1. Tujikumbushe

Kumbukizi ya Misk ya Roho 2018

Allah ni Alhakim…

Wasifu wa Sheikh Dourmohamed Issa

Ni mzaliwa na mkazi wa mkoani Mbeya, Tanzania. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Rujewa, Elimu ya sekondari katika shule ya Azania, aliwahi kusoma kituo cha kiislam cha Kimisri Chang’ombe na baadae akapata shahada ya sharia ya Kiislamu katika Chuo kikuu cha Kiislamu Madina, nchini Saudi Arabia. Ni Mwenyekiti wa taasisi ya Dhi Nureyn Islamic Foundation mkoa wa Mbeya, ni meneja wa shule ya awali na msingi ya Ummu Salama na ni mjumbe wa bodi ya wadhamini TBC.

Tunamshukuru Allah kwa kutukutanisha tena katika safu hii leo tukiwa buheri wa afya na siha njema.

Ni furaha yangu leo katika safu hii kuwaletea kumbukumbu ya muhadhara, uliohudhurishwa kwenu na mhadhiri mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 35 katika daawah kutoka nchini Tanzania Sheikh Dourmohamed Issakatika kongamano la pili la Afrika Mashariki lijulikanalo kama Misk ya Roho 2018.

Ambatana nami katika kudurusu walau kwa uchache maudhui aliyohudhurisha kwa anuani iliyokwenda kwa jina la “Allah ni Alhakim”.

Sheikh Dourmohamed alianza muhadhara kwa kujikinga na Shetani muovu kwa jina Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu, ni yeye pekee mwenye kuhimidiwa na kutegemewa.

Sheikh alianza kwa kusoma aya katika Quran (7:180) “Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo, na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake. Hao watakuja lipwa waliyokuwa wakiyatenda.” Na akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika hadithi iliyopokewa na Bukhari a Muslim “Hakika Allah ana majina 99, mwenye kuyafanyia kazi basi ataingia peponi.”

Ili kumtofautisha Allah na mahakim wengine wa duniani tunatakiwa kujua maana ya jina hili Alhakiim ijapokuwa tafsiri ya majina ya Allah anaijua yeye. Hakim ni yule ambaye anaweka mambo yake sawasawa na kila jambo analiweka mahali panapotakiwa, haamrishi ila mema, na anapoamrisha mema basi ndani yake kuna kheri na akikataza maovu pia ndani yake kuna kheri na anakuepusheni na shari za jambo hilo. Hakim hamuadhibu ila yule anaepaswa kuadhibiwa na pia aakadiria mambo yake yote kwa hekima na malengo maalum. Yeyote atakaefikiria kuwa Allah anafanya mambo yake shaghala baghala basi atakuwa amepotea upotovu mkubwa.

Kila jina la Allah limeambatana na sifa yake, sifa ya jina la Alhakiim ni Hikma, yaani Allah subhanahu wataala anasifika kwa ukamilifu na utimilifu wa Hikma. Kutokana na hilo tunatambua kuwa Allah hakuviumba viumbe bure bure tu, ila ameviumba kwa Hikma maalum ndio maana akaamrisha mambo, akayakataza baadhi, akawafungulia milango ya toba na akaweka adhabu kwa watakaokengeuka, hivyo kila jambo analiendesha kwa Hikma. 

Allah anasema katika Quran (23:115-116) “Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A’rshi Tukufu” Hapa Allah anasema katuleta kwa lengo maalum, na lengo hili amelieleza katika Quran (51:56) “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.”  Hikma ya kuumbwa kwetu ni kumuabudu Allah pekee bila ya mshirika, ndio maana dhambi ya shirki inakuwa kubwa kwa sababu mtu anakuwa amefanya uadui mkubwa kwa aliyekuumba na umevunja Hikma ya kukuleta hapa duniani.

Neno Hakim katika Quran limetajwa zaidi ya mara 90, na mara nyingi kaliambanisha na neno Aziz, Aliim na neno Khabiir kwa Hekima maalum. Allah anasema katika Quran (8:10) “…Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na Mwenye hikima.” Kuambatanishwa neno Al-Aziiz na Al-Hakiim hapa maana yake Allah hatumii nguvu zake ila kwa Hekima.  

Allah anasema katika Quran (6:83) “…Tunamnyanyua kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi.” Hapa Allah anamaanisha kuwa pamoja na kuwa Allah ana ujuzi lakini pia anatumia Hekima katika elimu yake. Na Allah anasema katika Quran (6:18) “Na ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari zote.”  Pamoja na kuwa Allah ana nguvu zote, na anajua khabari zetu zote lakini bado anatulea kwa Hekima zake.

 Allah amekadiria mambo yake yote kwa Hekima, aidha liwe jambo la kheri au la shari kwa kuwa Hekima yake Allah imekamilika kama alivyosema katika Quran (54:5) “Hikima kaamili, lakini maonyo hayafai kitu.” Kuonesha kuwa hikima ya Allah imekamilika, hata alivyoumba uhai na umauti, alikuwa na Hekima lengo lake atupe mtihani afahamu ni nani mwenye matendo mema kama alivyosema katika Quran (67:2).

