1. Tujikumbushe

Unawafahamu wahadhiri wa Misk ya Roho 2019?…

Pata kujua wasifu wa kila mmoja wao…

Tukielekea kongamano la tatu la Afrika Mashariki lijulikanalo kama Misk ya roho 2019, kwa umuhimu wa kipekee kabisa napenda leo niwatambulishe kwenu kwa wasifu wao wahadhiri watakaopata nafasi ya kutuwaidhi katika kongmano la Misk ya Roho mwaka huu.

Kwa tawfiqi yake Allah katika msimu huu wa tatu wa Misk ya Roho yaani Misk ya Roho 2019, In shaa Allah tutakuwa na masheikh saba kama walivyotajwa katika matoleo ya awali ya gazeti hili, masheikh hao ni; kutoka Rwanda ni Sheikh Djumapili Mbabajende, kutoka Burundi ni Sheikh Zuberi Bizimana, kutoka Uganda ni Sheikh Muhammad Abduweli, kutoka Kenya kutakuwa na masheikh wawili ambao ni Sheikh Yusuf Abdi na Sheikh Abubakar Abdi (Abu Hamza) na kutoka Tanzania ni Sheikh masheikh wawili ambao ni Sheikh Ibrahim Twaha na Dk. Sheikh Salim Qahtwan.

Fuatana nami kuweza kuwafahamu masheikh hawa kwa kupitia wasifu wa kila mmoja wao ili kujua kwa ufupi historia zao.

Sheikh Djumapili Mbabajende

Alizaliwa katika jiji la Kigali nchini Rwanda, alianza kusoma dini na kufanya daawah akiwa na umri mdogo sana. Miongoni mwa makhatibu wanaotegemewa katika miskiti mingi nchini Rwanda kote. Alisoma elimu ya msingi ya dini akiwa mdogo sana, Kisha akajiunga na sekondari ya dini Azhari Sharif na baadae alijiunga kitivo cha masomo ya kiislamu na lugha ya kiarabu katika chuo cha Azhar Sharif nchini Misri.

Sheikh Zuberi Bizimana

Alizaliwa Buyenzi, jijini Bujumbura nchini Burundi. Kutokana na mapenzi yake ya Elimu ya dini ya Kiislamu alipata nafasi ya kusoma shule ya msingi Madrasatul Husein Buyenzi kisha akajiunga na elimu ya sekondari Madrasatut Tahdhibu Bwiza na baadae alijiunga na kitivo cha shariah katika chuo kikuu cha Kiislam cha Muhammad Ibn Saudi nchini Saudi Arabia. Ana shahada ya sharia pia anaweza  kusoma, kuandika na kuzungumza lugha za Kirundi, Kiarabu, Kiingereza na Kiswahili.

Sheikh Muhammad Abduweli

Sheikh Muhammad Abduweli ni mzawa na mkazi wa Uganda, ni miongoni mwa wasomi vijana wachache waliotenga muda wao kuihudumia dini ya kiislamu. Mhitimu wa shahada katika kitivo cha Hadithi, chuo kikuu cha kiislamu Madina nchini Saudi Arabia, alisoma shahada ya uzamili ya sayansi ya hadithi,nchini Sudan, ni mkufunzi wa chuo kikuu cha kiislamu Uganda na pia ni imamu na khatibu masjid Tawhid Kampala Uganda.

Sheikh Yusuf Abdi

Alifunzwa Qur’an na kuhitimu akiwa na miaka 7 alianza kuhutubu akiwa na umri wa miaka 14, alikuwa makini na kufanya vizuri katika masomo yake ya dini. Baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari alielekea nchini Sudan kusoma msingi wa Dini, ni mfano wa kuigwa na mmoja wa wahamasishaji wakubwa wa vijana Afrika ya Mashariki. Anapenda kusafiri na kujifunza kutokana na safari hizo. Amekuwa Khatibu na Imam katika misikiti mingi huko nyuma, ni muasisi wa mfumo mpya wa nasheed Afrika Mashariki, mtunzi wa mashairi na mbunifu wa lahani pia ni muasisi wa studio ya Sauti Afrika.

Sheikh Abubakar Abdi (Abu Hamza)

Ni mzaliwa na mkazi wa Mombasa Kenya, alianza kufanya daawah tangu akiwa bado mwanafunzi mwaka 1979. Alisoma elimu ya msingi Mahad Thaqaafa, akasoma elimu ya sekondari (thanawi) Madrasatun Najah na baadae akasoma elimu ya chuo kikuu Jamiatul Imam, Riyadh nchini Saudi Arabia. Aliwahi kuwa Mudir idara ya daawah katika taasisi ya  Muntada Al-Islaamiya kwa miaka 11 (Kuanzia 1989-2000), ni mwalimu Madrasatul Hudaa Tchundwa kuanzia mwaka 1985-1989, Muwakilishi wa Majlis ya Maulamaa Kenya tangu mwaka 2000, Ni mshauri wa walimu MEC tangu mwaka 2000 pia ni Mwandishi wa kitabu cha Malezi Mazuri.

Sheikh Ibrahim Twaha

Alizaliwa mkoani Mbeya nchini Tanzania, ni mmoja kati ya viongozi waandamizi wa taasisi ya The Islamic Foundation. Pia ni daa’i wa muda mrefu, khatibu na Imamu mkuu wa Masjid Haqq mkoani Morogoro. Alianza kufanya kazi The Islamic Foundation kama Imamu na baadae mwaka 2008 akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya yatima, Baadae akachaguliwa kuwa kaimu mkurugenzi wa Idara ya Daawah ya The Islamic Foundation, Kisha mwaka 2011 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu (General Secretary) wa The Islamic Foundation na sasa ni Mkurugenzi mtendaji (Managing Director) wa The Islamic Foundation.

Dk. Sheikh Salim Qahtwan

Alizaliwa Mnyanjani Tanga Tanzania, alisoma elimu ya msingi ya dini Madrasatul Fauzia, ngazi ya sekondari Maahadul Faaruq na baadae alisoma sekondari ya juu (Advanced Level) Maahadul Imam Shafii, kisha alielekea Nchini Sudan katika chuo kikuu cha Undhurman ambapo alisoma shahada ya kwanza (Degree) na ya uzamili (Masters) na baadae alisoma shahada ya uzamivu (PhD) katika fani ya sharia chuo kikuu cha Inar nchini Sudan katika fani ya sharia. Alipata kuwa Mwalimu na Afisa taaluma katika taasisi ya Ansaar Muslim Youth Centre, ni mwalimu wa dini katika taasisi ya Al-Muntada, mratibu wa mkoa Jamaatul Akhlaaq Islamiyya (JAI) na pia ni afisa taaluma wa African Muslim Agency.

Ni matumaini yangu kuwa utakuawa umestafidi kwa kuwajua wahadhiri wetu wa Misk ya Roho mwaka huu. Ni wasomi na weledi ambao hutatamani kuwakosa, kwa ujumla tunasema kukosa kongamano hili ni kuidhulumu nafsi yako. Jipatie tiketi yako mapema katika vituo vilivyoainishwa ili kuweza kuhudhuria kongamano hili.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close