1. Tujikumbushe

Kumbukizi ya Misk ya Roho 2018

Kumpenda Allah na kuwapenda waja wake…

Sheikh Ally Kajura ni mzaliwa wa Rwanda. Yeye ana uzoefu wa kazi wa zaidi ya miaka minane, mingi kati ya hiyo ni katika kuutumikia Umma wa Kiislamu na iliyobakia ni kwa ajili ya maendeleo ya jamii na mazingira. Ana Shahada ya Uzamili ya Sharia kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu Madina, Saudi Arabia.

Yeye pia ni Rais wa Tume ya Mambo ya Nje na Diplomasia nchini Rwanda katika Jumuiya ya Kiislamu (RMC). Kadhalika, Sheikh ni mtaalamu wa programu za kompyuta na amefanya kazi kama Meneja wa Tovuti ya Kiislamu na pia alipata kuwa Mtendaji wa Matangazo ya Redio ya Sauti ya Afrika (VOA).

Shukrani za dhati na sifa zote njema zinamstahiki Allah kwa kututunuku nafasi adhimu ya kukutana kwa mara nyingine. Endelea kuwa nami katika safu hii ili tuweze kuyapitia kwa ufupi yale yaliyozungumzwa na Sheikh Ally Kajura chini ya mada isemayo ‘Kumpenda Allah na kuwapenda waja Wake.”

Sheikh Ally Kajura alianza utangulizi wa mada yake kwa kumshukuru pamoja na kumpwekesha Allah Azza Wajallah na kumtakia rehema na amani kipenzi chetu Mtume Muhammad.

Kabla ya kuanza rasmi muhadhara wake, alitufikishia salamu kutoka kwa Waislamu wenzetu waliopo Rwanda kisha akawashukuru wahadhiri waliotangulia kuzungumza kabla yake kwa kutoa mafundisho mazuri ambayo yanatuwekea mkazo tuzidi kumjua na kumpenda Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wake, Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Akaendelea kusema, kumuamini Mwenyezi Mungu ni wajibu na lazima. Muislamu Muaminifu lazima ampende Mwenyezi Mungu na ampende Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kabla ya kupenda vitu vingine vyote.

Akayasindikiza maneno yake kwa aya ya Qur’an [9:24]. Katika Sura At -Tawba Allah Aliyetukuka anasema: “Sema, ikiwa baba zenu, na wanenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyoyachuma, na biashara mnazoogopa kuharibika, na majumba mnayoyapenda ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihad katika Njia yake; basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.”

Allah anatuambia katika aya hii, ikiwa tutavipa nafasi zaidi vitu vingine kabla yake yeye (Allah), basi itakuwa hatujamuamini kikweli Mwenyezi Mungu na tuingojee adhabu yake kwa kutofanya hivyo (kutomuamini kwa yakini).

Sheikh alisema kuwa, watu wa kwanza kabisa waliompenda Allah na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kuliko vitu vyote walikuwa ni Maswahaba wa Mtume. Hao ndiyo walionesha kumpenda Allah kuliko vitu vyote ambavyo Allah amevitaja katika Sura At-tawba.

Sheikh akamtolea mfano Swahaba Sa’ad bin Abi Waqqas (Allah amridhie) ambaye ni miongoni mwa Maswahaba 10 walioukubali Uislamu na baada ya kusilimu alipata mtihani mkubwa sana katika familia yake na kujaribiwa sana na mtu wake wa karibu. Mtu huyo si mwingine bali ni mama yake.

Mama wa huyu swahaba alimpa mtihani mwanae (Sa’ad) kwa kumwambia kwamba, amesikia miongoni mwa mafunzo aliyokuwa akitoa Mtume ni kuwaambia watu wawaheshimu wazazi wao. Sa’ad akaitikia: “Ndiyo ni kweli Uislamu unatufundisha kuheshimu wazazi wetu.” Mama yake akasema tena: “Mimi mbele yako ni mzazi, mama yako ambaye nilikuzaa na ninakuamrisha uniheshimu kama mama yako kwa kumkufuru Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) na pia utoke katika hiyo dini ya Uislamu ambayo umeingia.”

Ona namna Maswahaba walivyokuwa na mapenzi ya dhati na Allah na Mtume wake. Sa’ad akamjibu mama yake: “Ewe mama yangu, haiwezekani mimi kumkataa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) wala kutoka katika hii dini ya Uislamu niliyoingia. Nimeshamjua Allah ‘Azza Wajalla na Mtume wake.”

