1. Tujikumbushe

Kumbukizi ya Misk ya Roho 2018

Furaha ya kweli inapatikana kwa Allah…

Wasifu wa Sheikh Jamaldeen Osman Sheikh Jamaldeen Osman kutoka Mombasa Kenya ni mhitimu wa Kitivo cha Hadithi kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madina nchini Saudi Arabia. Kwasasa, yeye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha RAF (RIU) Mombasa Kenya na ni Imam na khatibu katika misikiti tofauti nchini Kenya.

Utangulizi:

Natanguliza shukrani zangu za dhati kwa Allah, Muumba wa mbingu, ardhi na vyote vilivyomo.

Leo katika safu hii, tunakuletea kumbukizi ya mhadhiri mwingine aliyekuwepo katika kongamano la Afrika ya Mashariki, Misk ya Roho mwaka 2018, Sheikh Jamaldeen Osman aliyewasilisha mada iliyoitwa, ‘Furaha ya kweli inapatikana kwa Allah tu.’

Jumuika nami ili tuweze kuupitia muhadhara huu kwa kudondoa nukta muhimu walau kwa muhtasari.

Sheikh alianza kwa kumshukuru Allah Ta’ala, Mfalme wa haki, kisha akahadithia kisa cha mmoja kati ya waja wema maarufu, Fudhail bin Iyaadh. Fudhail ni mmoja wa wema waliotangulia wakubwa wanaoheshimika katika Uislamu,
lakini hata baada ya kusilimu alikuwa ni mwizi mkubwa na alisifika kwa ukabaji.

Siku moja usiku, akiwa njiani kwenda kukutana na mwanamke mjakazi ambaye si halali yake, Fudhail akawasikia wasafiri wapita njia wakishindana, ni njia ipi wapite huku mmoja wao akiwatahadharisha kuhusu wizi wa Fudhail. Hata hivyo, siku hiyo, Fudhail hakuwa na lengo la kuiba, hivyo alihuzunika sana.

Akaendelea na safari, kisha akasikia kijana mmoja akisoma aya ya Qur’an [57:16]: “Je! Wakati haujafika bado kwa walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka?… Aliposikia aya hii, akanyoosha mkono akasema: “Ewe Mola wangu! Wakati umefika wa mimi kubadilika.” Akakariri mara tatu maneno hayo. Baada ya tukio hilo, Fudhail alihama mji na akawa mja mwema aliyependwa na watu.

Tukio hili linaonesha kuwa, mtu akipanga kurejea kwa Mola wake, basi Allah humfanyia wepesi katika hilo.

Kisha baada ya kisa hicho, Sheikh alianza kuwasilisha maudhui yake kwa kuelezea vitu viwili alivyoumbwa navyo binadamu na vilivyoletwa kwa pamoja ambavyo ni mwili na roho. Vitu hivi viwili, ni vitu ambavyo vinasababisha watu watofautiane katika namna zao za kutafuta furaha katika maisha yao.

Wengi wetu huona tutapata raha na furaha tukiwa na mali nyingi au huhisi tutapata furaha tukiwa na vyeo au baadhi hudhani kupata ujuzi na kuwa na elimu sana ndio kutawapa furaha, huku wakimpa mgongo Mwenyezi Mungu.

Sheikh Jamaldeen alisema kwamba, kutofautiana juu ya namna ya kutafuta furaha maishani mwao, hupelekea kila mmoja kutafuta njia itakayompa furaha bila kujali kama anamuasi Allah Ta’ala. Mfano, wale wanaotafuta furaha kwa kutumia mihadarati na madawa ya kulevya, wanasahau kuwa kama kwa kufanya hivyo anamuudhi Allah, basi hiyo neema itakuja kuwa balaa kwao.

