1. Tujikumbushe

Kumbukizi Ya Misk Ya Roho 2018

Mapenzi ya Allah kwa Mja

Wasifu wa Sheikh Zuberi Bizimana

Sheikh Zuberi Bizimana ni mzaliwa wa Buyenzi, nchini Burundi. Alisoma Elimu ya dini ya Kiislamu katika Chuo cha Kiislamu cha Muhammad bin Saudi nchini Saudi Arabia. Sheikh Zuberi Bizimana pia ana Stashahada ya Rasimilimali Watu.

Tunamshukuru Allah kwa kutukutanisha katika safu hii leo tukiwa na siha njema, walio wagonjwa tunamuomba Allah awape afwu. Ni furaha yangu leo katika safu hii kuwaletea kumbukumbu ya muhadhara  wa mhadhiri nguli Sheikh Bizimana katika Kongamano la Pili la Afrika Mashariki lijulikanalo kama Misk ya Roho, 2018.

Ambatana nami katika kudurusu walau kwa uchache maudhui ya hotuba yake chini ya anuani: “Mapenzi ya Allah kwa mja.”

Sheikh Bizimana alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungi Aliyetukuka pamoja na kumswalia kipenzi chetu Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie). Pia, alishuhudia kwamba, Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah Ta’ala na kwa hakika Muhammad ni Mtume wake.

Sheikh Bizimana alianza kwa kusoma Aya mbili za Qur’an, (Surat Albaqara 2:259-260) ambazo zimeongelea kisa cha Uzair na kisa cha Nabii Ibrahim. Kijana Uzair, aliyekuwa katika matembezi katika mji wa Palestina, alifika katika mji mmoja na kukuta watu wote katika mji huo pamoja na wanyama wamefariki. Pia, alikuta mimea imekauka. Aliutazama mji ule, akistaajabu na kusema: “Je Allah Ta’ala anaweza kuurudisha mji huu uliokufa, na kuupa uhai tena?”

Palepale, Allah Ta’ala alimtuma Malaika Jibril (amani ya Allah imshukie) kuja kuiondoa nafsi ya Uzair. Akafariki, kama watu wengine katika mji ule. Allah Ta’ala aliacha maiti yake katika mji ule kwa muda wa miaka 100 (mia moja), kisha akamfufua. Katika safari yake, Uzair alikuwa na punda pamoja na chakula na vinywaji.

Uzair alipoamka akaulizwa anahisi ni muda gani alikuwa katika mji huo? Naye akajibu “Siku moja au sehemu katika siku.” Akaambiwa, tazama chakula chako na vinywaji vyako, vyote ambavyo vilikuwa katika hali nzuri hata havijaharibika. Kisha akaambiwa, mtazame punda wake. Alikuwa kaoza kabaki mifupa tu. Akambiwa, sasa tazama ambavyo mifupa hii itakavyoamka. Palepale, mifupa ile ilinyanyuka mbele ya Uzair, na kisha Allah Ta’ala akaivalisha nyama.

Sheikh Bizimana aliendelea kuelezea utukufu wa Allah Ta’ala kwa kuelezea kisa kingine. Hiki kilimuhusu Nabii Ibrahim (amani imshukie), ambacho kimetajwa katika Qur’an, Surat Baqara [2:260].

Nabii Ibrahim alimuuliza Allah Ta’ala: “Vipi kilichokufa kinaweza kuwa hai? Allah Ta’ala akamuuliza: “Haujaamini tu kama yote hayo nayaweza?” Nabii Ibrahim akamwambia: “Naamini, ila nataka utulivu wa moyo wangu.”

Akaambiwa Nabii Ibrahim atafute ndege wanne tofauti, awafuge, wamjue naye awajue, pia awape majina. Kisha, awachinje na kuwakatakata vipande vidogo vidogo, halafu  avichanganye na kuwagawa mafungu manne, kila fungu aliweke katika mlima tofauti. Hata hivyo, yeye, Nabii Ibrahim alitakiwa kubaki na vichwa vya ndege wale mkononi.

