1. Tujikumbushe

Tufuate haki, tuepuke dhuluma

Duniani kuna makundi mawili ya mambo. Kuna uongofu (haki) na upotovu (batili). Kwa kawaida mihimili hiyo hukinzana wakati wote na haiwezi kuchangamana hata siku moja. Kama mtu amezoea kula mali ya haramu ni vigumu sana kumtoa kwenye mrengo huo. Lakini watu wenye hekima wanajua fika kwamba siku zote haki huibuka mshindi katika vita baina yake na upotovu.

Dhuluma ni moja ya mambo ya upotovu. Inapotokea mtu anamdhulumu mtu mwingine, kuna mambo matatu unayoweza kufanya. Jambo la kwanza ni kumshawishi anayedhulumu aache na kuifuata haki. Kama akikubali basi tatizo la msingi hutatulika kirahisi.

Jambo la pili ni mtu anayedhulumiwa aendelee kudhulumiwa hadi mtu anayedhulumu atakapoona kwamba sasa dhuluma aliyofanya imetosha. Mara nyingi wanaochagua mfumo huu ni wale waliokwama kabisa na hawana njia ya kujinusuru.

Jambo la tatu na la mwisho ni mtu anayedhulumiwa kuamua kujitetea na kutetea haki yake hadi atakapohakikishia inapatikana. Mara nyingi wanaochagua mfumo huu hupita katika tabu nyingi, mateso, maumivu makali, uchungu, bughudha, manyanyaso na kila aina ya shurba. Mfumo huu mara nyingi huleta mabadiliko chanya.

Kimsingi, tunaweza kusema dhuluma inazidi kushamiri kwa sababu ya kuwapo mivutano mikubwa baina ya haki na batili. Hali hii inadhihirika wazi pale nguvu ya kishetani ya batili inapoonekana kushika hatamu katika kuwaongoza wanadamu.

Jamii inayopigia upatu au kuunga mkono dhuluma ni jamii ya watu wajinga, na kupitia ujinga wao huamini kuwa wataendelea kuwapo ulimwenguni. Ama jamii yenye watu wanaojitambua katu hawadhulumu watu kwa sababu wanafahamu huo ni mtego anaoutumia shetani (Iblis aliyelaaniwa) katika kuwanasa wanadamu.

Dhuluma ni jambo litakalowaachia watu mizigo mikubwa ya dhambi siku ya hesabu. Mtume amesema:

“Aliyekuwa na kitu cha dhuluma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham. Ikiwa ana amali njema, basi zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe.” [Bukhari].

Hii inathibitisha kuwa dhuluma ni jambo baya na lenye madhara makubwa duniani na Akhera pia. Mwenyezi Mungu ameweka mipaka na anataka tusiichupe kwani licha ya sharia zake kuwafikiana na mahitaji ya binadamu, sharia hizo zinakataza watu kutafuta mali kwa njia ya ghushi, rushwa na dhuluma.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na wala msiliane mali zenu kwa ubatilifu na mkazipeleka (rushwa) kwa mahakimu ili mle sehemu katika mali ya watu kwa dhambi hali ya kuwa mnajua.” [Qur’an, 2:188]

Vilevile Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuambia:

“Ogopeni dua ya aliyedhulumiwa kwani inapanda mbinguni kama cheche za moto.” [Hakim].

Kwa kuzingatia hayo, Muislamu anatakiwa ajisalimishe katika matakwa ya Allah Muumba na Mtume wake. Hilo ni jambo rahisi mno kwa waumini hasa ikizingaziwa kuwa asili ya mwanadamu ni kupendelea kheri na kuchukia maovu (Nafsi zimeumbwa kupendelea kheri).

Vyovyote iwavyo, kudhulumu haki za watu ni kwenda kinyume na fitra (maumbile ya mwanadamu) na ndio maana kunaleta madhara na maangamizo. Mitume na Manabii (amani iwe juu yao) waliletwa ulimwenguni kwa sababu moja kubwa, nayo ni kuwatoa watu katika giza la upotovu na kuwapeleka kwenye nuru ya uongofu.

Hivyo Muislamu fanya hima urudi katika fitra sahihi na jiepushe na vitendo vya dhuluma, rushwa na ufisadi. Tambua dhuluma ina mwisho wake. Dunia hii uliyopo sasa ni mfano wa kivuli chako; ukisimama husimama, na ukikifuata hukukimbia. Ikiwa walijua hilo vipi unafurahia kula mali ya dhuluma ilihali hujui umebakisha muda gani wa kuishi.

Je, wewe ni katika wanaodhulumu watu?

Kama jibu ni ndio, basi ni bora uache tabia hiyo mara moja kwani Mwenyezi Mungu anasema:

“Kwa hakika tumeiumbia Jehannam majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika.” (Qur’an, 7:179).

Yamkini nyoyo za watu hawa zimejaa huba na shauku ya kusaka ‘maisha bora’ ya dunia, hata kwa njia za dhuluma na ghushi. Na pindi wanaporuzukiwa mali hutumia mali hiyo katika mambo ya kufuru na uhuni, kana kwamba hakuna tena maisha ya baada ya kifo.

Jihadhari na mwisho mbaya

Ni ukweli ulio wazi kuwa kuogopa mwisho mbaya kunasaidia kujitathmini katika matendo na kuimarisha imani. Kutojali mwisho mbaya huondoa hofu ya Allah Ta’ala na hatima yake ni maangamivu.

Katika jumla ya ukumbusho kwa viumbe kuhusiana na mwisho wa watu wabaya, Allah Ta’ala anasema:

“Kab- la yenu zimepita nyendo nyingi, basi tembeeni katika ulim – wengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanaokanusha.” [Qur’an, 3:137].

Kimsingi, mja anapokumbuka kifo, maisha ya kaburini na adhabu za siku ya hesabu, moyo wake hulainika na hutumia kila nukta ya wakati wake katika kutathmini amali alizozitenda.

Dhuluma, kama alivyosema Mtume ni giza la Siku ya Kiyama. Hivyo, yeyote atakayeendelea kutenda dhuluma, aelewe wazi kuwa ataingia Jehannam.

Katika hadithi iliyopekewa na Imam Hakim na Bayhaqi, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Amenijia Jibril akaniambia, ‘Ewe Muhammad! Ishi upendavyo bila shaka wewe ni maiti (utakufa), na mpende umtakaye bila shaka utafarikiana naye, na tenda unavyopenda lakini ujue utalipwa kwa vitendo hivyo…”

Hadithi hii inawakumbusha Waumini kutathmini matendo (amali) zao wakiwa duniani kabla hayajadhihirishiwa na kuoneshwa kwa sura ya maandishi (kitabu) Siku ya Kiyama.

Kwa hiyo ndugu yangu Muislamu, usipambe mwili wako kwa nguo iliyopatikana kwa ghushi au dhuluma, pia usile chakula au kinywaji cha haramu. Badala yake, dumisha unyenyekevu kwa Allah, kula kilicho halali, ishi na watu kwa wema na uzuie ulimi wako kuwateta watu, kuwakejeli, kuwatukana, kuwasingizia na kadhalika.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close