1. Tujikumbushe

Nyoyo hutulia kwa kumtaja Allah

Juwairiyya bint Harith (Allah amridhie) amesimulia kwamba, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) aliondoka asubuhi baada ya kuswali sala ya Alfajiri. Mtume alimuacha Juwairiyya msikitini akiwa anamdhukuru Allah, na alibaki hapo mpaka muda wa Dhuhaa (baada ya kuchomoza Jua).

Mtume akamwambia Juwairiyya: “Upo hapo kama nilivyokuacha? Hakika mimi nilipoondoka hapo, nilisema maneno manne mara tatu. Lau (maneno hayo) yangelinganishwa na maneno uliyoyasema wewe kwa muda wote uliokaa msikitini yangekuwa sawasawa.”

Maneno hayo ni ‘Subhaanallah adada khalqihi, waridhwaa nafsihi, waziinata arshihi, wamidaada kalimaatihi’ (Utakasifu ni wa Allah kwa idadi ya viumbe wake na kwa ridhaa ya nafsi yake na uzito wa arshi yake na wino wa maneno yake.’” [Muslim].

Mafunzo ya tukio

Umuhimu wa kumtaja (kumdhukuru Allah)

Kumtaja Allah ‘Azza Wajallah’ ni miongoni mwa ibada zenye fadhila nyingi na malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Ibada hii (kumtaja Allah) humpa Muumini utulivu wa moyo na matumaini, kama Allah anavyobainisha:

“Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumtaja Allah. Hakika kwa kumtaja Allah ndiyo nyoyo hutua!” [Qur’an, 13:28].

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Muislamu anayemtaja Mola wake na yule asiyemtaja Mola wake, ni sawa na mtu aliye hai na aliyekufa.” [Muslim].

Ni muhimu Muislamu kukithirisha ibada ya dhikri kama anavyosisitiza Allah:

“Enyi mlioamini! Mdhukuruni Allah kwa wingi wa kumdhukuru. Na mtakaseni asubuhi na jioni. Yeye (Allah) na Malaika wake wanakurehemuni ili kukutoeni gizani na kuwapeleka kwenye nuru. Naye (Allah) ni mwenye kuwarehemu Waumini.” [Qur’an, 33:42–43].

Katika kuilezea aya hii, Ibnu Abbas (Allah amridhie) amesema:

“Allah hakuwaamrisha waja wake kutekeleza wajibu wowote bila ya kuweko mipaka iliyojulikana. Pia Allah hupokea nyudhuru za wale wasioweza kutekeleza (wajibu huo). Ama kumdhukuru Allah, hakuweka mipaka na hakuna atakayekuwa na udhuru wa kutoweza kumdhukuru Allah isipokuwa atakayedhalilika kwa kupuuza na kudharau, kwani Allah Ta’ ala anasema: ‘Basi mkumbukeni Allah mkisimama, na mkikaa, na mnapojinyoosha kwa kulala.’’ [Qur’an, 4:103].

Kadhalika, Abu Huraira (Allah amridhie) ameHadithia kwamba, siku moja Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa anatembea katika njia ya kuelekea Makka, akapita katika jabali moja linaloitwa Jumdaan. Mtume akatuambia:

“Tembeeni! Hili ni jabali la Jumdaan. Wametangulia Almufarriduun.” Tukauliza: “Almufarriduuna ni akina nani?” Akasema: “Wanaume na wanawake wenye kumtaja sana Allah.” [Muslim].

Na imepokewa kutoka kwa Abdullah Bin Busr (Allah amridhie) kwamba, mtu mmoja alimuuliza Mtume:

“Ewe Mjumbe wa Allah! Ibada za dini zimekuwa nyingi kwangu, basi nieleze kitu ambacho nitaweza kudumu nacho.” Mtume akamwambia: “Ulimi wako uwe laini kwa kumtaja Allah.” [Tirmidhi].

Katika tukio hili, tumemshuhudia Juwairiyya bint Harith, mke wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akikaa msikitini kila baada ya sala ya alfajiri mpaka wakati wa dhuha kwa ajili ya kumtaja Allah.

Kutofautiana ubora wa adhkaar

Miongoni mwa mambo ambayo Muislamu anatakiwa kuyazingatia ni ubora wa kile anachokifanya. Kuna aina nyingi za dhikri ambazo zimethibiti kutoka kwa Mtume (rehema na amani zimshukie). Dhikri zote zilizothibiti kutoka kwa Mtume ni bora na zina fadhila nyingi, lakini zinazidiana kwa ubora kulingana na matamshi yake au malipo yaliyotajwa kuwa yanapatikana kwa kusoma dhikri hizo.

Miongoni mwa dhikri bora na zenye malipo makubwa ni ile tuliyoitaja katika Hadith ya Muslim mwanzoni mwa makala hii. Dhikri hiyo ni:

“Subhaanallah adada khalqihi, waridhwaa nafsihi, waziinata arshihi, wamidaada kalimaatihi (Utakassifu ni wa Allah kwa idadi ya viumbe wake na kwa ridhaa ya nafsi yake na uzito wa arshi yake na wino wa maneno yake.”

Muislamu anaweza kutumia muda mfupi kupata thawabu nyingi kwa kutamka maneno haya. Hakuna ajuaye idadi ya viumbe wa Allah, uzito wa arshi yake wala wingi wa wino ulioandika maneno yake isipokuwa Allah mwenyewe. Kwa kulijua hilo, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliegemeza idadi ya dhikr katika vitu vingi visivyojulikana idadi yake ili amtaje Allah kwa wingi usiojulikana.

Kwa njia hiyo, Mtume akawa anamdhukuru Allah kwa wingi na kumshinda mkewe, Juwairiyya ambaye alikuwa anamdhukuru Allah baada ya sala ya Alfajiri mpaka muda wa dhuhaa (baada ya kuchomoza Jua).

 Kutumia muda wa ibada vizuri

Katika tukio hili, tumeshuhudia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alivyohamaki alipoona mkewe, Juwairiyya ameketi muda mrefu msikitini kwa ajili ya kumdhukuru Allah.

Mtume hakumkosoa Juwairiyya bali alimfundisha dhikri bora na zenye malipo makubwa. Ni dhahiri kuwa, Juwairiyya alikuwa peke yake msikitini akimdhukuru Allah kwa unyenyekevu mkubwa. Lakini hilo halikumzuia Mtume kumpa muongozo ulio bora.

Bahati mbaya sana, baadhi yetu tumekuwa tukifadhilisha zaidi adhkaar za kutunga na nyimbo. Sehemu kubwa ya dhikri hizo ni mashairi yanayowazungumzia watu na kuwasifu.

Watu wamekuwa wakipoteza muda mwingi usiku na mchana kufanya dhikri ambazo hazijathibiti kwa Mtume, wakiamini hilo ni jambo zuri na linaloruhusiwa kisharia.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Maneno mawili ni mepesi mno juu ya ulimi, mazito mno katika mizani, yanapendeza mno mbele ya Ar–Rahmaan (Mwenye kurehemu). Maneno hayo ni: “Subhaana Llahi wabihamdihi Subhaana Llahil Adhwiym (Ametakasika Allah na sifa njema zote ni zake, Ametakasika Allah Aliye Mtukufu.” [Bukhari na Muslim].

Muislamu atakayetamka maneno haya kwa unyenyekevu, atachuma thawabu nyingi mno kuliko yule anayeimba na kurukaruka usiku kucha akiamini kuwa ametan – gulia kwa kheri nyingi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close