7. Visa Vya Mitume

Kisa cha Nabii Ayyub: Mfano wa Subira

Katika makala iliyopita tulimuona Nabii Ayyub (amani ya Allah imshukie) akiridhia kudura ya Allah aliyetukuka aliyeamua kumpa mtihani mzito. Katika makala hii tuangazia zaidi msimamo wa Nabii huyu unayomfanya awe mfano katika subira.

Ayyub mja mwenye subira

Allah aliukuta moyo wa Nabii Ayyub (amani ya Allah imshukie) upo radhi na wenye uvumilivu, pamoja na balaa zito lililomkabili. Nabii Ayyub hakuwahi kuchukia kutokana na balaa hilo hata siku moja. Hivyo Allah ‘Azza wa-Jallah, akamsifu yeye kwa kusema: “Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu,” (Qur’an, 38: 4). Angalizo muhimu Zimekuja riwaya kupitia baadhi ya vyanzo dhaifu kwamba Nabii Ayyub (amani iwe juu yake) alijaribiwa na Mola wake kwa maradhi makubwa na ya kutisha kama vile ukoma, mbalanga na maradhi mengine ambayo huwafanya watu wajitenge naye kwa kuogopa kuambukizwa na kwamba yeye alitengwa nje ya mji katika dampo la kutupia taka. Kauli zote hizi ni za uongo juu ya Nabii wa Allah Ayyub (amani ya Allah imshukie). Haiwezekani Allah aliyetukuka amjaribu Nabii wake yeyote kwa kumpa maradhi yatakayowafanya watu wajitenge naye kwa sababu kufanya hivyo ni kuweka kizuizi baina ya Nabii huyo na ufikishaji wa wito na mahu- biri ya Allah aliyetukuka pamoja n a sharia na hukumu zake. Kwa hiyo, hizo ni katika kauli na visa vya uongo na dhaifu (Is – railiyyati), ambavyo vinapingana na mafundisho ya Qur’an na Sunna (Hadithi) Sahihi za Mtume. Mke mtiifu wa Nabii Ayyub Maradhi yaliendelea kumsumbua Nabii Ayyub (amani ya Allah imshukie) hadi jamaa zake wa karibu na wa mbali wakaacha kumuuguza. Watu wake hawakumjali tena isipokuwa mke wake mtiifu na mvumilivu. Mke wake huyu alikuwa akimchunga Nabii Ayyub na kumuhudumia hadi akiba yake aliyokuwa nayo ikamalizika. Mkewe alikosa njia nyingine ila kwenda kuwatumikia watu ili kupata fedha ya kumnunulia chakula mumewe mgonjwa. Ayyub (amani ya Allah imshukie) alizidi kupata uchungu pale anapona hali ya mkewe ilivyobadilika kutoka utajiri wa hapo awali hadi ufakara, na kutoka katika raha na neema hadi shida, mateso na kuwatumikia watu. Hali ya maradhi na balaa ikazidi kuendelea kumwandama Nabii Ayyub (amani ya Allah imshukie) kwa miaka mingi huku mkewe akiendeleza subira, uvumilivu juu ya hukumu ya Allah na kumdhukuru Allah. Watu wakawa wanamuhurumia mkewe Nabii Ayyub, kutokana na matatizo yaliyomsibu mumewe lakini ukafikia muda watu wakaanza kuogopa kwa kudhani kwamba ni maradhi ya kuambukiza kwa maana yanaweza kutoka kwa Nabii Ayyub na kumwambukiza mkewe kisha na wao kuyapata maradhi hayo kupitia kwa mkewe. Kwa sababu hiyo, watu wakawa wanatahadhari na mkewe na wakampiga marufuku kufanya kazi tena katika maeneo yao. Mke mtiifu wa Nabii Ayyub alifikiri sana na kujiuliza angejikwamua vipi ili aweze kumlisha mumewe mgonjwa na kumuhudumia. Nabii Ayyub aliendelea kuzama katika lindi la mawazo hadi akapata ufumbuzi mgumu kwani hakuwa na namna nyingine. Mke wa Ayyub alikata misokoto ya nywele zake na kwenda kuziuza kwa mabinti wa matajiri kwa kupewa ujira wa chakula na vinywaji vingi. Kisha alirejea kwa mumewe kwa furaha na bashasha kubwa kwa kuwa amefanikiwa kumpatia yeye chakula. Kila ilipotokea hali hiyo, Nabii Ayyub alimuuliza mkewe wapi alipata chakula hicho? Mkewe aliogopa kuzungumza ukweli na kwa kuhofia kumkasirisha mumewe Kwa hiyo mke wa Nabii Ayyub kila alipoulizwa alijibu: “Nimewatumikia baadhi ya watu na kupewa ujira huu.” Miaka ya majanga na matatizo ikazidi kumwandama Nabii Ayyub (amani ya Allah imshukie) huku maradhi yakimzidia kila uchao na wakati huohuo akiishi katika ufukara uliotopea na upweke nkubwa kwa sababu ya kukimbiwa na jamaa na ndugu. Ni pekee mkewe, mtiifu, mwenye moyo safi na wa huruma aliyebakia akimhudumia. Pamoja na yote hayo, Ayyub hakutetereka bali aliendelea na msimamo wake uvumilivu, kushukuru na kuridhia hukumu na maamuzi ya Allah aliyetukuka.

Majadiliano baina ya watu wawili

Jambo pekee lililomuhuzuni Nabii Ayyub (amani ya Allah imshukie) katika moyo wake ni majadiliano ambayo aliyasikia kutoka kwa watu wawili wa karibu naye zaidi. Mmoja kati yao alisema kumwambia mwenzake: “Hakika Nabii Ayyub inaonesha ametenda dhambi kubwa sana, kama si hivyo haya maradhi yangekuwa yameshapona.” Nabii Ayyub alizipata habari hizi kupitia kwa mtu mwingine aliyekuja kumsimulia. Naye mmoja kati ya wawili hawa alifikiiri sana kuhusu hali ya Ayyub na masaibu yanayoendelea kumpata kwa muda wa miaka kumi na nane na wala Allah hakumuondolea yeye haraka masaibu hayo. Hivyo, mtu huyu ikawa anafikiri kwamba huenda labda balaa alilokuwa analipata Nabii Ayyub ni kutokana na dhambi kubwa aliyoifanya. Mtu huyu alimdokeza mwenzake kuhusu fikra inayojiri ndani ya moyo wake. Nabii Ayyub hakuvumilia aliposikia maneno hayo. Alihisi uchungu mkubwa na bila ajizi aliwabainishia masaibu yake. Huenda hilo likafuta fikra mbaya walizokuwa zilizojengeka kwa watu hao. Nabii Ayyub aliwaambia nini watu wale? Fuatilia kisa hiki to- leo lijalo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close