1. Tujikumbushe

Tuwakumbuke yatima, wajane na maskini Ramadhan hii

Tumeusiwa kuwasaidia yatima, wajane na wenye uhitaji ili waweze kukidhi mahitaji yao muhimu. Matajiri na watu wengine wanapaswa kurejesha kwa Mungu sehemu ya mapato yao (sadaka na zaka) kusaidia watu hawa wenye uhitaji.

Kijamii, kuwasaidia yatima na wenye uhitaji hupelekea kulinda heshima zao, kuunganisha nyoyo na kutia nguvu maelewano ya watu. Nafsi zimeumbwa kuwapenda wale wanaozifanyia wema na kuwachukia wale wanaozifanyia ubaya. Moja kati ya ubaya, ni masikini kuwaonea husda matajiri; kwa upande wa pili, matajiri kuwadharau na masikini.

Kuwasaidia masikini ni mojawapo ya njia ya kupata mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ni sehemu ya wema (ihsani). Watu wanaojitolea katika njia za kheri watapata mwisho mwema kwa sababu ya kuwahurumia, kuwafurahisha na kuwajali waja wa Allah.

Kwa kufanya hivyo, wao hupata huruma na mapenzi makubwa ya Allah. Vile vile, kujitolea kunapelekea kupata ziada ya kheri na baraka nyingi, na pia ni sababu ya kupata kivuli cha Allah katika siku ambayo haitakuwa na kivuli ila kivuli cha Allah.

Miongoni mwa fadhila za kutoa ni kupata badala (ya kile ulichotoa) kutoka kwa Allah pamoja na dua ya Malaika kila siku. Allah Aliyetuka anasema:

“Sema, ‘Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakachokitoa yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanaoruzuku.” [Qur’an, 34:39].

Na katika hadithi, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anatuambia:

“Hakuna siku ambayo hupambazukiwa waja isipokuwa malaika wawili huteremka. Mmoja wao husema, ‘Ewe Mola mpe badala mwenye kutoa.’ Na mwingine husema, ‘Mpe uharibifu mwenye kuzuia.” [Bukhari na Muslim].

Aya na hadithi vinaonesha kuwa mwenye kutoa anapata badala ya hicho alichokitoa. Na Allah kwa ukarimu wake hutoa ziada kwa watu wenye kuwafanyia wema waja wake. Kimsingi, Muislamu anatakiwa kuondoa hofu ya kupungukiwa mali (kufilisika) ili akamilishe dhana ya uchamungu ambayo ndiyo sababu ya kufaradhishwa funga ya Ramadhan.

kujitolea, tiba ya choyo, ubahili

Katika jamii ya leo iliyokumbwa na maradhi ya choyo na ubahili, Waislamu, kwa kutumia ibada ya kujitolea, ndiyo wenye nafasi ya kutibu maradhi hayo. Lakini huenda Waislamu wengi hawalijui hili kwa undani wake.

Bahati nzuri, huu ni msimu wa Ramadhan ambao pamoja na mambo mengine tunapaswa kuutumia katika kuwakirimu watu kwa namna atakayotuwezesha Mwenyezi Mungu. Ni jukumu letu kuwajali na kuwahudumia masikini, yatima, wajane na wenye shida ili na wao waweze kutimiza ibada ya funga kwa utulivu.

Mwenye uwezo wa kumsaidia mtu mmoja, wawili au watatu kupata futari afanye hivyo kwa lengo la kutafuta radhi za Allah, na si kwa ria au kujionesha. Pia, ni muhimu kwa waajiri kuwafanyia ukarimu wafanyakazi wao kwa kuwapa mahitaji muhimu ya futari na mengineyo.

Mtume wetu (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa karimu mno ndani ya Ramadhan, hivyo nasi tunatakiwa tumuige kwani yeye ndiye kigezo chema, kama Allah anavyothibitisha:

“Hakika nyinyi mnacho kigezo chema kwa Mtume wa Allah kwa anayemtaraji Allah na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allah sana.” [Qur’an, 33: 21].

Ramadhan ni mwezi wa kujenga uhusiano mwema wa kiroho na kijamii kwa marafiki, majirani, familia na wafanyakazi. Tueneze hisia za ukarimu kwa kila mtu kwani ukarimu ni jambo linalopenya kwa urahisi mno katika nyoyo za watu.

Waislamu tunapaswa kutumia fursa ya mwezi wa Ramadhan kuzirejesha nyoyo zetu katika ukarimu kama ule uliooneshwa na wazee wetu. Endapo tutapuuzia jambo hili la kuwasaidia wengine, tutakuwa tumepoteza tunu muhimu mno katika maisha yetu ya kidini na kijamii.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close