1. Tujikumbushe

Tujiandae kuhudhuria kongamano la Misk ya Roho Desemba mosi

Zimebaki siku 5 hadi kufanyika Kongamano kubwa la Kidaawa la Afrika Mashariki linaloandaliwa na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yenye makao yake makuu mjini Morogoro, Tanzania.

Kongamano hilo linalofanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo, linatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili Desemba mosi, 2019 katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo Masheikh saba kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda watawasilisha mada.

Ama kwa hakika Misk ya Roho ni kongamano muhimu kulifuatilia kwa Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu. Tunasema, ni tukio kubwa kutokana na elimu na uzoefu wa Masheikh hawo katika kuchambua masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa katika muktadha wa dini .

Hivyo twaona, kongamano la Misk ya Roho lina umuhimu na faida kubwa kwa Waislamu a hata wasio Waislamu kwani litawawezesha kujifunza dini yao.

Waislamu tusichezee fursa hii muhimu bali tujitokeze kwa wingi ili kuwasikiliza Masheikh zetu kwani ili tufanikiwe duniani na Akhera tunahitaji uelewa mzuri na sahihi wa dini na hamasa ya kutekeleza tunayojifunza.

Mbali na hayo, jamii ya Kiislamu hapa Afrika Mashariki na duniani kote inapitia kipindi kigumu, hivyo kuwasikiliza Masheikh hao kutatoa mwanga mzuri juu ya hatua gani za kuchukua ili kuhakikisha tunapambana na changamoto zinazotukabili.

Itakuwa ni unyimi wa fadhila kama tutamaliza tahariri hii bila kuipongeza Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) kwa kazi hii kubwa ya kuratibu kongamano hili. Hongera TIF, hongera viongozi wa TIF.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema, katika jamii ni muhmu liwepo kundi, hususani la Wanazuoni, japo wachache, ambalo litakuwa likifanya kazi ya kuwaamrisha watu mema na kuwakataza maovu.

Kwa hali hiyo, TIF wanafanyia kazi kwa vitendo kauli ya Allah Mtukufu inayosema: “Na iwe miongoni mwenu kundi linalolingania katika kheri, wanaamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio waliofanikiwa …,” [Qur’an, 3:104].

Mwisho tunatoa pongezi kwa taasisi na kampuni zote zinazojitolea kufadhili tukio hili adhimu. Kwani kwa kitendo chao hicho, wanakuwa wanachangia katika kuuendeleza Uislamu. Allah awalipe kheri.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close