7. Visa Vya Mitume

Kisa cha Nabii Yunus Aliyemezwa na Samaki

Katika mtiririko wa visa adhimu vya Mitume, tuliona katika toleo lililopita sehemu ya kwanza ya kisa cha Nabii Yunus (amani ya Allah imshukie).

Katika mtiririko wa visa adhimu vya Mitume, tuliona katika toleo lililopita sehemu ya kwanza ya kisa cha Nabii Yunus (amani ya Allah imshukie). Katika kisa hicho tuliona kuwa Nabii Yunus alimezwa na samaki baharini ambako aliomba dua akiwa ndani ya tumbo la samaki na hatimaye Allah akajaalia samaki yule akamcheua. Katika muendelezo wa kisa hiki, leo tunafafanua zaidi mkasa huu na kuangalia matukio yaliyofuata. Malaika wamwombea Yunus kwa Allah Aliyetukuka Akiwa ndani ya tumbo la samaki, Nabii Yunus (amani ya Allah imshukie), aliomba dua isemayo: ”Lailaaha illa Anta Sub-hanaka Inniy kuntu Minadhwalimiyn,” (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu). Maombi haya ya Nabii Yunus yakawa yanazunguka katika Arshi Tukufu ya Allah. Malika wakasema: “Ewe Mola wetu Mlezi, hivi hii siyo sauti dhaifu na maarufu inayotoka katika miji migeni ya mbali?” Allah aliyetukuka Akasema: “Hivi hamuijui sauti hiyo?” Wakasema: “Ewe Mola wetu ni nani huyo?” Allah Aliyetukuka Akasema: “Huyu ni mja wangu Yunus.” Malaika wakauliza: “Mja wako Yunus ambaye bado maombi na amali zake zinakubaliwa?!”Malaika wakasema: “Ewe Mola wetu, tunakuomba umuhurumie kupitia amali zake za kipindi cha raha zimwokoe yeye na balaa hili.” Hivyo, Allah akakubali maombi ya Malaika na akamwokoa Nabii Yunus kwa kumwamuru samaki ammeze kisha kumtupa ufukweni. (Taz: Mukhtasar wa Ibin Kathir4/ 18-19). Yunus (amani ya Allah imshukie) alitoka katika tumbo la samaki akiwa dhoofu kutokana na maradhi na shida huku kiwiliwili chake kikiwa hakina nguvu. Allah aliyetukuka anasema: ”Lakini tulimtupa ufukweni patupu, h a l i y u m g o n j w a ” (Qur’an, 37:145). Na Allah aliyetukuka akamuoteshea yeye katika ufukwe wa bahari mti wa Yaqtwini, mmea wenye majani mapana, wenye faida nyingi katika mwili. Nabii Yunus ikawa anakula katika majani ya mti huo na kujificha chini ya kivuli chake kutokana na jua kali. Nabii Yunus akabaki kuwa katika hali hiyo kwa muda mpaka siha yake ikaanza kurejea kidogo kidogo. Imepokewa Hadithi na Ibn Abii Waqqas (Allah amridhie) amesema amemsikia Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) akisema: “Jina la Allah ambalo akiombwa kupitia jina hilo hujibu haraka na anapoombwa haja yoyote ile hutoa, ni dua ya Nabii Yunus.” Ibn Abii Waqqas akamuuliza Mtume: “Ewe, Mjumbe wa Allah, dua hii ni mahususi kwa Yunus pekee ama ni kwa Waislamu wote?” Mtume akasema: ”Dua hiyo ilikuwa ni mahususi kwa Nabii Yunus, na pia ni kwa waumini wote pindi wanapoisoma.” Kwani hukusikia kauli yake Allah aliyetukuka pale aliposema: “Na Dhan-Nuni (Yunus) alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: ‘Hapana Mungu asipokuwa wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.’ Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivi ndivyo tunavyowaokoa waumini” (Qur’an, 21: 87-88) [Taz: Tafsiri ya Bin Jariri Atwabari,sura ya Al-anbiyaai 17/82] Na imekuja katika Hadithi nyingine ya Mtume (rehema na amani imshukie) iliyopokewa na Imamu Tirmidhiy na An-Nasai. Mtume amesema: ”Dua ya Dhan-Nuni (Yunus) ‘Lailaahaillaanta Subhaanaka inniy kuntu minadhwaali m i y n ,’ M u i s l a m u akimuomba Mola wake dua hii kwa shida yoyote ile Allah humtatulia shida yake.” Simulizi za Nabii Yunus na kijana mmoja Mtume wetu Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake) a m e t u h a b a r i s h a kwamba Nabii Yunus alijificha katika kivuli cha mti wa Yaqtwin, na kwamba aikuwa akila majani yake na kwamba kipindi fulani, mti huu ulinyauka na kukauka. Hivyo, Nabii wa Allah Yunus akalia kutokana na kukauka kwa mti huu, Allah akamfahamisha

