1. Tujikumbushe

Ulimi unapokuwa kiungo cha shari

“Mwanadamu anapoamka (asubuhi), viungo vyake vyote vinaulaumu ulimi vikisema, Mche Allah kwetu (ewe ulimi) kwani sisi tuko katika hifadhi yako. (Wewe) ukiimarika nasi tutaimarika na ukienda kombo nasi tutakwenda kombo.” [Ahmad na Tirmidhi].

Maneno niliyoyanukuu hapo juu ni mafundisho ya Mtume Muhammad (rehema na amani ya Mwenyezi Mungu imfikie) kuhusu umuhimu wa kuchunga (kuhifadhi) ulimi. Pamoja na faida nyingi tunazoweza kuzipata kupitia ulimi, kiungo hiki kinapotumiwa bila tahadhari madhara yake huwa ni makubwa mno.

Yawezekana jamii iliyomzunguka mtu ikafaidika na maneno yake au ikawa inakerwa na kukwazwa na maneno ya mtu huyo. Mtu mwerevu ni yule ambaye anauhifadhi ulimi wake, mwingi wa kunyamaza na akizungumza anazungumza maneno mazuri yenye faida kwake na kwa watu wengine.

Mmoja kati ya wema waliopita aliwahi kusema: “Mtu anapohifadhi sikio lake ni kwa faida yake mwenyewe na anapohifadhi ulimi wake inakuwa ni kwa faida yake na ya watu wengine.”

Mwema huyu alimaanisha kuwa, unachokisikia kinakufaidisha au kukudhuru mwenyewe ila unachokisema huenda kikagusa watu wengine.

Allah Aliyetukuka ametubainishia faida ya ulimi na maafa yake pale aliposema: “Je, huoni jinsi Allah alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Allah huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka. Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, uliong’olewa juu ya ardhi. Haupo imara.” [Qur’an, 14: 24–26].

Maneno yenye manufaa yananufaisha dunia na akhera na maneno mabaya yanaharibu dunia na akhera. Amebainisha Allah kuwa kujiweka mbali na maneno yasiyofaa ni katika alama za uzuri wa imani ya mja na ni sifa ya waja wema wa Allah. Qur’ an inasema:

“Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa heshima yao.” [Qur’an, 25:72].

Kujiweka mbali na mambo na vikao vya kipuuzi hupelekea kusalimika na madhara mengi yanayosababishwa na ulimi. Allah anatufahamisha kupitia aya mbalimbali namna ya kuchunga ndimi zetu. Anasema:

“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa. (Mwenyezi Mungu) atakutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi yenu. Na anayemtii Allah na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.” [Qur’an, 33:70–71].

Kila anachotamka mwanadamu kinaandikwa, na mbele ya Allah kitadhihirishwa. Vile vile, kila mtu atayakuta yale aliyoyatanguliza mwenyewe kwa viungo vyake. Kubwa zaidi ni kuwa viungo hivi hivi ndiyo vitamshuhudia mtu kutokana na yale anayoyafanya hapa duniani na ulimi ukiwa miongoni mwa viungo hivyo.

Allah anasema: “Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiyatenda. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye haki iliyo wazi.” [24: 24–25].

Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) ametupa muongozo wa kutusaidia na mbinu ya kuhifadhi ndimi zetu aliposema:

“Yeyote anayemwamini Allah na siku ya mwisho azungumze maneno mazuri au anyamaze.” [Bukhari na Muslim].

Mtu akikosa la kuzungumza ni bora anyamaze kwani hiyo itakuwa ni kheri kubwa kwake na atasalimika kutokana na madhara ya ulimi. Si kila unalolijua yafaa kulizungumza. Wakati mwingine ni vema kuacha maneno mengi hata katika mambo unayoyajua kuwa ni ya kweli.

Swahaba Ali bin Abi Twalib (Allah awe radhi naye) amesema:

“Wasemesheni watu kwa yale wanayoyafahamu. Hivi mnapenda akadhibishwe Allah na Mtume wake?”

Yawezekana ukazungumza maneno ambayo yana ukweli lakini kwa namna ulivyoyazungumza ukawa umesababisha fitina na matatizo makubwa kuliko ulichokusudia kukizungumzia. Abdullahi Ibn Masoud amesema:

“Hutawasemesha watu maneno yasiyofika katika akili zao isipokuwa yatakuwa fitina kwa baadhi yao.” [Muslim].

Hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anazuia ulimi wake na kuuhifadhi kutokana na kila uovu katika nyakati zote na hali zote. Tabia ya binadamu ni kupenda kuzungumza sana na wakati mwingine huzungumza bila umakini na kutozingatia anachokisema.

Binadamu hueneza habari zote anazozisikia bila hata kuzichunguza na kuthibitisha ukweli wake. Imam Ibnu Al–Jawziy amesema:

“Katika maajabu ni kuwa ni rahisi zaidi kwa mwanadamu kujilinda na haramu, dhuluma, uzinifu, wizi, kunywa pombe na mengineyo; lakini inakuwa vigumu kwake kulinda ulimi wake. Wakati mwingine unaweza kumkuta mtu anaashiriwa vidole kwa mema na uchamungu huku anazungumza maneno ya kumchukiza Allah pasina kujali.”

Naye Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) alipata kuulizwa, ni kitu kitakachowaingiza watu motoni kwa wingi? Akasema ni mdomo (ulimi) na utupu.” Kwa hiyo, ulimi ni kiungo chenye makosa makubwa na yenye madhara makubwa kwa watu, ikiwamo kusema uongo, kusengenya, kufitinisha na kugombanisha watu.

Yawezekana mtu akapoteza maisha au kufungwa jela miaka kadhaa kutokana na uongo uliosemwa na watu wengine. Pia mtu anaweza kuwagombanisha watu na hata kuwafarikanisha kwa sababu ya ulimi.

Mifano ya kauli mbaya na za kuudhi zinazotolewa na baadh yetu ni nyingi na ndio maana tunajiuliza kama kweli wanafahamu umuhimu wa kuzuia ndimi zao zisinene mabaya. Wengi wetu hawatambui kwamba kadiri wanavyotamka maneno mabaya na ya kuudhi, ndivyo wanavyojiweka katika hatari ya kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu.

Sisi wanadamu tunapaswa kumuogopa Mwenyezi Mungu na kuchunga ndimi zetu ili tufaulu siku ya malipo. Mungu anasema:

“Hii (siku ya Kiyama) ndiyo siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Allah amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.” [Qur’an, 5:119].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close