1. Tujikumbushe

Msikate tamaa na rehema za Allah

Abu Sa’id al-Khudri (Allah amridhie) amemnukuu Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema alikuwepo mtu mmoja miongoni mwa wale waliokuwepo kabla yenu ambaye aliuwa watu 99, akaulizia mtu mjuzi zaidi katika ardhi, na kufahamishwa kwa mtawa wa kinaswara. Mtu yule akamwendea yule Mtawa na kumwambia kuwa, ameua watu 99. Kisha akamuuliza? ‘Je, ntakubaliwa toba yangu?” (Yule mtawa) akamwambia, hapana.

Yule mtu akamuua na kukamilisha idadi ya watu 100, kisha akaulizia tena mtu mjuzi zaidi katika ardhi, na akafahamishwa kwa mwanazuoni fulani. Mtu yule alimwendea mwanazuoni yule akamwambia kuwa ameua watu 100, na kumuuliza: “Ntakubaliwa toba yangu?” Akamwambia: “Ndio. Nani atakuwa kizuizi kati yako na toba? Nenda katika ardhi fulani kwani katika ardhi hiyo  kuna watu wanamwabudu Allah, nawe  umwabudu Allah wala usirudi katika  ardhi yako kwani hiyo ni ardhi ya uovu.

Akaondoka, mpaka akafikisha nusu ya  safari, umauti ukamjia. Akamgombewa  na Malaika wa rehema na Malaika wa adhabu. Malaika wa rehema wakasema:  “Ametujia akiwa ni mwenye moyo wa  kutubia kuelekea kwa Allah Aliyetukuka.” Nao Malaika wa adhabu wakasema: “Hakika yeye hajapata kufanya kheri kamwe.”

Akawajia Malaika katika sura ya kibinadamu, wakamfanya awe hakimu kati yao. Akasema: “Pimeni masafa yaliyopo kati ya ardhi mbili ile itakayokuwa karibu zaidi ndiyo yake.” Walipopima, wakamkuta yupo karibu zaidi na ardhi aliyokuwa ameikusudia, na Malaika wa rehema wakamchukua. Tukio hili linatupa mafundisho kadhaa wa kadhaa. Hebu tupitie mafundisho hayo.

Usikatie tamaa rehema za Allah
Mkosefu hatakiwi kukatia tamaa na rehema za Allah. Hata kama anahisi ana  dhambi ujazo wa ardhi, ni wajibu kutubia kwa Allah hivi sasa na haraka mno. Allah Aliyetukuka amesema: “Naye ndiye anayepokea toba kwa waja wake, na anasamehe makosa, na anayajua mnayoyatenda.” (Qur’an, 42:23).

Tuombe mwisho mwema
Tunatakiwa tumuombe Allah atupe mwisho mwema. Allah Aliyetukuka  amesema: “Na yakimbilieni maghfira ya  Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyowekwa tayari kwa wachamungu. Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.

Na ambao pindi wafanyapo uchafu au  wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka  Mwenyezi Mungu na wakamwomba
msamaha kwa dhambi zao na nani  anayefuta dhambi isipokuwa Mwenyezi  Mungu?  na wala hawaendelei na waliyoyafanya na hali wanajua. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao.” [Qur’an, 3:133-136].

Hizi ni sababu za kiujumla za kuupata msamaha wa Allah ambazo Allah aliyetuka ametuelekeza kuzikimbilia  wakati wote katika maisha yetu. Suala la kuupata msamaha wa Allah linahitaji  juhudi na kwenda mbio katika mambo  ya kheri kutokana na makosa mengi  ambayo tunayafanya kwa kutambua au  kwa kutotambua.

Tubia kwa Allah toba ya kweli

Mwanadamu ni mwingi wa makosa, hivyo anatakiwa awe mwepesi wa kujirudi na kukimbilia yale yatakayosaidia katika kuupata msamaha wa Allah. Hakika ni maumbile ya mwanadamu kurudia kosa baada ya muda. Hata hivyo, inatakiwa ufanye juhudi nyingi za kuweza kutorudia, lakini ukikosa inabidi urudi utake msamaha kwake. Ikiwa utaweza kutimiza yale masharti ya kusamehewa
basi InshaAllaah! Allaah aliyetukuka atakusamehe.

Jaribu sana utimize masharti yafuatayo: Acha maasia, juta kwa kuyafanya hayo maasia na azimia kutorudia makosa hayo. Na ukiwa umemkosea mwanadamu mwenzako, basi muombe msamaha.

Imam Ibn Al-Qayyim (Allah amrehemu) amesema:

Mtu anayetenda bila elimu ni sawa na yule anayesafiri bila muongozaji, na inajulikana kuwa mtu kama huyu ni mwepesi sana kuangamia kuliko kuokoka. “[Miftaah Daar As-
Sa’aadah, 1/182-83].

Usifutu masuala usiyo na elimu nayo
Fatwa ya mwanachuoni wa kinaswara  ambaye alikuwa hajui hukumu ya kisheria ilimsababishia kifo yeye mwenyewe kwani alimsababisha yule mkosefu akate tamaa na rehema za Allah. Mtu asiye na elimu ni lazima aulize wajuzi ili wampe muongozo sahihi.

Haitakiwi kwa mtu asiyekuwa na elimu  hata kama ni mwingi wa ibada atoe fatwa kwani atawapoteza watu wengi na atajisababishia madhara mwenyewe kama ilivyomtokea huyu mnaswara. Kama angekuwa na elimu, asingeuziba mlango wa toba kwa huyu mkosefu. Mwanazuoni ni sawa na daktari ambaye anamtibu mgonjwa na kumpa matumaini ya kupona.

Jiepushe na marafiki waovu
Mwenye azma ya kutubia kwelikweli anapaswa kuwahama rafiki zake waovu  aliokuwa anaandamana nao, na pia kuy- aacha maeneo na mazingira yaliyojaa  uovu na kuchochea maasi dhidi ya Allah. Mtu anayetaka kutubia afuatane na watu wema ili ajifunze na kuzoea kufanya mema.

Usimdharau mtenda dhambi
Usimdharau mtenda dhambi, vyovyote atakavyokuwa ametenda, bali mpe matumaini ya kusamehewa. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika mtu atafanya matendo ya peponi katika yale yanayoonekanwa na watu hali ya kuwa ni mtu wa motoni.” [Bukhari].

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close