1. Tujikumbushe6. Malezi

Ni yupi rafiki bora?

BINADAMU ni kiumbe wa kijamii. Hii ina maana, maisha ya binadamu yananategea sana watu mbalimbali anaosuhubiana nao kwa namna moja au nyingine wakiwemo wanafamilia, wanaukoo, majirani, wafanyakazi wenzake na bila kusahau marafiki.

Mjadala wetu wa leo katika safu hii unahusu marafiki, watu muhimu sana ambao wakati fulani wanaweza kuwa karibu nawe na kuwa na ushawishi kuliko hata ndugu yako.

Mtu mmoja mwenye busara aliwahi kusema: “Ndege wafananao huruka pamoja.” Mwingine akasema: “Nioneshe rafiki zako nitakuambia wewe ni mtu wa aina gani.” Kauli hizi ni msisitizo wa ukweli kuwa marafiki wana ushawishi mkubwa katika tabia za mtu.

Kwa hiyo, kwanza: Mara nyingi marafiki huchaguana kwa kuwa na mambo yanayofanana. Pili: Pnapo tofauti ya tabia kati ya marafiki, kuna uwezekano mkubwa upande mmoja kuambukiza mwingine tabia kwa sababu mnapofanana tabia, hapo ndiyo urafiki hunoga.

Hivyo, ukiwa kama Muislamu, unapokuwa na marafiki wenye tabia njema, utafaidika kwa kukuambukiza wema huo. Lakini kama una marafiki wenye tabia mbaya ni hasara kwako kwa sababu hawatakushawishi ila mambo ya shari.

Kwa kuyajua haya, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) katika hadith iliyosimuliwa na Abu Huraira (Allah amridhie) ametuasa:

“Mtu hufuata dini ya rafiki yake, kwa hiyo kila mmoja aangalie nani anamfanya kuwa rafiki.” [Sunan al-Tirmidhi].

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amezungumzia kwa upana suala la urafiki katika Kitabu chake kitukufu, Qur’an.

Kwa mfano, Mwenyezi Mungu anatuonya kuhusu marafiki tunaoambatana nao pale aliponukuu kauli za majuto ya watu wa motoni waliochagua marafiki wabaya:

“Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema, ‘Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki! Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwishanijia. Na kweli shetani ni haini kwa mwanadamu.’” [Qur’an, 25:28- 29].

Katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu anazidi kutuhadithia namna Siku ya Kiyama marafiki watakavyogeukana na kuwa maadui wenyewe kwa wenyewe, isipokuwa wachamungu ambao wao watasalimika. Mwenyezi Mungu anasema:

“Siku hiyo, marafiki watakuwa ni maadui wao kwa wao, isipokuwa wachamungu. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na hofu siku hiyo wala hamtahuzunika.” [Qur’an, 43:67- 68].

Kisha katika aya zinazofuata, Mwenyezi Mungu anaazidi kufafanua sifa za ‘marafiki wachamungu’ ambao wametajwa kuwa hawatakuwa na hofu wala huzuni siku hiyo.

“…Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu. Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo…. ” [Qur’an, 43:69 – 73].

Kwa maslahi yetu Waislamu, Mwenyezi Mungu ametuelekeza aina ya marafiki bora na sababu zinazowafanya marafiki wa aina hiyo kuwa bora pale Mwenyezi Mungu alisema:

“Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika sala, na hutoa zaka, na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.” [Qur’an, 9.71].

Urafiki katika muktadha wa familia

Marafiki ni muhimu sana kwani wanaweza kukusaidia kuboresha maisha, kupata maendeleo na faraja. Marafiki pia ndiyo watu ambao mtakaa muda mwingi kushauriana na kubailishana mawazo huku wakati mwingine mkicheshana na kuburudishana. Marafiki pia wanasaidia kukupa faraja unapokumbwa na shida mbalimbali. Vilevile, marafiki hukuondolea upweke nyakati ambazo wengine wamekuacha. Rafiki wa kweli pia anaweza kuwa msiri wako.

Aina za marafiki

Marafiki wana daraja tofauti. Kwanza, wapo marafiki ambao wana uswahiba uliolala katika jambo fulani moja maalum tu.

Mfano, kuna marafiki wengi ambao wameletwa pamoja kwa sababu ya mapenzi ya dini, michezo, biashara na kadhalika. Pili, upo urafiki wa kila kitu, urafiki wa kina ambao hakika ni urafiki wenye nguvu sana. Nguvu ya aina hii ya pili ya urafiki, yaani urafiki wa kila kitu, ni kubwa sana. Ni aina ya urafiki ambao una nguvu kubwa pengine kuliko hata undugu.

Hata ukisikia watu wanaitana ‘best friends’ ujue wapo katika aina hii ya urafiki.

Aina hii ya pili ya urafiki aghlabu hujumuisha hata familia zote mbili za wahusika.

Katika aina ile ya kwanza ya urafiki watu hukutana katika maeneo fulani tu, wakaongea huko na kumaliza mambo yao. Kwa maana nyingine ni urafiki wa vijiweni. Kwa upande wa mwingine, aina ya pili ya urafiki inahusisha siyo tu wahusika kutembeleana nyumbani bali hata familia zao pia: mke kwa mke, mume kwa mume, watoto kwa watoto hujenga urafiki.

Kwa kuwa huu ni urafiki unaohusisha maingialiano ya kina, uchaguzi wa rafiki unatakiwa ufanyike kwa uangalifu kwa sababu kama utachagua rafiki mbaya utapata hasara siyo wewe tu bali pia familia nzima. Ukichagua rafiki mzuri, wewe na familia yako mtapata faida kubwa.

Kwa sababu hiyo nikumbushe kwa mara nyingine tena ile hadith ya Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) iliyosimuliwa na Abu Huraira:

“Mtu hufuata dini ya rafiki yake, kwa hiyo kila mmoja aangalie nani anamfanya kuwa rafiki.” [Sunan al-Tirmidhi].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close