1. Tujikumbushe

Niliogopea Nafsi Yangu Ewe Mjumbe wa Allah

Ulikuwa ni usiku wenye baridi kali katika vita vya ‘Dhatu Ssalaasil.’ ‘Amr bin al-’As (Allah amridhie) aliota, akapatwa na janaba. Akaihurumia nafsi yake, akawaza ikiwa ataoga basi anaweza kuangamia. Akaamua kutayamamu (kutumia udongo badala ya maji) kisha akawaswalisha Maswahaba wenzake (Allah awe radhi nao). Baada ya vita, wenzake wakamfahamisha Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) Mtume akasema: “Ewe ‘Amr, umewaswalisha wenzako ukiwa na janaba?” ‘Amr (Allah amridhie) akasema: “Nimeigopea nafsi yangu na kwa hakika Allah Mtukufu amesema, “Wala msijiue. Hakika Allah ni Mwenye Kuwahurumia”. (Qur’an, 4:29). Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) akacheka na hakusema kitu (Bukhari). Kwa hakika, tukio hili linatuwekea wazi sifa miongoni mwa sifa za mfumo wa Uislamu na sharia yake, uwepesi. Asili ya twahara ni kutumia maji lakini ikiwa maji yamekosekana au mtu ameshindwa kutumia maji kwa sababu za kiafya, basi amefanyiwa wepesi wa kutumia udongo badala ya maji. Katika swala, mtu akishindwa kusimama ataswali akiwa amekaa, akiwa ni msafiri ameruhusiwa kupunguza swala zenye rakaa nne kwa kuziswali rakaa mbili mbili. Si hivyo tu, msafiri pia ameruhusiwa kukusanya swala ya Adhuhuri pamoja na Alasiri pia Magharibi kuiswali pamoja na Isha. Katika ibada ya funga, ikwa mtu ni mgonjwa au ni msafiri kukawepo mashaka ya kufunga, anaruhusiwa kula mchana kisha atakuja kulipa funga yake katika siku nyingine ambazo mashaka hayo yatakuwa yameondoka. Katika Hijja na zaka hizi, ni ibada ambazo zimefaradhishwa kwa wale tu wenye uwezo. Hivi ndivyo ulivyo Uislamu katika sharia, dini iliyojengwa katika misingi bora, inayozingatia udhaifu wa mwanadamu na hali ya mazingira aliyokuwa nayo na ukaweka taratibu zilizokwenda sambamba na hali hiyo pamoja na mazingira hayo. Mama Aisha (Allah mridhie) anatufahamisha wazi katika hadithi nyingine kuwa Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) hakupata kukhiyarishwa katika mambo mawili isipokuwa alichaguwa lile lililokuwa jepesi kati ya mawili hayo muda wa kuwa si dhambi. Ikiwa ni jambo lenye madhambi ndani yake basi alikuwa mbali mno na jambo hilo kuliko watu wote (Bukhari). Ni wazi kuwa, wepesi uliowekwa katika mambo mengi ndani ya Uislamu hasa katika masuala yanayohusiana na ibada, unapelekea nafsi kupenda ibada na kufululiza katika utekelezaji wake, hata katika hali ya mashaka. jambio hili pia linatuonesha wazi kuwa kutopenda kuyaendea yale aliyotuwepesishia Allah katika ibada mbalimbali kunatufanya kuyafanya magumu mambo mbalimbali na kuyatia uzito usiostahiki, na hatimaye tunakwama katika kuyatekeleza kwa ufanisi. Hapa ndipo Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) alipotueleza: “Hakika hii dini ni nyepesi na hakuna yoyote atakayeitia uzito isipokuwa itamshinda”( Bukhari). Watu wanashindwa kutekeleza ibada kwa ufanisi kwa sababu ya kutopenda kutumia fursa zilizopo kulingana na hali na mazingira ya utekelezaji wa ibada hizo. Wengine wanafanya hayo wakitegemea kuwa wanapata malipo makubwa zaidi kuliko yule anayezifanyia kazi ruhusa mbalimbali alizotuwekea Allah katika sharia zake, jambo ambalo si kweli. Allah anapenda kuwaona waja wake wakitumia ruhusa hizi alizowawekea kulingana na hali zao. Katika tukio hili, tunajifunza umuhimu wa kuzilinda nafsi zetu kwa kuziepusha na mambo yote yanayoweza kutudhuru au kutuangamiza moja kwa moja. Kuna mambo mengi mno katika maisha yetu ambayo tunayafanya lakini ndani yake kuna madhara kwetu sisi wenyewe au kwa watu wengine. Ni vema tukaelewa kuwa kuhifadhi nafsi ni jambo muhimu sana katika maisha ya mtu na kujidhuru au kuwadhuru watu wengine ni kosa kubwa mbele ya Allah Mtukufu, lakini pia ni kusababisha uharibifu na maangamivu katika ardhi ya Allah. Tunaona wazi mfano huu wa ‘Amr bin al-’As (Allah awe radhi naye) alivyoogopa kuijiumiza kwa maji ya baridi katika usiku uliokuwa na baridi kali akaamua kutumia udongo. Taarifa hizi zilipomfikia Mtume (rehma na amani za Allah zimshukie) alifurahishwa na majibu ya utetezi kutoka kwa ‘Amr. Utetezi huu aliuelekeza katika kuilinda na kuihifadhi nafsi yake isije ikaangamia. Wale wanaozidhuru nafsi zao kwa kutumia vitu vya aina mbalimbali kama vile sigara, madawa ya kulevya, mirungi na vitu vingine vyenye kemikali zenye madhara, wajifunze kupitia mafundisho haya ya Uislamu. Ni bora watu hao waone mafundisho ya Uislamu katika kulinda nafsi na uzito wa jambo hilo katika sharia. Ikiwa katika kumuabudu Allah haitakikani mtu ajidhuru itakuwaje katika mambo mengine yasiyokuwa na umuhimu katika maisha ya mwanadamu yatakapopelekea kujidhuru yeye mwenyewe? Kwa hakika adhabu yake itakuwa ni kali. Watu wamebuni starehe mbalimbali hata katika yale yenye madhara kwa nafsi zao. Wengine wamewekeza katika bidhaa zenye madhara kwa afya za watu na kuzifanya ndiyo muhimili wa chumo lao na vipato vyao, wakiendesha maisha yao kwa kuteketeza nafsi za watu na kueneza ufisadi katika ardhi. Tukio la ‘Amr bin al-’As (Allah awe radhi naye) litabakia kuwa miongoni mwa matukio yanayoonesha sifa za kipekee zinazoangaza katika mafundisho ya Uislamu, kuwafahamisha walimwengu kuwa Uislamu ni dini inayojali maisha ya watu, ni dini inayotoa mafundisho ya kuhifadhi na kulinda uhai wa watu na haikuwa dini yenye fujo na mafundisho ya kuangamiza watu kama wanavyodai maadui wake.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close