1. Tujikumbushe

Kumbukizi Ya Misk Ya Roho 2018

Ndio Nina Bashiria Utukufu Wa Allah…

Wasifu wa Sheikh Yusuf Abdi

Alifunzwa Qur’an na kuhitimu akiwa na miaka 7, alianza kuhutubu akiwa na umri wa miaka 14, alikuwa makini na kufanya vizuri katika masomo yake ya dini. Ni mfano wa kuigwa na mmoja wa wahamasishaji wakubwa wa vijana Afrika Mashariki. Amekuwa Khatibu na Imam katika misikiti mingi huko nyuma, ni muasisi wa mfumo mpya wa nasheed Afrika Mashariki, ni mtunzi wa mashairi na mbunifu wa lahani pia ni muasisi wa studio ya Sauti Afrika.

Karibu tena katika safu ya Kumbukizi Ya Misk Ya Roho 2018. Hatuna budi kumshukuru.Allah aliye mku ,kwa kutupa afya na uzima mpaka kufikia leo hii.

Leo tutayapitia machache kati ya mengi yaliyowasilishwa na Sheikh Yusuf Abdi katika mada yenye anuani ya “Ndio Nina Bashiria Utukufu Wa Allah.” Mhadhiri huyu mahiri kutoka Kenya ambae Allah amemjaalia kuweza kuhudhuria katika Misk Ya Roho 2017 pamoja na 2018 na pia tunataraji kuwa nae mwaka huu tena In Shaa Allah katika Misk Ya Roho 2019.

Sheikh Yusuf Abdi kabla ya kuanza kuzungumzia mada yake,alitangulia kuyasema yale ambayo alifaidika nayo kutoka kwa mhadhiri mwenzake aliyemtangulia,Sheikh Ally Jumanne.Miongoni mwa hayo ni;

Waislamu tunahitajika tusome sio tu elimu ya dini bali na elimu nyingine isiyo ya dini kwa kufanya hivyo tutapata kuuona na kuuelewa zaidi ukubwa wa Allah na aliweza kuufahamu ukubwa wa Allah kupitia vilivyo angani ambavyo ni vikubwa kuliko tunavyodhani au kufikiria. Akaongezea kwa kuelezea namna gani maswahaba walikuwa ni watiifu na hatuna haki sisi leo hii kuwadharau kwa sababu wao waliamini kwa ishara na maneno ya Mtume tu bila kuyashuhudia au kuyaona kama tuonayo leo sisi katika sayansi na teknolojia.

Akaanza kubashiria utukufu wake Allah kwa kusema “Mwenyezi Mungu ametuletea dini iliyokuwa nzuri na uzuri wa dini hii inaenda sambasamba na maumbile ya mwanadamu.” Allah aliyesifika ni mzuri na uzuri wake umedhihirika katika dini yake kamwe Allah hawezi kutuamrisha yale tusiyoyaweza kuyafanya na hawezi kutukataza mambo ambayo hatuwezi kuyaacha. Chukulia mfano,laiti kama Mwenyezi Mungu angesema hatuna ruhusa ya kuoa Je ingelikuwa ni dini ya aina gani hii?

Allah anasema katika Qur’an (3:14) “Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema.”

Inaposomwa aya hii, watu hudhani Allah amekusudia kuiponda dunia na wengi wameelewa hivyo na hilo hutokana na namna mashekhe wanavyoelezea maneno haya ya Allah, wakati hivyo sivyo Mwenyezi Mungu alivyomaanisha. Akaongeza kuwa Mwenyezi Mungu katika aya hii ameelezea maumbile ya mwanadamu kama alivyoumbwa , sio makatazo na wala Allah hajaiponda dunia ila mwishoni mwa aya hiyo akaeleza ubora wa maisha ya akhera kuliko ya duniani ambayo ni yenye kudumu kwa kusema hivyo wala hakuwa na maana kuwa duniani ni pabaya bali alitilia mkazo kwamba maisha ya akhera ndio yaliyo bora zaidi.

Allah hajasema dunia ni mbaya bali baadhi ya yale yanayofanyika duniani ni mabaya na miongoni mwa hayo ni matamanio yanayofanywa na watu na yanayoenda kinyume na dini (pamoja na mafundisho ya Mtume). Allah katuletea dini yenye kufanana na fitra (asili) ya mwanadamu kwa maana ya kuwa pale unapofikwa na msiba una haki ya kulia na kuhuzunika, ukipata jambo lenye kufurahisha basi cheka haiwezekani mtu akafiwa halafu aanze kucheka kwamba kapatwa na msiba au watu wawe harusini halafu mtu akatoe mawaidha kuhusu umauti. Kuonyesha kama Allah hatukatazi jambo wala hatuamrishi kitu isipokuwa ni lililokuwa katika uwezo wetu na lenye faida kwetu.

Kusisitiza hilo Allah amesema katika Qur’an (30:30) “Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa Lakini watu wengi hawajui.”

Aya hii inathibitisha kwa namna gani dini hii ilivyokuwa sawa na maumbile ya binadamu na ndiyo iliyokuwa sahihi. Sheikh akatubashiria tena utukufu wa Allah,kwa kusema kuwa Allah ametuletea dini iliyokuwa nyepesi kutokana na sisi tulivyoumbwa. Na Allah amefanya hivyo kwa sababu anajua mwanadamu ni kiumbe dhaifu.

Sheikh Yusuf akasema kuwa tunastareheka tunavyoishi duniani na tutastareheka tunapokufa na huo ndio Uislamu. Akasisitiza kuwa Allah ametupa majina na utambulisho wetu kuwa ni “Waislamu”, tusijipe tabu ya kujiongezea majina mengine badala ya hilo. Allah amefanya wepesi katika kila kitu mpaka katika uumbaji du’a baina yake na mja wake yoyote atakayemuomba (wala hakusema walioamini).

Katika Qur’an(3:186),Allah amesema; “Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu,Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.”

Akaendelea kutusihi kushikamana na dini na kitabu tunachotakiwa kukifuata na akaonyesha umuhimu wa kufanya hivyo kwa kusema,atakayeshikamana na kuifuata Qur’an basi ataishi maisha ya raha kwa sababu kitamuongoza ipasavyo.

Katika kitabu kitukufu, mwanzoni mwa  Surah Twaha Allah anasema “Hatukukuteremshia Qur’ani ili upate mashaka. Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.”

Hivyo basi,tuwe karibu na dini pamoja na kitabu cha Allah ili tuweze kuwaidhika na kunufaika nacho.

Akamalizia kwa kutupa bishara kwa kutumbukusha kuwa Allah anawapenda wenye kufanya ihsani, Allah anawapenda wenye kumcha Mungu na Allah anawapenda wenye kutubia na kwa kusema maneno hayo akatuasa kutubia kwa Allah kadri uwezavyo na wala usiache kufanya hivyo kila utakapokosea kwa sababu hakuna aliyewahi kutubia kisha akawa malaika. Usikate tamaa na msamaha wa Allah hata kama ulikuwa unamuasi kwa miaka mingi tubu kwake kwa sababu yeye (Allah) anapenda kusamehe na huwapenda wenye kutubu na anafurahi mtu anapotubu kwa sababu anajua ya kuwa mtu amekubali makosa yake na amejua pamoja na kuamini katika msamaha wa Allah ndio maana amekiri kukosa kwake na akatubia.

Kwa haya na mengineyo mengi usikose kuwa nasi tena katika makala hii wiki ijayo In Shaa Allah

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close