1. Tujikumbushe

Utukufu wa Ustaarabu wa Kiislamu

Utukufu wa dini ya Kiislamu na ustaarabu wake unadhihirika kwa namna mbalimbali. Ustaarabu na utukufu huu unaifanya dini hii adhimu iwe ya sifa za kipekee zinazopambanua na dini nyinginezo.

Awali ya yote, Uislamu ni dini iliyoteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia vyanzo viwili vikuu: Qur’an na Sunna. Vyanzo hivi viwili vinaongoza wanadamu wote kwenye njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ameisifu dini hii kuwa ni kuwa yatokana na Yeye Mwenyewe.

Ushahidi wa hili ni kauli yake Allah Ta’ala: “Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na waliopewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu” [Qur’an, 3:19].

Dini ya viumbe wote, ya kimataifa

Pia, Uislamu ni dini ya wote, kwa maana haikukusudiwa kundi maalumu la watu au wala haikukusudiwa kutoa mafunzo mahsusi. Uislamu unaalika viumbe wote, wanadamu na majini, na kutoa muongozo wa maisha ya duniani kwa ajili ya maandalizi ya maisha ya Akhera.

Allah Ta’ala anasema: “Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyoogopa kwa yale yaliyomo humo. Na watasema, ‘Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika?’ Na watayakuta yote waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote” [Qur’an, 18:49].

Vilevile, Uislamu ni dini ya kimataifa iliyoenea kote ulimwenguni. Ujumbe wa Uislamu hauishii katika enzi fulani, kizazi fulani wala mahala maalum. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesifiwa katika Qur’an kuwa ni rehma kwa ulimwengu, kama ilivyokuja katika kauli ya Allah Aliyetukuka:

“Ametukuka aliyeteremsha Furqan kwa mja wake ili awe muonyaji kwa walimwengu wote.” [Qur’an, 25:1].

Dini ya kimaumbile, uwastani

Uislamu vilevile ni dini ya kimaumbile. Kila mtu huzaliwa akiwa Muislamu kisha wazazi humshawishi ajiunge na dini nyinginezo, kama ilivyoelezwa katika Qur’an Tukufu:

“Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.” [Qur’an, 30:30].

Kadhalika, Uislamu ni dini ya uwastani au ukatinakati. Maana yake ni kuwa mafunzo na misingi ya dini hii yanazingatia uwastani na sio misimamo mikali. Pia, dini hii huzingatia wepesi, upole na hupinga upendeleo wowote.

Ukatinakati umesisitizwa katika aya kadhaa na hadith nyingi za Mtume. Mfano, Mwenyezi Mungu anasema:

“Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa Wastani ili muwe Mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni Shahidi juu yenu” [Qur’an, 2:143].

Dini ya tabia njema

Uislamu ni dini ya tabia njema na maadili. Hivyo, haishangazi kwamba imani ya mja inakamilika kwa kuwa na tabia njema katika mambo yote na hali zote.

 Licha ya kuwa ni sababu ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, tabia njema pia ni msingi wa kheri za Dunia na Akhera. Pia, Mwenyezi Mungu Akamsifu Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa kusema:

“Na hakika, Wewe una tabia tukufu.” [Qur’an, 68:4]. Naye Mtume alielezea lengo kuu la utume wake kwa kusema: “Hakika nimetumwa kukamilisha tabia njema.”

Vilevile, Qur’an Tukufu inahimiza sifa na tabia njema na kusimulia visa kadha vinavyoonesha utukufu wa tabia njema. Miongoni mwa tabia hizo ni ushujaa wa Nabii Musa (amani imshukie) na nguvu zake katika kupambania haki.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na alipoyafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema, ‘Mna nini?’ Wakasema, ‘Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana.’ Basi Musa akawanyweshea kisha akarudi kivulini, na akasema, ‘Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitajiwa kheri utakayo niteremshia.’

Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema:

‘Baba yangu anakuita akulipe ujira wa kutunyweshea.’ Basi alipomjia na kumsimulia visa vyake, alisema, ‘Usiogope; umekwishaokoka kwenye watu madhalimu’ Akasema mmoja katika wale wanawake: ‘Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu’” [Qur’an, 28: 23-26].

Kwa kifupi, ustaarabu wa Kiislamu una sifa maalum zinazoufanya udumu katika uzuri wake tangu enzi za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) mpaka Allah Atakaporithi ardhi na yaliyomo juu yake. Ustaarabu huu umedumu katika misingi imara na kuvuka vikwazo vyovyote.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close