1. Tujikumbushe

Tetemeko likitokea tena sitaishi nanyi kamwe

Kutoka kwa Safiya bint Abi Ubayd (Allah amridhie) amesema: “Katika zama za Umar bin Khattwab (Allah amridhie) kulitokea tetemeko kubwa la ardhi mpaka vitanda vikatikisika.” Baada ya tukio hilo, Umar aliwageukia watu na kuwaambia: “Mmezusha jambo kwa haraka mno. Kama tetemeko litatokea tena, basi nitaondoka.”

Katika riwaya nyingine ya Hadith hii, Umar amesema: “Enyi watu! Matetemeko hayatokei ila kwa jambo ambalo mmelizua (wenyewe). Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu ipo mkononi mwake, kama (tetemeko) litatokea tena sitaishi nanyi kamwe.” [Taz: ‘Muswannaf Ibn Abi Shaybah,’ Juz. 2, Uk. 473].

Mafunzo ya tukio

Ardhi ni neema kubwa ambayo Allah ametuneemesha kwayo. Juu ya ardhi tunaishi na kufanya kazi zetu kwa amani na utulivu. Hata hivyo, wengi wetu hatuoni thamani ya ardhi hadi pale matetemeko yanapotokea.

Kwa maana hiyo, tunapaswa kuyatazama majanga ya asili kama ikiwemo matetemeko ya ardhi, mafuriko, kimbunga na maporomoko ya ardhi kwa jicho la mazingatio ili tuweze kuonyeka na kuchukua tahadhari kama Uislamu ulivyotufundisha.

Ni wajibu wetu kuzishukuru neema tulizobarikiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuziheshimu na kuzitumia vizuri. Allah anatuambia:

“Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwishatengenezwa. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.” [Qur’an, 7:85].

Ukumbusho

Matetemeko ya ardhi ni ukumbusho kwa Waumini juu ya hali na mazingira ya Siku ya Kiyama. Allah ‘Azza Wajallah’ anasema:

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu. Hakika tetemeko la saa (Kiyama) ni jambo adhimu. Siku mtakapokiona (hicho Kiyama) kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu (kama) wamelewa, kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.” [Qur’an, 22:1–2].

Hakika Allah huleta matetemeko kwa lengo la kuwahofisha watu ili warejee kwake na kufanya toba.

“Na hatupeleki ishara (miujiza, maonyo) isipokuwa kwa ajili ya kuhofisha.” [Qur’an, 17:59].

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Jua na Mwezi ni ishara mbili miongoni mwa ishara za Allah. Havipatwi (viwili hivyo) kwa sababu ya kufa yeyote wala kwa uhai wake, bali Allah hufanya hivyo ili kuwahofisha waja wake.” [Bukhari].

Katika ufafanuzi wake kuhusu Hadith hii, Sheikh Ibnu Taymiya (Allah amrehemu) amesema:

“Matetemeko ya ardhi ni miongoni mwa ishara za Allah ambazo kwazo huwahofisha waja kama anavyowahofisha kwa kupatwa kwa Jua, Mwezi na matukio mengine. Matukio yote hayo yana sababu zake na hekima zake.” [Majmu’ul fatawa].

Tetemeko la ardhi ndiyo tukio kubwa zaidi ambalo huharibu majengo na kusababisha vifo. Ni kwa sababu hiyo, Qur’an Tukufu imelitaja tetemeko la ardhi kama tukio kubwa.

Kukithiri kwa matetemeko ni dalili ya Kiyama

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametujuza kuwa Kiyama kikikaribia majanga mengi yatatatokea.

“Hakitosimama Kiyama mpaka elimu iondoshwe, na matetemeko yawe mengi, na zama ziwe fupi, na fitna zidhihiri, na vifo viwe vingi na mali ziongezeke.” [Bukhari].

Maasi husababisha majanga

Katika tukio hili, tumeshuhudia Umar bin Khattwab (Allah amridhie) akiwaambia watu: “Mmezusha jambo kwa haraka mno.” Kauli hii inaonesha kuwa wakati wa ukhalifa wake, baadhi ya watu walifanya makosa (madhambi) ndiyo maana tetemeko lilitokea.

Qur’an inasema: “Ufisadi umedhihiri nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale iliyochuma mikono ya watu ili (Allah) awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.” [Qur’an, 30:41].

Watu wanapokithirisha dhuluma, mauaji, kula riba, uzinifu, kuacha sala, kuzuia zaka, kupunja katika vipimo na kuimba/kucheza muziki, Allah huwaadhibu kwa mabalaa kama vile njaa, kimbunga, magonjwa, ukame na matetemeko ya ardhi.

Ibnul Qayyim (Allah amrehemu) amesema: “Miongoni mwa taathira za maasi katika ardhi ni kutokea kwa matetemeko na kuondoshwa kwa baraka.”

Muumini humkumbuka Allah na kurejea kwake

Muumini wa kweli moyo wake huwa hai. Muumini anapoona ishara mbalimbali za Allah, hurejea kwake kwa kufanya toba hali ya kuwa ni mwenye hofu kubwa.

Tunasoma katika somo la Tareikh kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipopita katika miji ya Thamudi (watu wa Mtume Swaleh) aliwakataza Maswahaba zake kuingia katika nyumba zao isipokuwa wawe wanalia. Pia, Mtume aliwakataza Maswahaba kunywa maji ya visima vya watu wa Thamudi. Yote hayo yanatokana na maovu waliyoyafanya.

Ni vizuri waja wakarejea kwa Allah pindi yanapotokea majanga. Sheikh Ibnu Uthaimin (Allah amrehemu) amesema, kitendo cha watu kuswali pindi linapotokea tetemeko kama wanavyofanya katika sala ya kupatwa kwa Jua au Mwezi ni miongoni mwa mambo ambayo wanazuoni wametofautiana.

Lakini kauli yenye nguvu ni kuwa, likitokea tetemeko pataswaliwa. Kwa mujibu wa kauli iliyo sahihi zaidi, tetemeko likitokea kila mtu atasali peke yake nyumbani, kwani haijathibiti kwa uwazi katika sunna kuwa watu waswali jamaa kama ilivyo sala ya kupatwa kwa Jua.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close