1. Tujikumbushe

Kwanini uhudhurie Misk ya Roho?

Kulikosa kongamano hili ni kujidhulumu…

Kongamano la Misk ya Roho ni moja ya makongamano makubwa kuwahi kufanyika katika historia ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla kwa kuwa huhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka kila kona ya jiji la Dar Es Salaam na viunga vyake, mikoa mbali mbali ya Tanzania na pamoja na nchi za jirani ukiachilia mbali halaiki ya watu inayofuatilia matangazo yanayorushwa mubashara katika vituo mbalimbali vya runinga na redio duniani kote.

Ni watanzania wachache sana au wana Afrika mashariki wa kawaida wanaoweza kumudu kuhudhuria mihadhara na makongamano yanayofanyika katika nchi zote za Afrika Mashariki ili kustafidi na kupata ladha tofauti za masheikh wa nchi hizo kwa wakati mmoja kutokana na sababu za uchache wa kipato na muda, lakini kupitia kongamano hili tunaweza kuwapata masheikh wengi kutoka nchi zote hizo katika mimbari moja, hii ni fursa adhimu sana.

Kuna sababu anuai zinazoonesha umuhimu wa kuhudhuria mihadhara, warsha na makongamano mbalimbali yanayoandaliwa na taasisi za kiislamu ambayo kwa kiasi kikubwa huchangia kuchagiza mwamko wa umma wa kiislamu hasa katika zama hizi ambazo jamii tunayoishi imekumbwa na baa la ujahili.

Ingawa dhumuni kuu la kongamano hili ni kulingania, lakini ulinganiaji unaweza kuwa ni nyenzo ya kuchochea mambo mengine kama kujuana, kujenga urafiki na kukutana na watu waliopoteana kwa muda mrefu, kwa maana hiyo kongamano hili pia ni uwanja wa kujenga udugu wa kiimani. Kwa mtazamo wa haraka haraka Misk ya Roho huweza pia kutumika kama jukwaa la kuunga mahusiano ya kindugu, kibiashara na nyanja nyingine yoyote iwayo.

Kama ilivyoelezwa na mmoja wa masheikh waliohudhuria kongamano la kwanza la Afrika Mashariki kuwa pamoja na kuwa yeye ni sheikh anayeheshimiwa sana huko kwao lakini hakuwahi kuwa na muamala wa karibu na baadhi ya masheikh wa nchi nyingine, hivyo alipata fursa ya kukaa nao, kubadilishana fikra na kutanua mawanda yake ya kutoa daawah katika nchi nyingine.

Kongamano la Misk ya Roho pia kwa upande mwingine linaweza kuwa kama sehemu ya kukutana pamoja waislamu wa Afrika Mashariki ambapo huwaleta pamoja waumini na viongozi wao na kujadili mambo mbalimbali yanayoikumba jamii yetu kwa ujumla ambapo mijadala hiyo kama itatiliwa maanani na hadhira basi kwa kiasi kikubwa huweza kuleta mabadiliko chanya katika ngazi ya familia na mataifa yetu kwa ujumla.

Tunapoangazia umuhimu wa kongamano hili ni vyema pia kuyatupia macho manufaa yapatikanayo katika mada zinazowasilishwa ambazo kwa kiasi kikubwa zinaigusa jamii moja kwa moja na zinalenga kujenga mustakabali mwema wa jamii zetu, mfano rejea ni mada zilizosheheni kwatika kongamano la kwanza la Misk ya Roho la mwaka 2017 ambapo mada zilizosheheni ni Jinsi ya kuwa na Ikhlaas, Umuhimu wa Elimu, na Thamani ya Amani. Pia katika kongamano la pili la Misk ya Roho mwaka 2018 mada zilizosheheni ni kuhusu “Utukufu Wake” Allah (Subhanahu Wata’ala). Mada kuu itakayorindima mwaka huu ni “Kitabu Changu”.

Kwa upande wa wafanyabiashara halali wa kiislam ambao kwa kipindi kirefu wamekosa sehemu ya kutangaza biashara zao kwenye vyombo vinavyowafikia moja kwa moja wanajamii kongamano hili pia ni fursa ya dhahabu kwao kuifikia jamii kwa kuungana na waandaaji (The Islamic Foundation) wa makongamano haya.

Kongamano la Misk ya Roho pia ni sehemu mbadala ya vijana kustarehe na kufurahi katika namna ambayo Allah anaipenda na kuiridhia, tofauti na ilivyozoeleka ambapo sehemu nyingi ambazo vijana wanapenda kufurahi kwazo ni sehemu batili na potofu.

Familia nazo zinaweza kutumia kongamano la Misk ya Roho kama siku maalum ya kutoka kwa pamoja (outing) ambayo itakuwa ni tofauti na ada kwa jamii zetu hivyo kujenga mahusiano mazuri kwa familia zetu na kuwazoesha wanafamilia kuhudhuria vikao vyema.

Ni kheri iliyoje kuwa mmoja ya waliohudhuria au waliodhamini kikao ambacho ndani yake anatajwa Allah na mtume wake, bila shaka ni kitu kizuri chenye manufaa ambacho hakuna kati yetu anatamani kukosa kheri zake, tuazimie sasa kuwa wadau wa kwanza wa kongamano hili na mengine mengi yanayoandaliwa kwa ajili yetu.

Kongamano la Misk ya Roho litafanyika (In shaa Allah) mnamo tarehe 1/12/2019 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar Es Salaam, unaweza kuhudhuria kongamano hili kwa kujipatia tiketi yako katika vituo vilivyotajwa au kulipia kwa njia ya mitandao ya simu (Tigo Pesa au M-Pesa) kupitia nambari 0718000433 au 0742877775 (Hakikisha jina ni Tajmohamed Shaaban).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close