1. Tujikumbushe

Mwanadamu na neema za Allah

Mpishano wa usiku na mchana

Kimsingi, maisha ya mwanadamu yanategemea sana uwepo wa usiku na mchana. Mchana ni kwa ajili ya kuhangaikia maisha na usiku kwa ajili ya kuupumzisha mwili na akili yake. Lakini bila shaka mwanadamu huyo anakiri kwamba, hana mchango wowote katika kuleta majira haya yanayomtawala yeye pamoja na viumbe wengine wakiwemo wanyama, wadudu na ndege.

Bas jambo lililotarajiwa kwa wenye akili timamu ni kufikiri na kupata jibu la kukinaisha juu ya nani mvumbuzi wa mwangaza wa mchana na ujoto-ujoto wake na kiza cha usiku kinachozimua ujoto-ujoto huo, ambapo hisabu ya miaka hujuilikana kupitia mfumo huo muhimu na wa ajabu, kisha ajinyenyekeshe kiutumwa (kumuabudu) kwake.

Qur’an inauelezea mpishano huu wa usiku na mchana, kama tunavyoushuhudia, kuwa umetokana na mfumo mkuu aliouweka Mwenyezi Mungu unaokitawala na kukiongoza kila kiumbe ili kiumbe hicho kilifikie lengo la kuumbwa kwake. Kwa maneno mengine, Allah Aliyetukuka, ndiye aliyeumba usiku na mchana na kuvipa zamu za kuja kwa wanadamu. Aidha, hiyo inaonesha kuwa ni moja ya rehema na ishara za kuwepo kwake. Pia hiyo inaonesha wingi wa neema ambazo Allah amewatunuku waja wake.

Hebu turejee aya zifuatazo: “Yeye ndiye aliyelijaalia Jua kuwa na mwangaza na Mwezi kuwa na nuru na akaupimia vituo ili mjuwe idadi ya miaka na hesabu. Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki, anazipambanua ishara kwa watu wanaojua. Hakika katika kutafautiana na usiku na mchana na katika alivyoumba Mwenyezi Mungu katika Mbingu na Ardhi, zipo ishara kwa watu wanaomcha Mwenyezi Mungu.” [Qur’an, 10: 4-5].

“Na kutokana na rehema zake amekujaalieni usiku na mchana ili mpate utulivu ndani yake na ili mtafute fadhila zake na ili mumshukuru.” [Qur’an, 28:73].

Tusome tena aya nyingine hizi zifuatazo: “Sema, mnaonaje lau Mwenyezi Mungu atajaalia usiku kuendelea hadi Siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Allah angelikuleteeni mwanga, basi hamsikii? Sema, mnaonaje lau Mwenyezi Mungu ataujaalia juu yenu mchana kuendelea hadi Siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Allah atakayewaletea usiku mkapata utulivu (mapumziko), basi hamuoni?“ [Qur’an, 28: 71-72].

Mvua

Binadamu anajua pia uzito na umuhimu wa neema ya mvua ambayo siyo hitajio la wakulima pekee, bali viumbe wote. Mvua hulainisha hewa na kuondoa joto kali, huleta unyevunyevu na huotesha miti mirefu ya matunda na ya kivuli. Kadhalika mvua hustawisha mimea kwa ajili ya chakula, na majani mazuri yanayolipamba ganda la mgongo wa ardhi likapendeza hadi kuwa malisho ya wanyama.

Allah Aliyetukuka anasema: “Na Yeye ndiye ateremshae mvua baada ya (walimwengu) kukata tamaa na hueneza neema zake, na yeye ni mlinzi na msifiwa.” [Qur’an, 42: 28].

Tuizingatie tena kauli ya Allah isemayo: “Na Yeye ndiye aliyeteremsha kutoka mawinguni maji, kwayo tukaotesha kila kitu, tukaotesha majani ya kijani katika mimea hiyo, tukatoa ndani yake punje zilizopangana, na katika mitende hutoka katika vikole vyake vishada vyenye kuinama, na anakuotesheeni bustani za zabibu na zaituni na makomamanga yanayofanana na yasIyofanana. Basi angalieni matunda yake yanapotoa na yanapoiva. Hakika katika hayo kuna ishara kwa wenye kuamini.” [Qur’an, 6: 99].

Na yote aliyonayo mwanadamu ni matokeo ya wingi wa neema na rehema za Allah, hivyo mwanadamu hana jinsi ya kujitenga nayo. Akiyakosa kwa Allah hawezi kuyapata kwa mwengine. Allah amesisitiza hilo kwa kusema:

“Na neema yoyote mliyonayo basi inatoka kwa Allah.”[Qur’an, 16:53].

Basi hizo ni baadhi tu ya neema kuu za Allah juu ya viumbe wote hapa ulimwenguni zinazomhakikishia kila kiumbe kupata mahitaji yake ya msingi. Neema hizi hapa duniani zimewaenea watu wote:

“… na rehema zangu zimekienea kila kitu.” [Qur’an, 7:156].

“Na lau kuwa si hisani ya Alla juu yenu na rehema zake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni mpole (mngelipata tabu sana).” [Qur’an, 24: 20].

Lakini kuna rehema (neema) nyengine kubwa ambazo Allah amewaandalia waja wake wachamungu huko Akhera hasa wale waliofuata vilivyo maagizo ya Allah walipokuwa duniani.

Imethibiti kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “ Mwenyezi Mungu amezigawa rehema vigawanyo mia moja, na akashusha ardhini kigawanyo kimoja. Kwa kigawanyo hicho, viumbe wote wanahurumiana (kiasi) mpaka mnyama huondoa kwato (mguu) yake juu ya mtoto wake kwa kuogopa kumkanyaga (kumuumiza).” [Bukhari]. (Na katika mapokeo mengine: “Na akabakisha tisini na tisa atawarehemu waja wake wema Siku ya Kiyama).

Hapa tunaona upeo usio kifani wa rehema za Allah. Ikiwa hii tuinayo kwa viumbe wote ni moja kati ya vifungu mia moja, basi itakuwaje rehema yake huko peponi! Rehema isio na mwisho! Na hapa ndipo inapodhihiri siri ya kauli yake:

“..naye kwa Waumini ni mwingi wa rehema.” [Qur’an, 33:43].

Tunamuomba Allah atudumishie neema zake hapa duniani na atujaalie katika waja wake wema watakaozifaidi neema zake zisizo na mwisho huko Akhera. Aaamin.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close