1. Tujikumbushe

Masheikh watakiwa kujipamba sifa njema

Viongozi wa dini ya Kiislamu wameombwa kujipamba na sifa njema zitakazowafanya waaminike na kuwa mfano bora kwa jamii kama mafundisho ya Uislamu yanavyohimiza. Wito huo umetolewa na masheikh mbalimbali wakati wa mhadhara ulioandaliwa na kituo cha Kimisri cha hapa nchini (Az-har Sharif ) na kufanyika katika chuo cha Nur As-Sunna, Bunju jijini Dar es Salaam.

Akiongea katika mhadhara huo, Sheikh Saidi Abdul-Khaliq Al-Shimiy, kutoka katika kituo hicho alisema kuwa baadhi ya Waislamu wamekosa imani na viongozi wao kutokana na matendo yasiyopendeza kutoka kwa baadhi ya viongozi hao.

“Matendo ya baadhi ya viongozi wetu wa dini yanasikitisha sana, hayapendezi. Hii imefanya Waislamu wawatilie mashaka viongozi hao kama kweli wanastahili kuitwa viongozi,” alisema Sheikh A-Shimiy.

Sheikh Al-Shimiy ambaye alitoa mada iliyopewa kichwa cha habari: ”Umuhimu wa kuwepo Mfano Bora katika Maisha ya Muislamu,” amesema kuwa kiongozi wa Kiislamu hana budi kuwa na tabia njema kwani wao ni kioo cha jamii. Naye Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Misri, Sheikh Mohammed Hassan Attiya amesema kuwa kituo hicho lengo lake ni kueneza Uislamu sahihi na ikiwemo kuwahimiza Waislamu katika masuala ya maendeleo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya chuo hicho cha Nur As-Sunna, Mwalimu Mkuu, Sheikh Yussuf Abdullah alipongeza juhudi za kituo hicho cha Kimisri akisema kinafanya kazi kubwa ya kueneza fikra na ufahamu sahihi wa Uislamu.

Sheikh Abdullah aliongeza kuwa wamejifunza mengi katika mhadhara huo na kusema wao kama viongozi watazingatia yaliyosemwa. “Yamezungumzwa mengi hapa, sasa ni wajibu wetu kuyatekeleza kwa vitendo ili jamii inufaike kupitia kwetu,” alisema Sheikh Abdullah.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close