kufuta ujumbe aliokuja nao Yesu. Moja ya hoja nzito za Qur’an Tukufu ni kwamba Mwenyezi Mungu ameshusha mifano mingi, ili kuufanya ukweli ubainike wazi bila ya mazonge. Mifano hii inawafaa watu wote watakaoitumia isipokuwa kwa sharti kwamba wawe wadilifu katika utafiti wao. “Masihi mwana wa Maryam si chochote isipokuwa ni Mtume. Wamekwishapita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa” (Qur’an, 5:75). Je? Kitendo cha Isa (Yesu) na Maryam (Maria) (amani ya Allah iwashukie) kula chakula, hakitoshi kuonyesha kuwa walikuwa tegemezi? Nini dhana yako ya Mwenyezi Mungu? Anakula chakula? Katika Uislamu Mwenyezi Mungu amejitosheleza na hahitaji chochote – hafanani na binadamu kwa namna yoyote. Katika theolojia, dhana ya Mwenyezi Mungu ni nyeti. Hakuna shaka, ni Uislamu tu ndiyo unaokidhi vigezo makini katika kumbainisha Mwenyezi Mungu peke yake, ambaye ndiye hasa anayestahili kuabudiwa. Kumtukuza Isa na kumpa hadhi ya Mungu ni kumkutana Mwenyezi Mungu na kumdhalilisha Yesu mwenyewe. Isa alizaliwa Mtume na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na wale wanayemuomba badala ya Mwenyezi Mungu wamemfananisha na masanamu ya kuchonga na miungu mingine iliyotengenezwa na wanadamu. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu anajua wazi kwamba Isa (amani ya Allah imshukie) hakuwahi kupindisha ujumbe aliopewa kwamba “Hapana Mola apasaye Kuabudiwa kwa Haki isipokuwa Mwenyezi Mungu”. Na Mwenyezi Mungu mwenyewe anasema ndani ya Qur’an: “Walilaaniwa waliokufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryam. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka” (Qur’an, 5:78). Ni jambo lisilokuwa na shaka kwamba Isa (Yesu) (amani ya Allah imshukie) alikuwa na hadhi maalumu aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Katika makala inayofuata, Insh’Allah, tutabainisha baadhi ya neema maalumu ambazo Yesu alipewa na Mwenyezi Mungu, tukiangazia jinsi alivyobarikiwa kama mtu maalumu, bila ya kuwa na haja ya kuinuliwa katika hadhi asiyostahili. Bado inaendelea, Insh’Allah!

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close