1. Tujikumbushe

Wajibu wa kulinda mali na damu za wasiokuwa Waislamu

Mwanadamu katika Uislamu hajitawali, bali anatawaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Ni vya nani vilivyomo katika mbingu na katika ardhi? Sema, ‘Ni vya Mwenyezi Mungu.’” [Qur’an 6:12].

Pia, Allah anasema: “Na ni vyake vilivyotulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.” [Qur’an, 6:13].

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akiwafundisha Maswahaba zake kusema wakati wa kutoa Shahada: “Ewe Mola! Hakika mimi ni mja wako, na mwana wa mja wako (Adam), na mwana mja wako (Hawa), uamuzi wako wa haki ulishapita kwangu.”

Wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipokuwa kwa haki.” [Qur’an, 6:151].

Kwa maana hiyo! Kwa kuwa nafsi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hakuna yoyote aliye na haki ya kuifanyia uonevu au kuhatarisha uhai hata kama atakuwa ni mtu mwenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni.” [Qur’an, 4:29].

Na Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msiwaue wanenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni hatia kubwa.” [Qur’an, 17:31]. Mtu anayewafanyia uadui viumbe wa Mwenyezi Mungu, kwa hakika atakumbana na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na mwenye kumuua Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.” [Qur’an, 4:93].

Na anasema: “Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni. Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhalimu, basi huyo tutamwingiza Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.” [Qur’an, 4:29-30]

Siku moja, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa ameshika pazia la Ka’aba na huku ananong’ona kwa kusema: “Uzuri na harufu nzuri ilioje ulionayo! Utukufu na utakatifu ulioje uliokuwa nao! Ninaapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad ipo mikononi mwake, heshima, mali na damu ya Muislamu ina hadhi kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko wewe (Ka’aba). Na hatuna tunachodhani isipokuwa heri.”

Heshima hii ya kulinda mali na nafsi haikomei kwenye nafsi ya Muislamu pakee, bali yaihusu hata nafsi ya asiyekuwa Muislamu (nayo ina haki ya kulindwa), na hairuhusiwi kufanyiwa uadui.

Qur’an imekusanya na kusheheni Aya za aina hii. Kwa mfano, Mwenyezi Mungu anasema: “Wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipokuwa kwa haki.” [Qur’an, 6:151].

Neno nafsi katika Aya hii limekuja katika mfumo jumuishi, yaani linajumuisha nafsi zote bila kuangalia dini. Japo zipo baadhi ya Hadithi zilizotaja nafsi ya Muislamu pekee, zipo pia Hadithi nyingine zilizotaja kwa umahasusi nafsi za wasiokuwa Waislamu. Mathalan, Imam Abuu Daud anasimulia kwa sanad yake kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anasema: “Zindukeni kuwa, mtu anayemdhulumu anayeishi kwa ahadi, au kumpunja haki yake, au akampa kazi zaidi ya uwezo wake, au akachukuwa kitu chake bila ya ridhaa yake, mimi nitapambana naye Siku ya Kiyama.”

Na Imam Bukhari anasimulia kutoka kwa Abdallah bin Umar kuwa, Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) anasema: “Mtu aliyemuua anayeishi kwa mkataba, hatoinusa harufu ya pepo, na harufu ya pepo hupatikana katika umbali wa mwendo wa miaka 40.

Kwa upande mwingine, ukiangalia utukufu wa mali ya asiyekuwa Muislamu, tunakuta Mwenyezi Mungu amempambia mwanadamu kupenda na kujilimbikizia mali, na akaifanya mali kuwa ni pambo na anasa ya dunia. Mwenyezi Mungu anasema: “Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayobakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini.” [Qur’an,18:46].

Vilevile, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Kwa hakika mali bora ni ile iliyo kwa mtu mwema.” Mwenyezi Mungu ameharamisha wizi na akaweka adhabu ya mwizi, kwa lengo la kulinda mali za watu. Mwenyezi Mungu anasema:
Na mwizi mwanaume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyoyachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.” [Qur’an, 5:38].

Adhabu hii inaijumuisha mali ya Muislamu na asiyekuwa Muislamu, pia hata ikiwa imepatikana kwa njia ya haramu, utapeli, udanganyifu au madhara. Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Msiliane mali kati yenu kwa dhuluma, isipokuwa itakapokuwa biashara mliyoridhiana. Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemu.” [Qur’an 5:29]. Naye Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu anayetulaghai si katika sisi.”

Yote haya ni kwa sababu ya kuuweka muonekano mwema wa Uislamu kwa wasiokuwa Waislamu ili wasije kusema kuwa, Dini ya Kiislamu haina utaratibu wa kulinda mali na damu za wasiokuwa Waislamu.

Hakika zimekuja Aya na Hadithi kadhaa kutoa msisitizo wa mambo yaliyoharamishwa. Zaidi ya hayo, Qur’an ikaeleza wazi kuhusu suala la kuwatendea wema wasiokuwa Waislamu ambao hawana madhara wala uadui dhidi ya Waislamu. Mwenyezi Mungu anasema: “Mwenyezi Mungu hawakatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakupigeni vita, wala hawakutoeni kwenye majumba yenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.” [Qur’an 60: 8].

Mwisho, Mtume (rehema za Allah na amani zishukie) anasema katika maelezo yake yanayowajumuisha watu wote: “Watu wenye huruma watahurumiwa na Mwenyezi Mungu. Wahurumieni walio ardhini nanyi mtahurumiwa na aliye mbinguni.”

Kila Muislamu ana wajibu wa kulinda mambo haya. Muislamu asilifanye suala la kulinda mali na damu kuwa ni la dini kwani Qur’an na Sunna vinaonesha kuwa, suala la kulinda mali na damu linamhusu kila mtu.

Muhimu ifahamike, hakuna haki ya kufanya uharibifu kwenye haki za wengine. Waislamu wanatakiwa na Uislamu wachukue dhamana ya kulinda na kuhifadhi damu na mali za watu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close