1. Tujikumbushe

Tusake pesa lakini tusichupe mipaka

Kwa muda mrefu, watu wengi hususan vijana wamekuwa wakihamasishwa kushiriki michezo ya kubahatisha (kamari) kupitia vyombo vya habari. Kadri watu wengi zaidi wanavyoshiriki michezo hiyo ndivyo vyombo hivyo vya habari vinavyopata mgao wa matangazo kutoka kampuni za kamari.

Kwa hapa Tanzania, michezo ya kamari maarufu ‘Jackpot’ imepamba moto huku washiriki wa michezo hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kupata utajiri wa haraka. Wapo waliotangazwa kuwa wameshinda nyumba, pikipiki na pesa taslimu kupitia droo zinazoendeshwa na kampuni za michezo ya kubahatisha.

Kampuni nyingi za michezo ya kamari zilianzishwa miaka sita iliyopita jambo ambalo limepelekea watu wengi kujitumbukiza kwenye michezo hiyo haramu kidini.

Tamaa ya kupata utajiri wa haraka imewafanya watu wengi zaidi, hasa vijana, ambao ni nguvu kazi ya taifa kushawishika kucheza kamari kupitia simu zao za mkononi. Watu wengi huamini kuwa siku moja watashinda fedha nyingi zitakazowawezesha kujikwamua na umasikini, jambo ambalo ni nadra kutokea.

Utafiti

Utafiti uliofanywa miaka ya karibuni na kampuni ya GeoPoll ya Marekani, ambayo ina ofisi zake za kanda ya Afrika jijini Nairobi unaonesha kuwa, katika bara la Afrika, nchi ya Kenya ndiyo inayoongoza kwa kucheza kamari, ambapo asilimia 75 ya Wakenya walio na umri wa chini ya miaka 35 wamewahi kucheza kamari. Utafiti huo pia umeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa vijana wake kucheza kamari kupitia simu zao za mkononi.

Kutokana na faida wanazozipata wachezeshaji, serikali nazo zimeamua kujipatia kodi kupitia michezo hiyo. Mathalan, nchini Kenya kampuni ya kamari hutozwa kodi ya asilimia 30 ya mapato yake. Katika bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali ya Kenya iliongeza kodi nyingine ya asilimia kumi kwa kila fedha iliyowekwa kama kamari ama dau.

Hii ina maana kwamba, mchezaji wa kamari atatozwa hata kabla hajashinda chochote.

Tatizo ni umasikini

Kushamiri kwa michezo ya kubahatisha Afrika Mashariki kumesababisha kampuni nyingi za kamari kuibuka.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na taasisi ya Economic Policy Research Centre (EPRC), yenye makao yake makuu mjini Kampala nchini Uganda umefichua kuwa, wengi wa wanaoshiriki michezo ya kamari walifanya hivyo kwa lengo la kujipatia kipato, kujikimu kimaisha na si kwa sababau za starehe.

Utafiti huo ulibaini kuwa, asilimia 45 ya wanaume walio na umri wa kati ya miaka 18 hadi 30 walijihusisha zaidi na aina fulani ya kamari. Utafiti huo pia umebaini kuwa, watu wanaocheza kamari kwa lengo la kukabiliana na umasikini wana uwezekano mkubwa wa kuwa waraibu kuliko wale wanaocheza kwa starehe.

Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa watu wanaocheza kamari, wanatumia takriban asilimia 12 ya mishahara yao kila mwezi katika michezo ya kubahatisha.

Athari kwa vijana

Biashara ya kamari ambayo inakua kwa kasi kubwa, inatajwa kuathiri maisha ya vijana wengi ambao wamekuwa masikini baada ya kupoteza fedha nyingi katika michezo ya kubahatisha.

Tatizo kubwa ambalo linawakabili vijana wengi ni kwamba hawataki kufikiria kujiajiri. Michezo ya kubahatisha imezifanya akili zao kushindwa kutafakari kwa kina juu ya namna ya kujikwamua na umasikini. Wanachowaza wao, ni kupata fedha za haraka pasina kufanya kazi.

Serikali zote duniani zinaelewa vyema maovu yote yanayotokana na michezo ya kubahatisha, lakini haziko tayari kupiga marufuku michezo hiyo. Hii inatokana na ukweli kwamba michezo ya kubahatisha ni kati ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.

Kushamiri kwa michezo ya kamari nchini, ni zao la mfumo wa uchumi wa kibepari ambao unavuna pesa nyingi kwa njia haramu ya kuwanyonya watu masikini, ambao pesa zao huchezeshwa kwa kutumia namba za bahati. Wanacheza maelfu, anashinda mmoja.

Kisha vyombo vya habari vinamtangaza mshindi ili kuwatia mshawasha wengine wacheze zaidi wakitegemea kubahatika kumbe wanapoteza fedha na kulaaniwa.

Uislamu na michezo ya kubahatisha

Katika dini ya Kiislamu, michezo ya kamari imeharamishwa kama Allah anavyosema ndani ya Qur’an [5:90]:

“Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa.”

Lakini katika dunia ya sasa, kamari imefanywa kuwa biashara na mtaji wa kuzalisha pesa. Jambo la kusikitisha ni kuwa miongoni mwa washiriki wakubwa wa michezo ya kubahatisha ni Waislamu.

Ushahidi mkubwa unaothibitisha kuwa Waislamu wanacheza michezo ya kubahatisha unapatikana katika majina ya washindi wanaotangazwa kila siku kwenye vyombo vya habari, ambapo kuna majina mengi tu yanayoashiria kuwa washindi hao ni Waislamu.

Ukiacha wachezaji, kuna kundi la wahamasishaji wa michezo hiyo, ambao baadhi yao ni vijana watangazaji maarufu wa redio na televisheni. Katika vipindi vyao mbalimbali, utawasikia vijana hao wakisifu na kuhimiza watu kucheza michezo ya kubahatisha inayotokana na kampuni zilizowaajiri.

Vijana hawa wa Kiislamu wamesahau kabisa kuwa dini yao imeharamisha kamari. Wanadamu hususan Waislamu wanatakiwa wajitahidi kutafuta riziki kwa mujibu wa muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie).

Huo ndio msimamo wa Muislamu anayekubali kwamba riziki iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake. Allah anasema kuhusu riziki:

“Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa njia asiyoitarajia. Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake.” [Qur’an, 65:2–3].

“Na hakuna mnyama yeyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha.” [Qur’an, 11:6].

Kwa sababu hiyo, tunapaswa kutafuta riziki kwa mujibu wa muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie).

Muislamu anatakiwa kufanya kazi ya halali ili kujipatia riziki kwa kuchunga mipaka aliyoiweka Mwenyezi Mungu. Kulingana na maelezo hapo juu, Muislamu anatakiwa atafute kipato kwa njia za halali kwa sababu kilicho haramu kwa mtu binafsi, pia ni haramu kwa familia na jamii nzima.

Uislamu umeweka utaratibu maalumu wa kutafuta kipato, ambapo kila mtu anao uhuru wa kuzalisha mali ya kutosha kukidhi mahitaji yake binafsi na familia. Hii ni kwa sababu, Uislamu una mfumo wake wa kiuchumi uliokamilika, ambapo kila Muislamu anawajibika kuchuma kulingana na mfumo huo.

Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa [Qur’an, 5:90].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close