1. Tujikumbushe

Mazingatio Kutoka Hijja

Ni wajibu wetu kutambua kuwa katika safari ambayo mwisho wake ni kukutana na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka atulipe tuliyoyatanguliza kwake, Mwerevu ni yule anayetumia nguvu, afya na mali yake katika yatakayomnufaisha hapo baadae.

Mjanja zaidi ni anayetumia fursa za nyakati bora kwani masiku yenye ubora humalizika haraka. Chonde chonde, tusibakie na umaskini wa ugumu wa nyoyo, kupoteza muda na kuchezea fursa ya umri.

Kwa mantiki hiyo, mwenye kutekeleza ibada yoyote afikirie undani na mazingatio ya kila hatua anayoipitia ili uthabiti katika utekelezaji wa maamrisho ya Allah ufikiwe. Ni hakika, hakuna alilotufaradhishia Allah ila ndani yake kuna hekima na mazingatio.

Yapo mazingatio mengi na makubwa kwa mwenye kutekeleza ibada ya Hijja katika kila hatua na mzunguko mzima wa ibada hiyo.

Ihramu ikukumbushe sanda
Wakati hujaji mwanaume, anapohirimia, huondosha mavazi ya kushonwa aliyokuwa ameyavaa ili, kwanza, kutekeleza maamrisho ya Allah na pili, tukio hili hutukumbusha mavazi ambayo mwanadamu atavaa kuelekea nyumba ambayo tutaiendea hivi karibuni, yaani kaburi.

Hazikuwa shuka mbili za ihramu isipokuwa ni mfano wa sanda ambazounazivaa na kutembea nazo iwe mazingatio na ukumbusho kuwa hiki ndio kitu pekee katika mali za ulimwengu ambacho utaandamana nacho kaburini, hata kama una mavazi ya kifalme. Huko hakitakufaa kitu katika mali yako ila matendo mema. Allah anatuambia kuhusu siku hiyo:

“Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa,” [Qur’an, 2:281].

Ka’aba: Kituo cha ulinganiaji
Ukifika Makka, ukiitazama Nyumba Tukufu, yakumbuke masiku adhimu yaliyopita na historia iliyofungamana na nyumba hii.

Tangu zama hizo wengi wamepita, kama wewe unavyopita, wamerejea kwa Mola wao ima wakiwa wema au waovu. Fikiri, je utakaporejea, baada ya kuafikishwa kufika katika eneo hili tukufu, unajiandaa kuwa mtu wa namna gani ili kujiandaa kwa maisha ya Akhera?

Kumbuka kuwa, Nyumba Tukufu, Kaaba, ni katika vituo vya mwanzo vya ulinganiaji wa Uislamu. Katika nyumba hii, alisujudu Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Maswahaba (Allah awaridhie) walikuwa hapo na walifanya heri za aina mbalimbali.

Kwenda Mina kwa ajili ya ibada za huko ni ishara ya kuheshimu matukufu ya Allah na kutekeleza amri za Allah. “Ndio hivyo! Na anayetukuza Matukufu ya Allah, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo,” [Qur’an, 22:32].

Arafa ishara ya kisimamo
cha Kiyama
Umeenda kando ya mji kwa ajili ya mpaka viwanja vya Arafa kusimama na watu wote katika hali ya joto kali na jua linalowaka. Hili likukumbushe siku ambayo watu wote watasimamishwa mbele ya Mola wa walimwengu wote. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema: “Katika siku iliyokuu, siku watapomsimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote?” [Qur’an, 83:8-9].

Makadirio ya urefu wa siku hiyo moja ni sawa na siku elfu 50 za hapa duniani. “Malaika na Roho hupanda kwendea kwake katika siku ambayo kadiri yake ni miaka 50 elfu! [Qur’an, 70:4].

Hali ya mtu siku hii inategemeana na matendo yake kwani jasho litakalowatiririka watu, hilo la Uwanja wa Arafa si kitu.

Wapo ambao jasho litawafunika, wapo ambao litawafikia katika vifundo vyao vya miguu au magotini au mabegani au shingoni. Wapo pia watakaofunikwa moja kwa moja (Allah atulinde na adhabu za siku hiyo). Ukiacha watakaofunikwa na jasho kwa viwango tofauti, wapo watakaofufuliwa pamoja na manabii, mashahidi, wa kweli pamoja na watu wema.

Ukiwa katika viwanja hivi, kumbuka kuwa, Malaika wa Allah wanateremka katika katika Viwanja vya Arafa siku hii ya tarehe tisa Dhulhijja. Hivyo, Fanya Istighfaar kwa wingi na tubia kwa Allah, huku ukiwa na mategemeo kuwa wewe ni miongoni mwa waja wema ambao Allah atajifaharisha nao mbele za Malaika na utarajie kuachwa huru na moto.

Watu wanapomiminika Muzdalifa kutoka Arafa wakiwa wamechoka kutoka na na kisimamo cha Arafa, nawe ukiwa miongoni mwao, kumbuka siku ya kufufuliwa na hali ya kutawanyika watakayokuwanayo watu: “Siku atakapoita muitaji kuliendea jambo linalochusha. Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika,” [Qur’an, 54:6-7]

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close