1. Tujikumbushe

Madhara ya hiyana katika ndoa

Mahusiano ya mwanamume na mwanamke ajnaby (nje ya ndoa), watu huyaita ‘hiana’ yaani kukosa uaminifu katika ndoa. Hata hivyo, katika Uislamu mahusiano hayo yameitwa ‘zinaa’ yaani ni mtu kumwendea kimatamaniyo mwanamke asiye mkewe.

Allah ameielezea zinaa kuwa ni uchafu na ni njia mbaya zaidi ya kutuliza joto na utashi wa kijinsia. Allah anasema:

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya. [Qur’an, 17: 32].

Utafiti unaonesha kuwa, zinaa  kama ilivyoelezwa katika Qur’an ni njia mbaya zaidi na ina madhara mengi. Madhara ya zinaa yakiwemo ya kiafya, kifamilia na kijamii  yameshachambuliwa na wasomi, waandishi na watafiti wengi katika vitabu na machapisho mbali mbali.

Tunachotaka kukigusia katika makala yetu hii ni jinsi ya utendaji zinaa unavyogharimu, kumsumbua na kumshusha hadhi mzinifu ikiwa ni sehemu ya adhabu hapa duniani kwa vile amechagua kupita njia mbaya zaidi.

Zinaa inavyofanyika kwa siri

Kimsingi, utendaji zinaa ni siri pevu hususan kwa wanandoa. Mume anapotaka kuwa na mahusiano na mwanamke fulani na watu wasimgundue, wa kwanza kumficha ni mke wake. Mume huelewa vyema kwamba iwapo mke atafahamu mahusiano hayo, atakasirika vibaya sana na kuwasha moto mkali nyumbani.

Nyumba nyingi zenye waume wazinifu haziishi migogoro, matusi na dharau kwani upepo mbaya wa uzinzi huzivumia nyumba hizo na kuziyumbisha nguzo za ndoa. Mume mzinifu anaelewa fika kuwa mkewe akijua kuwa ana anachepuka, basi mwanamke huyo atamuasi, ataparaganya maisha yao au atamkimbia kabisa na kurudi kwa famalia yake.

Zaidi ya hayo, mke kama ana imani dhaifu anaweza kutamani kulipiza kisasi kwa naye kwenda kwa mwanamume mwengine. Mume akigundua hili, huwasha moto wa hasira na wivu huku akisahau kwamba yeye ndiye aliyeanza kumfanyia khiana mkewe. Anasahau kuwa yeye mwanamme alipaswa kunyooka ili mkewe naye anyooke.

Kuhusu hili, Imamu Ali (Allah aridhie) anawaasa wanaume kwa kusema:

“Jiepusheni na uchafu wa zinaa na wanawake zenu watajipesha, na jiepusheni na mambo yasiyofaa kwa Muislamu. Zinaa ni deni. Ukikopesha, utalipwa hata kwa watu wa nyumbani mwako. Atakayezini naye ataziniwa hata kwenye kuta za nyumba yake ( jamaa zake).”

Licha ya baadhi ya wataalamu kuitilia shaka hadith hii, mafunzo yake yanaendana na ukweli na uzoefu kwani kwa kawaida mtu anapowafanyia wengine dhuluma, basi Allah humlipa mtu huyo kwa kumtia katika majaribu ya watu kumfanyia vibaya yeye mwenyewe au watu wa familia yake.

Zinaa huzaa uongo

Na ili mwanandoa mwenzake asigundue uchafu anaoufanya, mwanamme mzinifu atalazimika kusema uongo katika mambo yake mengi. Anaweza kumdanganya mkewe kuwa anasafiri au amezidiwa na shughuli hivyo atachelewa kurudi kazini, kumbe yuko katika viwanja haramu. Hapa atakuwa amejiingiza katika dhambi nyengine kubwa (uongo).