Allah Ta’ala alimtaka Nabii Ibrahim awaite kwa majina aliyowapa na ndege hao wangekuja kwake kwa kutembea. Nabii Ibrahim aliwaita mmoja mmoja, na wale ndege walimfuata huku wanatembea. Walipofika kwake, alikuwa akiwawekea vichwa ambavyo sio vyao, nao ndege wale wakawa wanakataa hadi kila mmoja alipowawekea kichwa chake sahihi.

Baada ya visa hivi viwili vya kuonyesha tukufu wa Allah Ta’ala, Sheikh Bizimana alitoa kisa kingine cha kipenzi chetu Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Sheikh Bizimana alisema, kuna siku Mtume wetu (rehema za Allah na amani zimshukie) alikaa na Maswahaba zake, akiwafundisha mawili matatu, akatokea Myahudi mmoja, akasimama mbele yao huku kajishika kiuno na kusema: “Muhammad, Nabii Issa alikuwa akifanya miujiza, na mie sitokuamini mpaka utufanyie muujiza mmoja.”

Maswahaba walitaka kumpiga lakini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwakataza na kunyanyua macho yake juu. Mbele yake kulikuwa na mti mkubwa. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akauzungumzisha mti ule: “Ewe mti, nakuomba kwa ajili ya Allah toka hapo ulipo na usogee karibu yangu.” Ule mti ulitoka pale ulipo, na ukubwa wake na uzito wake mpaka mbele ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na ukamsujudia.

Yule Myahudi kwa mshangao uliompata akataka kumsujudia Mtume, lakini Mtume alimkataza na kumwambia: “Laiti ningekuwa naweza kumuamrisha mtu amsujudie mwezie, basi ningeamrisha mwanamke kumsujudia mume wake.”

Sheikh Bizimana alituasa tunapokuwa kwenye mazungumzo yetu hasa ya vijiweni tusimuingilie Allah na kazi zake.  Sheikh akatupa hekaya (si katika Aya wala Hadithi) ya kisa cha kijana aliyejulikana kwa jina la Saad.

Kijana huyu alikuwa akifanya kazi za kusukuma toroli. Siku moja wakati wa Jua kali, akiwa na wenzake watatu aliwaambia: “Ndoto yangu ni kuwa kiongozi.” Wale wenzake walicheka sana.

Akawauliza rafikize, watataka nini kwake akiwa kiongozi. Mmoja wao akasema anataka nyumba ya kifahari, mwengine akasema anataka wanawake kumi warembo na watatu akasema: “Wewe ukiwa kiongozi, nipeleke sokoni, nivue nguo zote nichapwe viboko na baada ya hapo nifungwe kamba kwenye punda aniburuze soko zima.”

Baada ya mazungumzo hayo, nchi hiyo ikahitaji wanajeshi; Saad akajiandikisha. Baada ya kazi nzuri vitani, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi, kisha akawa mshauri wa mfalme. Kisha Mfalme alifariki akiacha mtoto wa miaka minne. Hivyo, ikabidi achaguliwe mtu atakayekaimu ufalme mpaka mtoto huyo atakapofikia makamo ya kuweza kutawala mwenyewe;  na hapo Saad akateuliwa kukaimu ufalme.

Saad aliamrisha wale rafiki zake watatu watafutwe na waletwe mbele yake. Hawakuamini macho yao walipomuona Saad kwenye kiti cha ufalme. Akawauliza: “Munakumbuka ahadi zetu?” Kisha, wote walipewa kile walichoomba wapewe iwapo Saad angekuwa kiongozi.

Sheikh Bizimana alimaliza kwa kusema kuwa tungeweza kuongelea utukufu wa Allah Ta’ala umri wetu wote bila kumaliza, lakini muhimu ni kuwa, Muislamu wa kweli ni yule anayemtanguliza Allah katika kila jambo.

Huo ndiyo muhtasari wa hotuba ya Sheikh Bizimana katika Misk ya Roho 2018. Unaweza kutazama muhadhara huu kupitia kiungo hiki: Bonyeza Hapa, wakati tukijiandaa kuipokea Misk ya Roho 2019.

Ungana nasi katika matoleo yajayo upate ufupisho wa mada zilizowasilishwa na wahadhiri wengine.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close