1. Tujikumbushe

RAMADHANI: Chuo cha uchamungu karibia kufunguliwa

Zama zinazidi kuzunguka, masiku yanazidi kukatika, na misimu ya kheri nayo inakuja kwetu Waislamu na kuondoka.

Kwa mara nyingine tena Waislamu tumeanza kunusa manukato mazuri yanayosukumwa na upepo mwanana wa Ramadhan, mwezi mtukufu wenye baraka na kheri nyingi na ambao Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ameuelezea kwa kusema:

“Atakayenyimwa kheri za mwezi huu – kwa uzembe wake – basi amenyimwa kheri zote.” [Nasai].

Katika kauli yake nyingine, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) akiwahutubia Maswahaba mwishoni mwa mwezi wa Shaaban alisema: “Umeshawajieni mwezi wa Ramadhan, ni mwezi uliobarikiwa…” [Nasai].

Tukiifananisha Ramadhan na madrasa ama chuo kikuu, tunaweza kusema kwamba, sasa tayari msimu wa kufunguliwa umewadia. Hiki ni chuo cha kiroho ambacho hutoa masomo yake kwa hekima na kwa usulubu bora katika kuzilea nyoyo. Mwezi wa Ramadhan ni chuo kikuu na funga ndiyo nembo yake inayoonekana kwa mbali sana.

Lengo la chuo hicho ni kupasisha zaidi na kukomesha zero zote kwa wanafunzi wake (Waislamu) na kuwafikisha kwenye kilele cha uchamungu.

Masomo ya Ramadhan

Somo la kwanza: Funga Masomo ya chuo hiki kwanza ni funga. Somo hili katika chuo hiki cha siku 29 au 30 zinazokariri katika kila mwaka, limeanza tokea mwaka wa pili Hijriyya.

Lengo kuu la funga ni kumkomboa mja kutokana na tawala za matamanio ya nafsi na shetani na kumsukumia kwenye utawala wa Allah na sheria zake.

Wanafunzi wa madrasa hii hawana budi kufahamu kwamba, mwenye kujitahidi katika somo hili atastahiki kutunukiwa kile alichokisema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie):

“Pepo ina mlango unaitwa Rayyaan. Hawaingii kupitia mlango huo ila wafungaji.” [Bukhari na Muslim]. “Mfungaji na furaha mbili: furaha ya kwanza pale anapofutari, na furaha nyengine ni atakapokutana na Mola wake.” [Muslim].

Kadhalika, wanafunzi wanapaswa kujua kwamba, jitihada katika somo hili (funga) husaidia sana katika kuangamiza ushawishi wa shetani kwa sababu njia kuu anayoitumia shetani katika kuwapoteza watu ni kuyapa nguvu matamanio. Inajulikana kuwa, matamanio huwa hai kwa kula na kunywa, kwa hivyo njia njia ikifungwa kwa siku na nsaa kadhaa, shetani hushindwa kuvunja ukuta.

Baina ya mja na Mola wake tu

Hili ni somo ambalo Mwenyezi Mungu amejihusihia na kumuhakikishia mja mafanikio na malipo yake makubwa kwa kusema:

“Matendo yote ya mwanadamu ni yake ila swaumu, swaumu ni yangu na mimi ndiye nitakayeilipa.”

Siri ya malipo hayo ni kwamba, kufunga kisheria humaanisha kujizuia na matamanio ya nafsi kwa ajili ya Allah. Mfungaji huacha kula, kunywa na kufanya mengine ambayo mengine ni ya halali hata kama atapata fursa ya kuyafanya na kusiwe na mtu atakayemuona. Kitendo hiki humfurahisha sana Mwenyezi Mungu, na kwa hali hiyo humlipa mja malipo yasiyo kifani.

Faida za funga kiafya

Wanafunzi wakilielewa vya kutosha somo hilo la funga katika chuo hicho, itawasaidia sana kiafya pia. Wataalamu wa afya wanaamini kuwa, funga ni moja ya njia bora za kinga na tiba kutokana na maradhi mbalimbali.

Kwa mfano, inajulikana kuwa funga huyeyusha sumu zinazotokana na vyakula mtu anavyovitumia kwa muda mrefu. Pia, funga huimarisha mwili na kuurejesha katika hali inayotakiwa kutokana na mabaki ya vyakula na vinywaji yasiyotakiwa mwilini.

Si hayo tu, funga humzowesha mja kupanga utaratibu mzuri wa milo ya kila siku na vilevile hupumzisha zana (mashine) za usagaji na mmeng’enyo wa chakula tumboni. Kadhalika, funga husaidia kupunguza unene, uzito wa tumbo (mwili) na wingi wa gesi na mafuta. Kwa ujumla faida za somo hili (funga) ni nyingi hatuwezi kuzitaja zote. Turidhike tu na kauli ya Allah:

“Na mkifunga ni kheri kwenu lau mungelikuwa mnajua.” [Qur’an, 2: 184].

Somo la pili: Qur’an Somo la pili katika chuo cha Ramadhan ni Qur’an. Somo hili lina mahusiano makubwa na lile la mwanzo kwani Qur’an imeteremshwa ndani ya Ramadhan, ambapo ndiyo imefaradhishwa funga.

Katika jitihada za kuliendea somo hili, mwanafunzi anapaswa kuwaiga masalafi (wema waliopita). Baadhi yao, walihitimisha Qur’an kila siku kumi, wengine baada ya kila siku saba, huku baadhi yao kila baada ya siku kumi wakihitimisha Qur’an.

Endapo mja atalifahamu vyema somo hili na baada ya hapo akalifundisha kwa wengine, basi anakuwa ni mbora wa umma huu kama alivobainisha Mtume katika hadith iliyosimuliwa na Uthman (Allah amridhie):

Bora wenu ni ambaye amejifunza Qur’an na akaifundisha.”

Ni kutokana na ubora huu wa mwezi wa Ramadhan ndiyo maana husemwa: “Lau umma ungelijua kheri zilizo ndani ya Ramadhan wangelitamani mwaka mzima uwe Ramdhan.”

Kwa ujumla faida za funga ni nyingi na hatuwezi kuzitaja zote. Turidhike tu na kauli ya Allah

“Na mkifunga ni kheri kwenu lau mungelikuwa mnajua.” [Qur’an, 2: 184].

Basi hasara kubwa iliyoje kwa ambaye matangazo ya kufunguliwa chuo cha Ramadhan asijiunge mpaka kikafungwa, au kwa uzembe wake akashindwa kuyafahamu masomo yaliyofundishwa na kufeli!

Waislamu chuo cha Ramadhan chafunguliwa tujipange.

Tunamuomba Allah atufikishe Ramadhan na atuwezeshe kufanya ya kheri yatakayomridhisha. Amin.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close