1. Tujikumbushe

Kumbukizi ya Misk ya Roho 2018…

Wasifu wa Sheikh Abdulrahman B. Mhina (Baba Kiruwasha)

Ni Sheikh aliyejipambanua kwa weledi wa kufundisha mambo ya malezi, ndoa na familia, amekuwa akikonga nyoyo za wengi hasa kwenye vipindi vya redio na televisheni, alisoma katika chuo kikuu cha Imamu Muhammad, Saudi Arabia. Ana stashahada ya lugha ya kiarabu. Ni mwalimu wa malezi kituo cha Ibn Jazar Sekondari pia ni muandaaji wa vipindi vya ndoa na malezi.

Miongoni mwa neema alizotutunuku Allah na tunazotakiwa kumshukuru kwa ajili ya kutubariki nazo ni uhai, afya na uzima.

Mhadhiri tutakayemzungumzia leo ambae nae alikuwepo kwenye Misk Ya Roho 2018 ni Sheikh kutoka Tanzania anayeitwa Sheikh Abdulrahman Mhina ila jina lake maarufu ni “Baba Kirwasha”.

Sheikh alianza muhadhara kwa kusoma aya ya Qur’an (30:21) “Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye  amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri”.

Miongoni mwa dalili zinazotufahamisha ukubwa na uwezo wa Mwenyezi Mungu pamoja na kustahiki kwake yeye kuabudiwa na asiabudiwe yeyote ni kule wanaume kuumbiwa wanawake kutokana na jinsi yao. Allah amefanya hivyo ili nafsi zipate kutulizana. Laiti kama Mwenyezi Mungu angewaumba wanaume watupu au kama angeumba wake kutokana na jinsi au namna nyingine, mfano wakawa hao wanawake wanatokana na majini au wanyama kusingekuwepo na mazoea au kupendana baina yao na wanaume.

Baada ya hapo, akasimulia kisa kifupi cha baba yetu Adam (Alaihi salaam). Mwenyezi Mungu alimuumba Nabii Adam kisha akamuweka Peponi wakati yupo huko, na ni sehemu ambayo ipo na kila kitu ila bado alikuwa akihisi upweke. Kutokana na Allah kuwa ni mwenye hekima na aliye na elimu zaidi kuliko sisi sote aling’amua kuwa Nabii Adam hawezi kukaa peke yake kwa sababu ni yeye (Mwenyezi Mungu) peke yake ndiye mwenye uwezo wa kuwa pekee na limethibitika hili katika Surah Al-ikhlas aya ya mwanzo [Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee] pamoja na hilo surah hii imeendelea kuonyesha kwamba Allah yuko peke yake,hakuzaa wala hakuzaliwa tofauti na namna binadamu alivyo.

Hivyo basi ili Allah kuonyesha upendo kwa kiumbe wake huyu (Nabii Adam) kwanza akampa usingizi, wakati amelala Mwenyezi Mungu akamuumba mwanamke kutokana na ubavu wa Adam. Alipoamka akamuona mtu kama yeye, baada ya kumuangalia akamuuliza “Ni nani wewe?”. Yule kiumbe akajibu “Mimi ni mwanamke”. Nabii Adam akamuuliza tena “Kwa nini umeumbwa?”, yule mwanamke akajibu “Mimi nimeumbwa ili wewe utulizane kwa sababu ulikuwa huna utulivu”.

Hiyo ndio sababu pia ya Allah kumpamba mwanamke na miongoni mwa alivyopambwa navyo mwanamke ni sauti yake, ulaini wa mwili wake, umbile lake pamoja na kuwa na asili ya yeye mwenyewe kupenda kuvaa marembo/mapambo. Akayakazia maneno yake kwa hadithi “Dunia ni starehe,na uzuri wa starehe hiyo ni kuwa na mke mwema”. Mwanamke ni neema lakini sio wote wanaolifahamu hilo. Kuna watu huwapiga wake zao, hivyo kweli ndivyo tunavyozithamini neema zetu?

