1. Tujikumbushe

Wito: Msiogope kuvaa hijab kwa kuhofia kudhihirisha Uislamu wenu

Imetajwa kuwa wanawake wengi wa Kiislamu wamekuwa wakisuasua kuvaa vazi tukufu la hijab kwa sababu ya kuogopa kudhihirisha Uislamu wao machoni mwa watu.

Hilo limebainishwa na washiriki wa kongamano la siku ya hijab duniani lililofanyika katika hotel ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam.

Naima Msika, mmoja wa waliohudhuria kongamano ambaye pia ni mwanaharakati wa vazi hilo tukufu, alisema kumekuwa na tabia ya watu kuogopa kudhirisha Uislamu wao kwa kuvaa hijab wakiamini kuwa wataonekana ni watu wa tofauti.

Wasiwasi huo umesababisha wanawake wengi leo hii kuvaa bila kujisitiri, wakivaa nusu hijab ili kuendana na usasa Naima alisema, haoni sababu wa wanawake kuogopa kuvaa hijab kwa sababu ni vazi lenye faida kubwa hapa duniani na kuna malipo makubwa mbele za Allah kwa wanaojistiri.

Naima aliwaambia wadada wa Kiislamu kuwa kujidhihirisha kuna faida kubwa, huku akitoa mifano na uzoefu wake wa kuvaa vazi hilo.

“Mimi nilikiwa nakwenda zangu Dubai. Nilipofika uwanja wa ndege wa Mwalimu Jurius Kambarage Nyerere (JNIA) nilihitaji kusali lakini sikufahamu wapi pa kusalia. Nilimuona mdada amevaa hijab nikajua huyu ni Muislamu. Akanisaidia kwa kunipeleka kusali pale anaposalia yeye. Nilimtambua kwa vazi lake, naye alinijua kwa vazi langu,” Naima alisema.

Alisema, mbali na vazi la hijab kumtambulisha limewahi pia kumpatia faida ya kujua sehemu ambayo imepangwa maalumu kwa ajili ya kusali, kitu ambacho awali alikuwa hakitambui.

Kwa upande wake mwandishi na mtangazaji wa kituo cha Azam TV, Fatma Chikawe, alitaka vazi la hijab lipewe thamani yake na kusiwe na haja ya kuogopa kuvaa. Akizungumzia wanaosuasua kuvaa vazi hilo, alisema wanapaswa kuvaa vazi hilo kwa kujiamini huku wakitaraji malipo kutoka kwa Allah.

Hata hivyo, Chikawe alisema zipo changamoto za kuvaa vazi hilo, ikiwemo kusemwa vibaya.“Sio kazi rahisi kujidhirisha, unahitaji uwe na moyo mgumu na imani thabiti hasa katika sekta ya michezo ambayo naifanyia kazi ambako imezoeleka wanawake wawe na muonekano fulani.”

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, Chikawe alisema anaendelea kupambana na kuhakikisha anabaki kudumu na vazi hilo tukufu.

Chikawe ambaye pia ni mtangazaji wa kipindi cha michezo kampuni ya Azam Media, aliwataka wanawake wa Kiislamu kujitambua, kuona fahari katika kuvaa hijab kwani vazi hilo linalinda utu, haki na heshima ya mwanamke.

“Mimi nilionekana wa tofauti, jamii ya wanamichezo haikuzoea kuona watu wakivaa hijab katika kazi hiyo. Nilikatishwa tamaa na kuambiwa sitoweza lakini naendelea kuvaa hijab tena kwa kujifaharisha nayo,” alisema.

Siku ya Hijab Duniani iliyoanzishwa rasmi mwaka 2013 huadhimishwa kila mwaka tarehe Mosi Februari kwa lengo la kufuta na kuondoa mazoea hasi yaliyoenea kuhusu wanawake Waislamu wanaovaa hijab Katika siku hii, wanawake wote, bila kujali dini au rekodi zao za huko nyuma hushajiishwa na kuhamasishwa kuvaa vazi la stara na staha la Kiislamu la hijab ili kupata tajiriba na uzoefu wa siku moja ya maisha ya mwanamke Muislamu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close