1. Tujikumbushe

Pamoja na jitihada, katika malezi uongofu unatoka kwa Allah

Wataalamu wanasema malezi ni mchakato mzima wa kuchunga ustawi na maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili, kihisia na kijamii.

Sisi kama wafuasi wa dini tukufu ya Uislamu, tunaamini kuwa mchakato huo wa melezi lazima ufanyike kwa mujibu wa mafundisho na maelekezo ya dini tukufu ya Kiislamu, ikiwemo Qur’an Tukufu na Sunna za Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), kama zilivyotufikia kupitia Maswahaba na Wema Waliotangulia.

Kutambulika kama mzazi au mlezi – iwe baba au mama – haitoshi kuwazaa watoto tu bali tunawajibika kuhakikisha vipengele vyote vya ustawi wa mtoto vinaangaliwa, kwa kadri ya uwezo mliobarikiwa nyinyi walezi. Vipengele muhimu vya mahitaji ya ulezi viko katika maeneo matatu.

Kipengele cha kwanza ni usalama na ustawi wa kimwili. Umuhimu wa amani, usalama na kinga dhidi ya madhara kimwili, hauhitaji kusisitizwa sana na ndio maana mataifa yanatumia mamilioni ya dola kulinda raia wake. Kama mataifa yanavyotumia mamilioni, mzazi naye vilevile anapaswa kuwekeza pesa katika kuwalinda watoto wake.

Jitihada za kuhakikisha watoto analindwa zisiwe za kusubiri hatari bali mzazi anahitajika kuchukua kila hadhari kuhakikisha watoto hawawi kwenye mazingira hatarishi. Mfano isiwe watoto wanazururura popote wapendapo hali mzazi hujui halafu wakipata tatizo ndio unakurupuka wakati tayari madhara yashatokea. Kumbuka kuw a athari huweza kubaki milele iwapo akipitia aina fulani za ukatili. Kinga ni bora kuliko tiba.

Kipengele cha pili ni maendeleo ya akili (taaluma, elimu, maarifa). haitoshi tu kulinda watoto dhidi ya madhara ya kimwili, bali ni muhimu vilevile kumjenga mtoto kiakili kwa kumpatia elimu itakayomuwezesha kumjua Mwenyezi Mungu, kufikiri na kuchanganua mambo, kujitegemea na muhimu zaidi kumpa silaha ya kumlinda dhidi ya upotofu.

Katika moja ya hadith za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) iliyosimuliwa na Abu Huraira, amenukuliwa akisema:

“’Mtoto hazaliwa ila katika AlFitra (Uislamu) kisha wazazi wake humfanya awe wa dini ya Kiyahudi, Kikristo au Majushi, kama mnyama anavyozaa mtoto timilifu. Unaona sehemu yoyote ya mwili wake imekatwa?’ Kisha akasoma, ‘Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui [Quran, 30:30].’”

Hivyo basi, ni muhimu sana mzazi amlinde mtoto dhidi ya fikra potofu zinazoweza kumfanya akengeuke kutoka kwenye dini yake ya asili: Uislamu.

Kipengele cha tatu cha malezi ni katika kumjenga mtoto ni ulinzi wa kihisia. Watoto wanahitaji kupewa ulinzi taaluma juu ya namna ya kudhibiti hisia zao zisijekuwadhuru. Miongoni mwa mambo muhimu yatakasaidia kumlinda mtoto kihisia ni imani imani katika Qadar, kwamba Hakuna uwezo wala nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Hatofikiria mtoto kujiua kwa sababu haikuwezekana kumuoa au kuolewa na fulani kwa sababu anajua huwezi kupata ili kile ambacho ni riziki yako aliyokuandikia Mwenyezi Mungu.

Uongofu ni kwa Mwenyezi Mungu

Wakati tukifanya jitihada za kuwalinda watoto dhidi ya upotofu, ni muhimu tuelewe pia kuwa Mwenyezi Mungu ndie awezaye kutuongoa sisi na vizazi vyetu. Hivyo basi, ni muhimu jitihada zetu ziende sambamba na dua. Tunayo mifano mingi kutoka katika Qur’an kuonesha kuwa Mitume wote (amani ya Allah iwashukie) walijua umuhimu wa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kumuomba awaongoe wao na vizazi vyao. Sisi ni nani hadi tusifuate mifano hiyo?

Hebu turejee baadhi ya nukuu hizo za Mitume.

“Palepale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi, akasema: ‘Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unayesikia maombi.’” [Qur’an, 3:38].

Pigilia mstari neno ‘uzao mwema.’ Bila shaka uzao mwema ni ule ambao utatambua jukumu tuliloumbiwa la kumubudu Mwenyezi Mungu na kulitekeleza.

Katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu amenukuu dua ya Nabii wake Ibrahim ambaye pia ameomba uongofu:

“Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu. Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu.” [14:40–41].

Katika aya nyingine, twakutana na kauli yake Allah Ta’ala akitaja moja ya dua za ‘Waja wa Rahman’ watakaolipwa makao ya juu:

“Na wale wanaosema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.” [25:74].

Katika mfululizo huu wa aya kutoka Qur’an zinazoonesha kuwa uongofu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, tumalize kwa hii:

“Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapofika utu uzima wake, na akafikilia miaka 40, husema, ‘Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayoyapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, n a mimi ni miongoni mwa Waislamu.” [46:15]

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close