Mama yake akaendelea kumlazimisha afuate amri yake na Sa’ad aliendelea kukataa.

Ndipo mama wa Swahaba Sa’ad akatafuta namna ambayo mtoto wake akisikia atapata hofu na ataacha Uislamu. Njia hiyo ni kuacha kula na kunywa kwa sababu alidhani mwanawe akijua, atamuonea huruma na atatii amri yake.

Hata hivyo, pamoja na Sa’ad kusikia kwamba mama yake amegoma kula na kunywa aliendelea kuufuata Uislamu mpaka watu wakamfuata Sa’ad na kumtaka akamuone mama yake kwani anakaribia kufa.

Sa’ad akafika kwa mama yake na kumkuta amelala hoi na amekataa kabisa kula mpaka mwanawe atoke kwenye Uislamu na amkufuru Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Alipofika pale, Sa’ad alimwangalia mama yake kwa muda wa zaidi ya dakika tano na watu walikuwa wakimwangalia yeye na wakahisi kuwa ameanza kumuonea huruma mama yake na ataenda kuikana dini ya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Hakika hiki ni kisa kigumu kinachoonesha mapenzi kwa Mwenyezi Mungu na dini yake.

Sa’ad akamsogelea mama yake, wakaangaliana, kisha akamwambia mama yake huku akipandisha sauti ili apate kusikika. Alisema: “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ‘Azza Wajalla. Ewe mama yangu, laiti Allah angekupa nafsi 100, kisha nafsi moja ikaanza kutoka baada ya nyingine mpaka zikafikia nafsi 100, siwezi kuacha dini hii ya ‘Laa ilaaha illa Llaa Muhammad rasulullah’. Ukikataa kula au kunywa mimi siwezi kukataa ‘La ilaaha illa Llah, Muhammad Rasulullah’.

Baada ya kusikia maneno hayo, na alipogundua Uislamu ulimuingia sana mwanawe, mama yake Swahaba huyu mtukufu akaomba apelekewe chakula na maji.

Sa’ad alipotoka, mama yake alimuendea Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) na kabla hajasema lolote, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akamuuliza Sa’ad: “Ni jambo gani umemfanyia mama yako, kitendo ambacho kimesababisha Allah ateremshe aya ya Qur’an ambayo itasomwa mpaka siku ya Kiyama.”

Kumbe Allah aliteremsha aya kwa ajili ya Sa’ad kwa kitu ambacho amekifanya na kumunga mkono. Limedhirika hilo katika Qur’an [29:8], inasema: “Na tumemuusia mwanadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu Mimi ndiyo marejeo yenu, na nitakwambieni mliyokuwa mkiyatenda.”

Sheikh Ally Kajura aliendeleza mada yake kwa kumtolea mfano Swahaba mwingine mahiri, Abubakr Siddiq (Allah amridhie) ambaye alionyesha mapenzi yake kwa Allah kwa kuwashinda Maswahaba wenzake katika kutoa sadaka kila alichonacho kwa ajili ya Allah na kukitumia ili kuipigania dini ya Uislamu.

Katika kumpenda Allah, Maswahaba Abubakr na Umar walikuwa wakishindana katika kutoa mali zao katika njia ya Allah, mpaka siku moja Umar alipanga kumpita Abubakr na akaja na nusu ya mali yake.

Mtume alimuuliza: “Ewe Umar, umebakisha nini kwa watu wa nyumbani kwako?” Umar akajibu: “Nimebakisha mithili ya mali niliyoleta.”

Kisha akaja Abubakr na kutoa kila alichomiliki. Mtume akamwambia: “Abubakr umewaachia nini watu wa nyumbani kwako?” Abubakr akasema “Nimewaachia Allah na Mtume wake.” Baada ya maneno hayo, Umar akasema: “Sitashindana nawe tena Abubakar.”

Haya ndiyo mapenzi waliyokuwa nayo Maswahaba kwa Allah na Mtume wake.

Sheikh akarudia tena kusisitiza kuwa, Waislamu tumpende Mwenyezi Mungu Azza Wajallah kwa sababu tukimpenda na tukimpenda Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie) basi tutapata furaha na mema yote hapa duniani na kadhalika siku ya Kiyama.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close