1. Tujikumbushe

Mwanadamu alivyofunikwa na neema za Mola wake

Kadri mwanadamu anavyoendelea kisayansi, anajikuta akizungukwa na neema za Muumba wake na anajikuta ni muhitaji wa neema hizo katika maisha yake ya kila siku.

Makala yetu wiki hii inshaAllah ina lengo la kuzitaja na kuzifanyia uchanganuzi kadri inavyowezekana baadhi ya neema hizo na kuonesha ukubwa na athari yake. Kisha tutaonesha jinsi mwanadamu anavyopaswa kumshukuru na kumuabudu mneemeshaji huyo adhimu.

Maana ya neema

Neema, rehema ama huruma ni hisia ya nafsi ambayo hupelekea kumpendelea mwengine kheri na kumkinga na shari. Na Allah hafanani na viumbe vyake katika sifa. Kwa maana nyengine, neema ni upole, hisani na ukarimu. Rehema/ neema ni moja ya sifa kuu za asili za Allah Muumba, ambazo zinathibitisha haki na stahiki ya kuabudiwa na viumbe. Na katika aya mbalimbali, Mwenyezi Mungu, amejisifu kwamba ni Mola Mneemeshaji, Mpole na Mwenye Huruma kwa Waja Wake.

Katika Surat Alfatiha ambayo Muislamu huisoma si chini ya mara kumi na saba kwa siku, Mwenyezi Mungyu anajitambulisha kuwa yeye ni ‘Rahmaan rrahiim’ na katika sura nyengine amesema:

“Na rehema zangu zimekienea kila kitu.” [Qur’an, 7: 156].

Katika Hadith iliyopokelewa na Abu Huraira (Allah amridhie) na kuandikwa na Bukhari na Muslim, Mtume amesema:

“Allah alipoumba viumbe aliandika katika daftari lake na kuliweka kwenye arshi yake, ‘Hakika rehema zangu zinashinda ghadhabu zangu. ’”

Alama za neema za Allah

Neema za Allah, kama alivyosema mwenyewe, ni nyingi mno kiasi kwamba hata tukizihesabu hatuzimalizi. Lakini moja ya neema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe ni kuwaumba kama binadamu na kuwatofautisha na wanyama na wadudu.

Allah Aliyetukuka amesema: “Kwa hakika tumemtukuza mwanadamu na tunambeba nchi kavu na baharini na tumemruzuku kwa aina mbalimbali za vyakula vizuri na tumemboresha juu ya viumbe vingi tulivyoviumba.” [Qur’an, 17: 70] .

Anasema pia: “Kwa hakika tumemuumba mtu kwa umbo bora kabisa.” [Qur’an, 95:4].

Vipawa

Vipaji au vipawa alivyotunukiwa binadamu kama vile akili, uwezo wa kufikiri, uwezo wa kujifunza na kuelewa, kuweoz wa ujieleza, uwezo wa kuona na kusikia, uwezo wa kumiliki mali pia ni katika alama za rehema na neema kubwa za Allah kwa wanadamu. Vingi katika vipawa hivi hawakupewa viumbe wengine. Na vile walivyopewa, basi ni kwa kiwango kidogo tu.

Mwenyezi Mungu anasema “Na Mwenyezi Mungu ndiye aliyekutoweni katika matumbo ya wazazi wenu hali ya kuwa hamjui kitu, akakujaalieni masikio, na macho na nyoyo ili mshukuru” (Qur’an, 16:78]. Na katika aya nyengine amesema: “Amemuumba mwanadamu akamfundisha kubaini/kueleza.” [Qur’an, 55: 3-4].

Vipaji hivi Allah anavijengea hoja na kuwahakikishia wanadamu kwamba, akiwanyan’ganya hakuna wa kuwarejeshea:

“ Sema, mwaonaje lau Mwenyezi Mungu akinyakua kusikia kwenu, na kuona kwenu na akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani angelikuleteeni vyote hivyo, hamzingatii? [Qur’an, 6:46].

Muongozo wa maisha

Na katika neema kubwa alizoneeshwa binadamu ni kupewa muongozo/mfumo sahihi wa maisha kupitia wateule wake (Mitume). Allah aliwajaza Mitume wake mapenzi kubwa na huruma juu ya watu wao, na akawapa na vitabu vyenye nukuu za sharia na hukumu mbali mbali zinazomuongoza mwanadamu katika kuliendelea lengo la maisha yake hapa duniani.

Allah analisemea hilo katika kauli yake: “Allah amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyowaletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anayewasomea aya zake, na anawatakasa na anawafunza kitabu na hekima, ijapokuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi” [Qur’an, 3:164].

Na katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu anasema:

“Hakika amekujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe, yanamuhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni sana, kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.” [Qur’an, 9: 128].

Mavazi

Neema nyengine ni kuteremshiwa mavazi. Mavazi huwatofautisha wanadamu na wanyama. Ni sitara, pambo na ni heshima. Chukulia lau wanadamu hivi walivyoumbwa. Je pasingekuwa na nguo, wangeishi vipi?! Katika hili Mwenyezi Mungu anasema:

“Enyi wanadamu, hakika tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu na nguo za pambo, na nguo za uchamungu ndiyo bora. Hayo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu ili mpate kukumbuka.” [Qur’an, 7: 26].

Safari

Nenda rudi hii anayoifanya binadamu nchi kavu, baharini na kwenye anga kwa raha na salama ni katika neema kubwa za Muumba. Imeandikwa katika Qur’an Tukufu:

“Yeye ndiye anayekuendesheni katika nchi kavu na baharini. mpaka mnapokuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, upepo mkali mara huwazukia na yakawajia mawimbi kutoka kila upande na wakaona wameshazongwa, basi hapo humuomba Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia maombi, ‘Ukituokoa na haya bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.” [Qur’an, 10: 22].

Katika aya nyengine amesema: “Na ni ishara kwao kwamba sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi liliosheheni, na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyovipanda, na tukitaka tunawazamisha wala hapana wa kuwasaidia wala hawaokolewi, isipokuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.” [Qur’an, 36:41-44].

Maji

Neema nyengine ni uwepo wa maji katika maeneo wanayoishi wanadamu na wanyama wao. Hii ni katika ihisani kubwa ya Allah isiyo kifani. Kwani maji ndiyo uhai. Qur’an inasema:

“ . . na tumekipa kila kitu uhai kutokana na maji.” [Qur’an, 21: 30].

Allah Aliyetukuka anaitaja neema hii kwa uzito mkubwa na kuwahakikishia kuwa pindi akiiondoa hawatoweza tena kuirejesha.

”Je hamuoni maji ambayo mnakunywa. Je nyinyi ndiyo ambao huyashusha kutoka vyanzo vyake au sisi ndiyo washushaji? Lau tungelitaka tungeliyafanya kuwa machungu, kwa nini basi hamshukuru? “ [Qur’an, 56: 68-70].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close