kwa kumlaumu: ”Hivi unalia kwa sababu ya mti huu kukauka, na wala hukulia kwa watu laki moja au zaidi ya hao uliotaka kuwahilikisha?!” Na siku moja afya ya mwili wake ilipoanza kurejea vema, alikuwa anatembea akamkuta kijana mmoja anachunga mbuzi na kondoo. Nabii Yunus akamuuliza kijana yule anatoka katika kaumu gani? Kijana yule akamjibu kuwa yeye anatoka katika kaumu ya Yunus. Hivyo akamtaka amfikishie salamu zake kwa kaumu yake, na awajulishe ya kuwa yeye amekutana na Yunus. Huyu kijana aliyekuwa na busara na utambuzi wa hali ya juu, kwa kuwa alijua hukumu iliyopo kwa jamaa zake kuhusu adhabu ya mtu mwongo, hivyo, akasema kumwambia Yunus: “Ikiwa ni Yunus bila shaka unafahamu kwamba adhabu ya mwongo asiyeleta ushuhuda wa kile anachokisema kwa desturi yetu ni kuuliwa. Hivyo basi ni nani atakayenishuhudilia mimi hayo unayoyasema? Yunus akasema: “Mti huu na eneo hili vinatosha kuwa ni shuhuda kwako wewe.” Kijana yule akamwambia Yunus: “Basi mti huu pamoja na ardhi yake viamrishe vinitolee ushahidi.” Yunus (amani ya Allah iwe juu yake) akawaambia atakapowajieni kijana huyu mtoleeni ushuhuda, mti na ardhi vikajibu: “Ndiyo”. Na yote haya yamefanyika kwa uwezo wake Allah aliyetukuka. Kijana akarejea kwa watu wake. Naye alikuwa na ndugu wenye hadhi na madaraka katika kaumu yake ambao humkinga yeye na kila anayetaka kumdhuru. Hivyo, kijana yule akamwendea mfalme na akamjulisha ya kuwa amekutana na Yunus, na akafikisha salamu za Yunus kwa mfalme na jamaa zake. Na habari iliyothibiti kwa Mfalme ni kwamba Yunus alikuwa tayari ameshakufa siku nyingi. Wasafiri walimuhadithia Mfalme kuwa Yunus amehiliki baharini kwa kumezwa na samaki. Habari ya kijana huyu kudai kuwa Yunus yu-hai ni uongo shahiri dhahiri. Hivyo mfalme akaamuru kijana yule auliwe palepale. Kijana akasema ana ushahidi unaothibitisha maneno yake. Hivyo Mfalme akatuma watu wake kwenda kuthibitisha jambo hilo. Na walipofika katika mti na eneo ambalo Yunus aliamrisha vitoe ushuhuda, kijana yule akaziuliza ardhi na mti kwa kusema: “Tunakuombeni kwa Allah, je, nyie mmemshuhudia Yunus kuhusu kadhia hii.” Vikajibu: ”Ndiyo”. Wajumbe wale wakarudisha majibu kwa mfalme wakiwa na hofu na wasiwasi. Mfalme alivyosikia habari hiyo alijivua madaraka yake, akaushika mkono wa kijana yule na kumkalisha katika kiti chake cha ufalme, na kisha kumsimika ufalme kwa kumwambia: “Wewe unastahiki zaidi wadhifa huu kuliko mimi.” Na Mtume wetu (rehema ana amani zimshukie) ametuhabarisha kuwa kijana huyo alihukumu kwa kipindi cha miaka 40, akisimamia mambo ya watu wake kwa kusuluhisha baina yao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close