1. Tujikumbushe

Penye kheri hapakosi shari

Baada ya mwanadamu kuumbwa na kuletwa hapa ulimwenguni, kumekuwapo na wimbi kubwa la vitendo vya kheri na shari vinavyofanywa na wanadamau. Hii inaonesha kuwa kheri na shari ndiyo msingi wa tabia zinazotawala maisha ya wanadamu hapa ulimwenguni.

Anasema Mola Muumba: “Natunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.” [Qur’an, 21:35]. Kwa sababu ya kuwapo vitendo vya kheri na shari hapa ulimwenguni, Uislamu umewaamirisha wafuasi wake kuwajibika katika kuamrishana mema na kukatazana maovu.

Mungu anasema: “Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu.” [Qur’an, 9:71]. Naam, tunawajibika kwa sababu palipo na wema, wapo waharibifu wenye kufanya ufisadi.

Anasema Mwenyezi Mungu: “Wanaume wanafiki na wanawake wanafiki, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanafiki ndiyo wapotofu.” [Qur’an, 9:67].

Kwa hiyo, tunapaswa kuyapima mambo yetu kwa jinsi yatakavyotupa faida au kutujengea hadhi mbele ya Allah. Katika zama hizi, Waislamu tulio wengi tumepoteza mizani hii. Na sisi tumezama katika kupima mambo kwa vipimo vya kidunia zaidi pasina kujali kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Hali hii inakwenda kinyume na malengo ya Muumini, ambaye siku zote anapaswa kujipima kupitia matendo yake yawe ya shari au ya kheri. Muumini hupima matendo yake kwa kuangalia je, nikifanya kitendo hiki nitapata radhi za Mwenyezi Mungu au nitamkasirisha?

Uovu kupewa nafasi kubwa kuliko wema

Katika dunia hii, kuna vizuri na vibaya, lakini vibaya ni vingi na vinapendeza zaidi katika macho ya wanadamu. Allah Aliyetukuka anasema: “Hawawi sawa wabaya na wema, hata huo wingi wa wabaya ukikufurahisha (usimili katika wingi huo). Basi mcheni Mwenyezi Mungu enyi wenye akili ili mpate kufanikiwa.” [Qur’an, 5:100].

Katika taratibu (Sunan) za Allah katika ulimwengu huu, ni kuwapo uongofu na wema, haki na batili, kunyooka sawasawa na kupondoka, lakini vyovyote iwavyo, ukweli utabakia siku zote kwamba Qur’an ndiyo kipimo cha haki na uadilifu.

Allah ametubainishia wazi kuwa Waumini hawalingani na waovu, si katika matendo wala malipo: “Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa. Ama walioamini na wakatenda mema, watakuwa katika bustani za makazi mazuri ndiyo pa kufikia kwa waliyokuwa wakiyatenda. Ama wale waliotenda uovu, basi makazi yao ni motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa, ‘Onjeni adhabu ya moto mliyokuwa mkiikanusha.’” [Qur’an, 32:18–20].

Kama ambavyo hawatalingana katika maisha ya Akhera, vilevile watu wema na waovu hawalingani katika maisha haya ya dunia. Allah anahoji: “Je! Wanadhani wanaotenda maovu kuwa tutawafanya kama walioamini, na wakatenda mema, sawasawa katika uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya wanayoihukumu!” [Qur’an, 45:21].

Kuwa miongoni mwawachache wenye kunufaisha

Historia inaonesha kuwa katika kila zama hapakosekani kundi kubwa la watu ambao dhamira yao ni kufanya uharibifu katika ardhi kwa maslahi yao binafsi. Kwa sababu ya kutenda kwao maovu, dunia imekuwa ikikabiliwa na matatizo na majanga mbalimbali huku kukiwa na kikundi kidogo tu cha watu kinachokataza na kuzuia uovu huo.

Anasema Mwenyezi Mungu: “Basi mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanaokataza uharibifu katika nchi, isipokuwa wachache tu, ambao ndiyo tuliowaokoa? Na waliodhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni wakosefu.” [Qur’an, 11:116].

Uovu unapoenea na waharibifu wakawa wengi, mvutano huwa ni mkubwa kwa sababu lengo la waharibifu ni kutoboa jahazi ili wasalimike hata kama watu wengine wataangamia.

Hivyo, kila mmoja wetu anawajibu wa kupiga vita maovu kwa sababu madhara yanapojitokeza hayachagui, huwakumba wanaohusika na wasiohusika. Hili ni jambo la kutiliwa mkazo na kila mmoja wetu, hasa ikizingatiwa kuwa, katika zama hizi, watu wengi hususan vijana wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya, wizi, uzinzi na mengineyo.

Cha kushangaza ni kwamba, katika jamii yetu wapo watu wakiwamo viongozi wa dini ambao hawaonekani kuchukizwa wala kukemea maovu yanayofanywa katika jamii. Hawa ndiyo aliowataja Ibnu Qayyim (Allah amrehemu) pale aliposema: “Ibilis amewahadaa watu wengi akawapambia kufanya dhikri nyingi, kuswali, kufunga, na kuipa nyongo dunia, wakaacha majukumu ya kuamrisha mema na kukataza mabaya.”

Kwa kuzingatia kauli hii, kila Muislamu anatakiwa akerwe na maovu huku akitafuta namna ya kupambana nayo kama ilivyokuwa kwa Nabii Shuaib (amani ya Allah iwe juu yake). Shuaib alisema kuwaambia watu wake:

“Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili wazi inayotokana na Mola Wangu Mlezi, na ikawa Yeye ameniruzuku riziki njema kutoka kwake? Wala mimi sipendi kukukhalifuni nikafanya yale ninayokukatazeni. Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyo weza. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye naelekea.” [Qur’an, 11:88].

Ndugu Muislamu, tambua kuwa mvutano kati ya kheri na shari, haki na batili ni wa muda mrefu kwani ulianza tangu alipoletwa mwanadamu hapa duniani. Hivyo, ndugu unalo jukumu kubwa la kupambana na maovu kama walivyopambana Mitume na Manabii wa Allah. Usitosheke na kufanya ibada ya sala tu, bali chukua hatua zinazostahiki katika kila unalodhani ni jambo la dhambi ima kwa kulikemea au kuliondosha.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close