1. Tujikumbushe

Tuhuishe ustaarabu wa kutoleana salamu

Katika ulimwengu wa wasomi, Uislamu unatajwa kama dini ya amani, upendo, utulivu na ustaarabu. Hata hivyo, kwa hali ilivyo sasa na kama hatua za makusudi hazitachukuliwa, kazi iliyofanywa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na wale waliofuata mwenendo wake itapotea na hatimaye kujikuta tumepoteza heshima na ustaarabu wetu mbele ya jamii.

Si hivyo tu, pia tutakuwa watu wasio na mwelekeo na fahari juu ya Mtume wetu. Nasema hivyo kwa sababu, ustaarabu ndiyo unaoipa jamii utambulisho. Sura na haiba ya jamii huweza kueleweka na kuelezeka kirahisi kutokana na ustaarabu wa watu wake.

Ustaarabu humuwezesha mtu kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake.

Ustaarabu wa Kiislamu

Ustaarabu wa Kiislamu ni wasifu wa ziada wa uwepo kwa utamaduni wa kijamii ambao unabeba maana halisi ya maendeleo. Ndiyo kusema kwamba, mafanikio yasiyojengwa katika misingi ya ustaarabu wa Kiislamu ni mafanikio yasiyokuwa na tija.

Lengo kuu la ustaarabu wa Kiislamu si tu kufanikisha utulivu, usalama na amani na kupiga vita maovu, bali pia kuwapa watu fursa ya kuchagua aina ya maisha inayowapa uhalali, furaha na raha ya kuwa binadamu katika jamii yao.

Historia ya Uislamu inaonyesha jinsi Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie) walivyojitahidi kuhuisha ustaarabu wa kutoleana salamu. Katika zama za Mtume, ubora wa watu ulipimwa kwa kutoleana salamu. Suala hili lilipewa kipaumbele cha kwanza katika miji yote iliyokuwa chini ya Dola ya Kiislamu. Mantiki yake ilitokana na ukweli kwamba roho ya jamii au taifa ni ustaarabu wake.

Hatua hii ilikuwa na umuhimu mkubwa na wa mfano katika kujenga heshima, fahari, umoja na uzalendo miongoni mwa Waislamu. Tofauti na sisi, Maswahaba wa Mtume (radhi za Allah ziwafikie) walikuwa ni wepesi sana wa kutekeleza mafundisho ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) pale anapotoa maagizo yoyote.

Katika kulifanyia kazi agizo la kutoleana salamu, Maswahaba hawakuwa ni wenye kusubiri mpaka wakutane na watu ili wawatolee salamu bali walikuwa wakiwafuata, kuwajulia hali na kuwatolea salamu.

Tazama namna Abdullah bin Umar (Allah awaridhie) alivyokuwa akilifanyia kazi jambo hili. Kutoka kwa Tufail bin Ubayya bin Kaab (Allah amridhie) amesema kuwa alikuwa akimwendea Abdullah bin Umar (Allah awaridhie), kisha anakwenda sokoni asubuhi pamoja naye.

Tufail akasema, walipofika sokoni wakati huo wa asubuhi, Abdullah alikuwa hapiti kwa muuza bidhaa ndogondogo za hali ya chini, wala mwenye biashara kubwa, wala masikini isipokuwa humtolea salamu.

Tufail akasema: “Siku moja nilimwendea Abdullah bin Umar (Allah amridhie) akanitaka nifuatane naye kwenda sokoni.” Nikamuuliza: “Unakwenda kufanya nini sokoni ilihali wewe husimami kwenye biashara (kununua) wala huulizi bei wala hukai katika mabaraza (vikao) vyovyote?”

Abdullah akasema: “Ewe Abaa Batni (alimuita hivyo kwa sababu Tufail alikuwa na tumbo kubwa). Hakika si vinginevyo, tunakuja hapa mapema kwa ajili ya kutoa salamu, tunamsalimia yule tutakayekutana naye.” [Malik katika Muwatta].

Hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Abdullah (Allah amridhie) akionesha umuhimu wa kutoleana salamu.

Katika kutilia mkazo umuhimu wa kupeana salamu, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anatufundisha kuwa kupeana salamu ni haki ya kila Muislamu.

“Haki za Muislamu kwa Muislamu mwenzake ni sita… (Mtume akataja mojawapo ya haki hizo kuwa ni) unapokutana na nduguyo Muislamu umtolee salamu.” [Bukhari na Muslim].

Allah anatuhimiza kutoleana salamu hasa kutumia salamu iliyo bora zaidi. Anasema:

“Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni Aya zake mpate kuelewa.” [Qur’an, 24:61].

Kutoleana salamu ni sababu ya kupendana kama alivyobainisha Mtume (rehema za Allah na amani ya imshukie).

“Hamtoingia peponi mpaka muamini, na hamuwezi kuamini mpaka mpendane. Je, nikujulisheni jambo ambalo mtakapolifanya mtapendana? Toleaneni salamu baina yenu.” [Muslim].

Muislamu anapokutana na nduguye au anapoingia nyumbani au kazini ni haki awatolee salamu waliomo humo. Uchache wa kusalimia ni kusema:

“Assalamu Alaykum” na ukamilifu ‎wake ni kusema: “Assalamu Alaykum Warahmatu Llahi Wabarakatuh.”

Juu ya hivyo, mwenye kuamkiwa inampasa arudishe maakimizi yaliyo bora zaidi ambayo ni:

“Waalaykumu Salamu Warahmatu Llahi Wabarakatu.”

Katika kulisisitiza hilo, Mwenyezi Mungu anasema: “Na mnapoamkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo (kama mlivyoamkiwa). Hakika Allah ni mwenye kuhesabu kila kitu.” [Qur’an, 4:86].

Hivi ndivyo Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie) walivyohuisha ustaarabu wa kutoleana salamu.

Hivyo, yatupasa tudumu na jambo hili la kusalimiana ili tuweze kufuzu hapa duniani na kesho Akhera. Qur’an inasema:

” Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: ‘Salaamun Alaykum’amani iwe juu yenu! ingieni peponi kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda.” [Qur’an, 16:32].

Pamoja na ukweli huo, wengi wetu tumeshindwa kuipa umuhimu salamu, licha ya faida na manufaa yake kuturejea wenyewe.

Kwa hakika, salamu katika Uislamu ni jambo jema na lenye nafasi kubwa katika kuleta amani, mahaba na mshikamano miongoni mwa wanajamii. Bahati mbaya sana wengi wetu tumeghafilika na suala la kutoleana salamu aidha kutokana na kiburi, uvivu au ubinafsi.

Kando na hao, pia wapo baadhi yetu ambao hawatoi salamu ila kwa watu wanaowajua miongoni mwa ndungu, jamaa ama marafiki zao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close