Mfano utafiti unaonyesha nchi inayoongoza kwa watu kujitoa nafsi zao ni Sweden ingawa wana maisha mazuri. Tatizo ni kuwa hawajatafuta furaha ya kweli inayopatikana kwa Allah, nayo hiyo ni hasara kubwa.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an, [20:124-126]: “Natakayejiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu. Aseme, ‘Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona?’ (Mwenyezi Mungu) atasema: ‘Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa.’”

Sheikh akamnukuu Sheikh Ibn Taimiya (Allah amridhie) akisema: “Yule ambaye atakayetanguliza chochote kingine na kumpa Mwenyezi Mungu mgongo, Allah atamshughulisha nalo jambo hilo alilolitanguliza badala yake (Allah). Na Allah atafanya hicho alichokipa kipaumbele kiwe chanzo cha yeye kupata dhiki.”

Kisha Sheikh akatuasa tusiwafuate na wala tusidanganyike na wale ambao wameamua kumpiga vita Mwenyezi Mungu na waloamua kuishi maisha ya maasi (maovu).

Licha ya kuwa na dhiki, mtu atakayeyapa mgongo mafundisho ya Allah, pia Allah atamuacha. Ijulikane kuwa, Mwenyezi Mungu akishaacha kukulinda basi shetani atakutawala.

Allah anasema katika Kitabu Kitukufu, Qur’an [43:36-38]: “Anayefanyia upofu maneno Ar -Rahman tunamwekea shetani kuwa ndiye rafiki yake. Na hakika wao (mashetani), wanawazuilia njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka. Hata atakapotujia atasema, ‘Laiti ungelikuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya Mashariki na Magharibi rafiki muovu mno wewe!’”

Wanasema wanazuoni, yoyote atakayedhani hapa duniani atapata furaha kwa kumuasi Allah Aliyetukuka, basi amemdhani Mwenyezi Mungu kwa ubaya. Hii ni kwa sababu, Allah amejaalia furaha halisi kuwa katika kumtii yeye tu, kwa ushahidi wa Qur’an [16:97]: “Mwenye kutenda mema mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini tutamhuisha maisha mema…”

Mwanadamu atapata furaha katika kumtaja Mwenyezi Mungu. Allah anasema katika Qur’an [13:28]: “Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi
Mungu ndio nyoyo hutua.” Pia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Ukiitaka furaha ndani ya nyumba yako soma Qur’an. Katika Qur’an ukiisoma Surat al-Baqara peke yake utapata furaha, utapata baraka ndani ya nyumba. Na atakayeacha kusoma Surat al-Baqara atapata majuto. Na hawawezi wale wanaofanya uganga na uchawi na uhasidi kuikaribia nyumba inayosomwa ndani yake Surat al-Baqara.”

Hivyo basi, pale ambapo mtu atahisi dhiki kwenye nafsi yake, basi amtaje Allah na aisome Qur’an. Hakika maisha ya raha na yenye furaha huja kwa kumkumbuka na kumtaja Allah, kutekeleza maamrisho yake, kuachanna aliyoyakataza na kumshukuru kwa neema alizotujaalia.

Swali ni Je, Muumini anapokuwa ni mwenye kumfuata Mwenyezi Mungu hatokuwa ni mwenye kupata mitihani? Kwa hakika, mja huyu Muumini atapata mitihani kama alivyosema Allah katika Qur’an [29:1-3]: “Alif Laam Miim. Je wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema tumeamini nao wasijaribiwe? Hakika tuliwajaribu waliokuwa kabla yao na kwa hakika Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wakweli na atawatambulisha walio waongo.” Hivyo, hata walioamini nao watapewa mitihani, lakini watakaofaulu mitihani hii ni wale wenye subira na wanashukuru kisha wakasimama katika njia iliyo sawa. Allah ametubainishia hali yetu itakavyokuwa pale tutaposhikamana naye kuwa tutakuwa na maisha mazuri na misiba itakapotukuta tutakuwa na subra.

Hata hivyo, tutapata mafanikio haya endapo tu tutashikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka tutaacha makatazo yake, tutamshukuru kwa neema zake na tutamuomba msamaha kwa makosa yetu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close