Allah ameumba vitu vingi hapa duniani, lakini hizi tuzitumie kama nyenzo za kutuwezesha kufikia lengo kuu na Hekima ya kuumbwa kwao ambalo ni kumcha Allah Subhanahu Wataala. Allah anasema katika Quran (30:27) “Na yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyingine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.”

Allah hakutuumbia usiku kuwa ni milele kwa Hekima maalum kama alivyosema katika Quran (28:71) “Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu angeliufanya usiku umekukalieni moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mweyezi Mungu atakayekuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii?”  na akasema tena katika Quran (28:72) “Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu angeliufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mweyezi Mungu atakayekuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?” Hekima ya Allah kuumba usiku na mchana ni kama alivyoeleza katika Quran (28:73) “Na ni katika rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kumshukuru.”

Katika Hekima za Allah ni Qadar, ili kuzungumzia Hekima ya Qadar ya Allah ni lazima kwanza mtu aweze kuamini Qadar, na kwa mujibu wa Quran na Sunnah wanachuoni wameigawanya Qadar katika makundi manne Al-Ilm (Elimu ya Allah), na Alkitaaba (Kitaabatul Qadar), na Mashiiatu Llahi (Kuamini matakwa ya Allah) na kuamini Maqaadir bil-Khalq.

Katika Qadar jambo la kwanza ni kumuamini Allah katika elimu yake iliyotangulia, anajua kilichokuwa, kitakachokuwa, vipi kitakuwa, namna gani kitakuwa na lini na wapi kitakuwa kama alivyosema katika Quran (33:40) “…Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu” Tunatakiwa kuamini kuwa elimu tuliyonayo sisi imetanguliwa na eimu ya Allah na tumepata elimu baada ya kuzaliwa kama alivyosema katika Quran (16:78) “Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru”

Jambo la pili katika Qadar lazima uamini kwamba Allah ameandika mambo yake katika kitabu cha Qadar, na hii ni nguzo miongoni mwa nguzo za Imaan. Allah anasema katika Quran (22:70) “Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo kitabuni, Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi”

Jambo la tatu kuamini mapendekezo au matakwa yake Allah Subhanahu Wataala namna gani anavyoyapitisha mambo yake. Yeye Allah huamua katika mambo yote ya ulimwengu na sisi hatutakiwi kuhoji juu ya uamuzi wake ila yeye anaweza kutuuliza sisi.

Jambo la nne ni kuamini Qadar zake katika uumbaji, na kwamba Allah ndiye muumbaji, hakuna muumbaji asiyekuwa Yeye kama alivyosema katika Quran (39:62) “Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu” na Allah akasema tena katika Quran (54:49) “Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo”

Katika kuzungumzia Qadar mara zote watu waliopotea na wavivu kufanya ibada huchukulia Qadar kama hoja kwao, Allah anasema katika Quran (35:8) “…Hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye…” Maulamaa wanasema tafsiri ya aya hii ni kuwa Allah humpoteza anayetaka kupotea na humuongoza anayetaka kuongozwa kwa Ushahidi wa baadhi ya aya katika Quran kama vile Quran (13:27) “…Hakika Mwenyezi Mungu humwacha kupotea amtakaye, na humwongoa anaye elekea kwake” na akasema katika aya nyingine, Quran (42:13) “…Na humuongoa kwake aelekeaye”  Na katika hadithi Al-Quds iliyothibiti kupitia kwa Abu Dharr, mtume anasema: “Amesema Allah Enyi waja wangu, hakika mimi nimeiharamisha dhulma katika nafsi yang una nimeifanya kwenu kuwa haramu basi msidhulumiane. Enyi waja wangu, nyinyi nyote ni wapotevu isipokuwa yule ambaye nitamuongoza, basi takeni uongofu kwangu nitakuongozeni”

Miongoni mw Fida za kuamini Qadar ni kuwa mja anapopatwa na matatizo au shida moyo wake hutulizana na kuamini kuwa jambo hilo limetoka kwa Allah, na pia anapopata neema kutoka Allah huwa anaamini neema hiyo imetoka Allah na siku yoyote inaweza kuondoka hivyo haimfanyi yeye kupata kibri kutokana na neema hiyo. Na muumini anapopatwa na jambo lolote liwe la kheri au shari anatakiwa kusema Amekadiria Allah, na alilolitaka amalifanya (Qaddara Llahu wamaa sha’a Fa’ala)

Hayo ndiyo kwa mukhtasari, yaliyoweza kuwasilishwa na Sheikh Dourmohamed Issa katika Misk ya Roho 2018 (Unaweza kutazama muhadhara huu kupitia kiungo hiki: Bonyeza Hapa ), wakati tukijiandaa kuipokea Misk ya Roho 2019 ungana nasi katika matoleo yajayo upate ufupisho wa mada zilizowasilishwa na wahadhiri wengine.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close