1. Tujikumbushe

Mwaka Mpya wa (1443h) Uwe wa Mikakati

Mwaka wa 1442 Hijriyya umekwisha na sasa umeingia wa 1443 kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu. Alhamdulillah! Waislamu tunapaswa kuzidi kumshukuru Allah Aliyetukuka kwa kutuweka mpaka tumeudiriki mwanzo wa mwaka huu mpya.

Ni vyema kila mmoja wetu kukaa na kujitathmini nini alichokifanya katika kustawisha dini na dunia yake, na anapaswa kuwa mkweli juu hilo. Wakati anayakagua matendo yake ya mwaka uliopita, asisahau kujiuliza ni kwa kiasi gani amefanya ya kumridhisha Mola wake kwa kutarajia malipo mema hapo atakaporudi kwake. Hii ni kwa sababu, mizunguko hii ya miaka huupunguza umri wa mja kwa haraka ya ajabu na humsogeza kwa Muumba wake.

Jamii ya Kiislamu nayo ina wajibu wa kujitathmini na kuona kama imesonga mbele, imebaki pale pale katika kipindi chote cha mwaka au imerudi nyuma zaidi hususan katika eneo la da’wah (kuitangaza dini) na kuiletea maendeleo na ustawi wa kweli.

Mwaka mpya na mikakati

Tukiwa mwanzoni mwa mwaka, hatuna budi kuweka maazimio ya kufanya vizuri zaidi kuliko tulivyofanya mwaka jana. Pia, yapaswa tufanye mabadiliko ya dhati na kutengeneza tulipopaharibu.

Mwaka mpya uwe wa kutekeleza majukumu. Katika ngazi ya mtu binafsi, Muislamu anatakiwa atekeleze majukumu yake kwa kuzidisha matendo mema yakiambatana na imani makini, isiyo na hata kivuli cha ushirikina.

Uwe mwaka wa Muislamu kujipinda kisawasawa katika kufanya ibada za ziada (nawafil), zikiwemo sala na funga za sunna. Aisali kila sala kwa wakati wake tena kwa jamaa.

Ibada za dhikri, dua, kumsalia Mtume, kusoma Qur’an, kukaa na wanazuoni n.k lazima ziyaathiri maisha ya Muislamu na ziwe na mkakati wake.

Mifarakano tena basi

Mwaka huu tuwe na azma ya kukomesha na kuzika mifarakano, bughdha, mijadala tasa na migogoro yote inayowakwaza Waislamu kufikia maendeleo yao, katika taasisi na jumuiya zao, misikitini, na sehemu zao za kazi.

Pia uwe ni mwaka wa wanazuoni, wahadhiri na walinganiaji kuungana na kurudisha maelewano, mapenzi, na mshikamano katika harakati zao za kuufundisha Uislamu na kuuendeleza. Pia, watumie umoja wao kuuleta pamoja umma wa Kiislamu,.

Mwaka huu pia uwe wa kuurejeshea Uislamu hadhi na nafasi yake ulimwenguni kote kimfumo na umakini wa sheria na uadilifu wake kwa walimwengu wote chini ya mwamvuli wa: “Laa ilaaha illa Llaah Muhammadu raoulullah.” Uwe mwaka wa Muislamu kuyajua na kujitahidi kuyatekeleza majukumu yake upande wa wazazi, familia, jamaa, majirani, ndugu zake katika imani, na kuwa karibu nao kama alivyoagiza Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na Mtume wake.

Allah anasema: “Na muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote, na wafanyieni ihsani wazazi wawili, na jamaa na mayatima, na masikini na majirani walio karibu na majirani walio mbali na rafiki walio ubavuni na msafiri aliyeharibikiwa..” [Qur’an, 4:36].

Mkakati kwa vyombo vya habari

Mwaka mpya wa 1443 uwe wa vyombo vya habari vya Kiislamu zikiwemo: redio, TV na magazeti, kujipanga na kufanya kazi kwa ushirikiano ndani na nje ya nchina kutafuta njia bora na za kisasa za kuufikisha ujumbe mtakatifu wa Uislamu kwa watu.

Kwa vyombo vya habari, mwaka huu pia uwe wa kuuwelewesha ulimwengu ubora na mazuri ya dini hii tukufu ili waikubali na wajiunge nayo.

Vyombo vya habari kwa mtindo wa kubadilishana uzowefu-havina budi kubuni njia bora na nyepesi za kuyawezesha matangazo yao kuwafikia Waislamu (na wasio Waislamu) popote walipo ili Uislamu ufahamike na uathiri maisha ya watu kila kona.

Huu pia uwe mwaka wa waliojaaliwa na uwezo mkubwa wa mali kuzidi kutoa kwa ajili ya kustawisha vituo vya kuiendeleza dini, vikiwemo madrasa na misikiti, pamoja na kuwawezesha wasimamizi wa vituo hivyo ili wafanye kwa ufanisi zaidi.

Qur’an na mwaka mpya

Huku tukiuanza mwaka mpya, tunapaswa kuzielekeza juhudi na ari zetu mpya kwenye kitabu cha Allah (Qur’an) kwa kukisoma na kuuelewa ujumbe wake, na kuwa na azma ya kweli katika kuutekeleza kivitendo.

Katika kulifanikisha hili, walimu wa madrasa (vyuo vya Qur’an) na wale wafundishao misikitini wanatakiwa kubuni mbinu mpya na rahisi za kuwafundishia watoto/watu jinsi ya kukitamka kwa ufasaha kitabu cha Mola wao, sambamaba na wazazi kuthamini juhudi za walimu hao kwa kuchangia kiasi cha kuwasaidia kukimu maisha yao na familia zao.

Maisha katika ndoa

Wakati tunauanza mwaka mpya, wanandoa walioishi kipindi chote katika migogoro, wanapaswa kuacha tena dharau, kiburi na ukaidi na sasa wafunguwe ukurasa mpya wa maelewano.

Wanandoa pia wanatakiwa warudi katika kutimiziana haki kisheria na kuifanya nyumba yao kuwa bustani mwanana ya kuwalea watoto wao.

Wanandoa wakumbuke kwamba, wao ndio wenye jukumu la awali la kukitunza kizazi chao kitakachokuja kuijenga ama kuibomoa jamii kimaadili na kiuajibikaji. Ni dhahiri kwamba, kama wataendelea kuhasimiana, kamwe hawataweza kusimamia majukumu yao ya kuwalea watoto kimaadili, watakuwa wamepanda mti mbaya utakaozaa matunda machungu yenye harufu mbaya kwa jamii.

Kwa ujumla, Waislamu tunapaswa kuupokea mwaka mpya wa 1443 Hijriyya kwa nia ya kufanya mabadiliko katika kila nyanja ya maisha na kwenda kwenye ufanisi zaidi, na hilo linawezekana kwa uwezo wa Allah. Tuanze sasa hatujachelewa.

Mwisho, tunamuomba Allah aujaaliye mwaka huu uwe wa neema, Baraka na taufiki, atuwezeshe kuyafanya yote aliyotuamrisha na kujiweka mbali na kila alilotukataza. Pia, tunamuomba atufishe tukiwa Waislamu, Amin.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close