Sheikh akaongeza kuwa hata uwe na mali kiasi gani katika maisha yako bado utakuwa haujakamilika mpaka uwe na mke na kuna watu ambao hawana pesa wala chochote cha thamani lakini ana mke mwema na mzuri na anaonekana ameridhika sababu ya ile raha ya moyo aliyokuwa nayo. Kutokana na mwanamke kuwa ni neema lazima tutafakari vipi tunaishukuru neema hiyo. Akakumbusha msemo wa kiswahili unaosema “Kitunze kidumu” na akasema hata katika dini yetu tumeaswa kuishi na wake zetu kwa wema na tuwatunze kama alivyosema Allah katika Qur’an (4:19) “…na kaeni nao kwa wema…”

Akiendelea kuifafanua aya ya Quran (30:21) Sheikh alielezea kwa kifupi hayo mawadda (mapenzi) kuwa ni mwanaume kumpenda mke wake na rahma (huruma) ni kule kumuonea mkeo huruma asifikwe na mambo mabaya.

Kuudhihirisha ukubwa wake Allah, ndio akayaleta hayo (upendo na huruma) baina ya mke na mume. Akasisitiza kuwa upendo haupatikani nje ya ndoa bali ndani ya ndoa. Mwenyezi Mungu amejaalia iwe hivyo kutokana na rehma zake. Akakumbusha kuwa upendo na kuoneana huruma ndio siri ya maisha mazuri na yenye raha katika ndoa ikiwa hakuna upendo maisha ya ndoa yanakuwa ni moto usiowezekana kuuzima. Kwenye amani ndio kwenye upendo, na kwenye upendo ndio kwenye amani.

Upendo aliouweka Allah baina ya mume na mke ndio rasilimali ya maisha ya ndoa. Upendo ndio unaoendesha maisha ya ndoa, kama ukikosekana upendo basi maisha ya ndoa yanakuwa yapo ukingoni.

Baba Kiruwasha akaweka msisitizo wa wanaume kujitahidi kuuendeleza upendo aliouweka Allah baina yao na wake zao kwa kutafuta vitu ambavyo vinaleta upendo kisha akaanza kuchanganua upendo wa kweli hasa ni upi, upendo ambao mtu atafurahi akiupata. Ni ule upendo wa halali kinyume na hapo upendo wowote ule utakuwa sio upendo wa kweli na wala hautoleta tija (faida).

Upendo wa kweli ni ule ambao watu hawapendani kwa maslahi ya dunia. Usimpende mtu kwa sababu ya uzuri kwa sababu yeye ni binadamu inaweza kutokea siku akaumwa, akapata ajali au akakutwa na mtihani wowote na uzuri ukapungua au kumpenda mtu kwa mali kwani upendo huo hautodumu na kila siku utakuwa ukichagua mwingine, kwa sababu kuna watu wanazidisha mali kila siku. Upendo wa kupendana kwa maslahi sio upendo, ni upendo feki.

Ili watu waelewe zaidi yale aliyokuwa akiyasema tangu mwanzo wa mhadhara wake alimtaja Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) kama mfano wa kuigwa wa mtu aliye na upendo wa kweli. Alikuwa akipenda, anapenda kwelikweli. Watu hasa wanandoa wanatakiwa wapendane kikweli na itakapotokea tatizo inabidi wahurumiane zaidi. Ikitokea mume ameenda hospitali na mkewe na akagundulika kuwa ni tasa inatakiwa huruma ndio izidi kutoka kwa mumewe, kwa sababu na yeye (mke) anataka apate mtoto sio kama hataki lakini hayo yote ni makadirio ya Allah.

Lakini wengine hunyanyasa wake zao kwa sababu ya masuala kama hayo na hufanya hivyo kwa sababu ya kukosa mapenzi ya dhati. Akaonya wanaume wasiyafanye hayo na wapendane na wenza wao kikweli sio tu kudanganyana kwa maneno. Alisema kuwa Mtume alimpenda sana Bi. Khadija hata baada ya kufa kwake alikuwa haishi kumtaja na kufanya mambo kwa ajili yake kwa kiasi ambacho kilimfanya Bi. Aisha ahisi wivu. Hivyo ndivyo Mtume (rehma na amani ziwe juu yake) ametupa funzo la kupendana kwa ajili ya Allah.

Alifanya hitimisho la muhadhara wake kwa kutuomba, kutusihi na kutukumbusha kupendana kikweli na upendo wa kweli haupatikani ila kwa waliomcha Mungu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close