Huzaa taklifa

Bila shaka mume atalazimika kumgharamia mwanamke anayezini naye. Anaweza kutumia fedha zaidi ya matumizi ya nyumbani kwake ili amridhishe mpenzi wake haramu wakati akielewa fika kuwa fedha hizo ambazo zinahitajika kwa ustawi wa familia yake. Hili nayo ni adhabu ya dunia kwa mzinifu.

Zinaa huchafua jina la mume (mzinifu)

Mzinifu hupoteza sifa, murua na uaminifu pindi watu wa nyumbani kwake, hasa mkewe, wanapombaini. Mwanamme hupoteza haiba yake mbele ya marafiki, wafanyakazi wenzake na majirani zake. Hata wakuu wake kazini wanakuwa hawamuamini tena. Hii ni kwa sababu amekosa uaminifu kwa mkewe.

Madhara haya mbalimbali tuliyoyataja kwa pamoja humjengea mume mazingira magumu sana katika maisha yake. Mwanamme hubaki katika wasiwasi, mashaka na simanzi na anakuwa amejiingiza katika shimo la hatia isiyompa raha na utulivu. Hii ndiyo mana ya kauli ya Allah:

“. zinaa ni uchafu na ni njia mbaya kabisa.”

Adhabu ya mzinifu

Mume, kabla hajafikiri kwenda kuzini anapaswa kukumbuka kwamba iwapo ushahidi ukisimama adhabu yake hapa duniani ni kupigwa mawe hadi kufa. Hata adhabu hii isipotekelezwa hapa duniani kwa sababu ya ujanja ujanja wa mtu kuikwepa au mamlaka za dunia kuikataa, haina maana kwamba Allah ameisahau. Lahasha, ifahamike kwamba, wahusika watawajibishwa tu Siku ya Kiyama.

Kuendelea na dhambi iliyopangiwa adabu hapa duniani kama zinaa, huku mtu akijitahidi kujificha na ikashindikana kusimamishiwa hadi Kiyama ni kujilimbikizia uzito wa adhabu itakayomkuta huko Akhera. Ndiyo mana tunawakuta watu walioteleza na kuingia katika hatia hii wakati wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) walijisalimisha katika mahakama yake na kusimamishiwa adhabu kabla ya siku hiyo nzito. Ilikuwa kama namna fulani ya kuizimua.

Imesimuliwa kwamba, Maaiz bin Malik al-aslami alikuwa yatima akilelewa na Hazala bin Nuaim. Ikatokea Maaiz kuzini na kijakazi fulani. Hazaala akamuelekeza Maaiz aende kwa Mtume na kumueleza alichokifanya huenda (Mtume) atamuombea (Maaiz) msamaha ili yaishe.

Maaiz alimkuta Mtume msikitini akamwambia: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, mimi nimezini.” Mtume akamwambia “Wewe, hebu rudi nenda kamuombe msamaha Mwenyezi Mungu” na akageuza sura yake pembeni. Maaiz akazungukia upande wa uso wa Mtume na kumwambia tena: “Mimi nimezini.” Mtume akarejea kumwambia tena tena: “Nenda kamuombe msamaha Mola wako” na kugeuza sura yake pembeni. Maaiz akamwambia tena kwa mara ya tatu: “Ewe Mjumbe wa Allah, mimi nimezini, basi nitwaharishe.”

Katika kisa hiki, tunaambiwa kwamba Mtume alimuuliza Maaiz maswali kadhaa ili athibitishe kutokea maana haswa ya zinaa. Kisha akaamrisha Maiz achukuliwe na apigwe kwa mawe. Akapigwa mpaka akafa. Baadae, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alisikia baadhi ya Maswahaba wakimtaja kwa vibaya kutokana na dhambi aliyoifanya. Mtume akawaambia:

“Maaiz ametubia toba ambayo lau ingeligawiwa kwa umma mzima ingeliwaenea.” [Bukhari].

Jambo la msingi ni kuacha kupita njia mbaya ambayo ameifunga ili watu waepukane na maafa yake hapa duniani na huko Akhera.

Allah ndiye mjuzi Zaidi

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close