1. Tujikumbushe2. Deen

Ukubwa wa Allah – Kumbukizi MYR18

Kumbukizi ya Misk ya Roho 2019

Wasifu wa Sheikh Ally Jumanne

Sheikh Ally Jumanne ni msimamizi wa maadili na maudhui Imaan Media (raqaabah). Alisoma elimu ya sekondari Kisauni Mombasa, Kenya na kisha akasoma shahada katika chuo kikuu cha kiislamu cha Madina nchini Saudi Arabia. Ni sheikh aliyejikita katika kutengeneza itikadi (aqida) za watu kwa kutoa mihadhara katika redio na televisheni za kiislamu na katika vyuo vikuu.

Ni furaha yangu leo katika safu hii kuwaletea kumbukumbu ya muhadhara, uliohudhurishwa kwenu na mhadhiri kutoka mkoa wa Morogoro nchini Tanzania Sheikh Ally Jumannekatika kongamano la pili la Afrika Mashariki lijulikanalo kama Misk ya Roho 2018.

Ambatana nami katika kudurusu walau kwa uchache maudhui aliyohudhurisha kwa anuani iliyokwenda kwa jina la “Ukubwa wa Mwenyezi Mungu”.

Sheikh Ally Jumanne alianza muhadhara kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu, na kisha kumswalia kipenzi chetu mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake kisha aliwausia watu kama alivyoiusia nafsi yake kumcha Allah Ta’ala.

Katika kuzungumzia utukufu wa Allah Sheikh alianza kwa kusema katika Quran kuna idadi ya aya 6236, kati ya hizo aya 1300 zimejikita katika kumtukuza Mwenyezi Mungu, Utukufu wa Allah katika uumbaji wake, na hiyo ni njia ambayo Allah amejitambulisha kwetu kwa kuwa haonekani, hasikiki sauti yake, hauwezi kunusa harufu yake, hatuwezi kumuonja wala huwezi kumhisi kwa kumgusa, na kwa hivyo akajiita Aliyefichikana (Al-baatwin) lakini Allah yeye anaonekana (Dhwahir) na huonekana kupitia matendo yake.

 Aya nyingi katika Quran zinazozungumzia uwepo wa Allah huwa zinazungumzia kuhusu mbingu, kwa kuwa mbingu ni miongoni mwa alama kubwa sana za uwepo wa Mungu, kama alivyosema katika Quran (51:47-51) “Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo wa hakika Sisi bila ya shaka ndio wenye uwezo wa kuzitanua. Na ardhi tumeitandaza, basi watandazaji wazuri namna gani sisi! Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie. Basi kimbilieni kwa mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake, wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake”

Hivi mpaka Allah anajitambulisha kwetu sisi inamaana hatumjui?, hata mnyama huwa anamkumbuka mtu aliyemfanyia hisani. Hivi kweli sisi binadamu ambao tuna akili timamu mpaka Allah ajitambulishe katika aya 1300. Kwa mukhtasari haya ndiyo malengo ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi. Ukimtambua Allah Ta’ala hakika utamuogopa na utamcha.

Miongoni mwa mada zinazopatikana katika vyuo vikuu vya kiislamu ni Miujiza ya kielimu kupitia Quran na hadithi za Mtume rehema na amani ziwe juu yake (Al-I’jaazu Al-Ilmi fil Quran wa Sunnatu Nnabawiyya), Muujiza ni kitu kisicho cha kawaida kilicho nje ya uwezo wa kibinadamu, ambacho Allah (S.W) hukidhihirisha kupitia kwa mmoja wa mitume wake ili huo muujiza uweze kutofautisha kati ya mtume wa kweli na mtume wa uongo, na kila mtume alipewa muujiza kulingana na jambo lililobobea sana katika jamii yake.

Nabii Musa (a.s) alipewa muujiza wa fimbo ulioonekana kama uchawi ili wachawi na wana mazingaombwe wa wakati ule waweze kumtofautisha na kwa hakika waligundua ni mtume wa Allah. Na mtume Muhammad (s.a.w) ambaye ni mtume wa mwisho, akapewa miujiza ya kielimu ambayo ni Quran na hadithi, ili miujiza hii iwe endelevu kwa watu wajao kwa mujibu wa fani zote walizonazo.

Quran imezungumza takribani katika kila fani ya zama zetu, lakini ilikuwa ikizungumza kwa lugha ya ishara ili watu wa zama zake kwenye miaka ya 570 watu wangelikufuru, kwahiyo mambo ya kisayansi yakazungumzwa kwa lugha ya ishara, na leo hii wasomi walipogundua wakaoanisha na kujua kuwa ndio yale ambayo Quran iliyazungumza na hivyo ikawa alama kuwa aliyoyasema hayo hawezi kuwa binadamu ila ni Allah Subhanahu wataala.

Mmoja kati ya wasomi wa elimu hii (Al-I’jaazu Al-Ilmi fil Quran wa Sunnatu Nnabawiyya) kimataifa Dk. Muhammad Raatib Annablusiy moja kati ya Makala zake alizozungumzia masuala ya utukufu wa Allah Jalla Jalaaluhu katika uumbaji wake wa mbingu, na mbingu (Assama’a) kwa lugha ya Qur’ani ni kila kilicho juu yako ukiachilia mbingu saba yaani anga yote kwa ujumla inaitwa mbingu alitumia uslubu ufatao; alifanya tufe la ardhi ni nukta ya kuanzia akawa analinganisha tufe la ardhi na matufe mengine katika anga akaendea kuonesha matufe mengine yalivyo makubwa akionesha utukufu wa Allah (S.W).

Mfano alisema ardhi yetu ikilinganishwa na Jua, pamoja na ukubwa wake wote litaingia mara Milioni moja na laki tatu (1,300,000) lakini jua tunaliona dogo kwa kuwa lipo mbali sana Kilomita 156,000,000. Kilomita hizi binadamu anaweza kutembea kwa gari inayotembea kwa mwendokasi wa 180 Kilomita kwa saa siku zaidi ya 36,000 kufika. Jua likileta mionzi yake katika mgongo wa ardhi na mionzi ni kitu kinachokwenda spidi sana (takriban kilomita laki 3 kwa sekunde) inachukua dakika nane mpaka mionzi yake kufika katika mgongo wa ardhi.

Pamoja na ukubwa wa tufe hili lakini linaweza kuingia mara 8 likilinganishwa na nyota moja iliyotajwa katika Quran inaitwa Asshi’ra na kama Allah alivyosema katika Quran (53:49) “Na kwamba Yeye ndiye mola mlezi wa nyota ya Shi’ira”. Ashi’ira ikilinganishwa na tufe la ardhi inaweza kuingia mara Milioni 10 pamoja na ukubwa wote wa ardhi. 

Katika anga kuna nyota inaitwa Assammakil Raamih ni kubwa kuliko jua mara alfu thelathini, kwa maana hiyo ni kubwa kuliko tufe la ardhi mara Bilioni 39. Lakini nyota hii ikilinganishwa na nyota inayoitwa Baitul Jawzaa ambayo ni kubwa kuliko jua mara Milioni 274, nyota hii ikilinganishwa na dunia yetu itakuwa kubwa mara Trilioni 355.

Katika anga kuna nyota nyingine inaitwa Qalbul Aqrab ni kubwa kuliko jua mara Milioni 343, ikilinganishwa na ardhi yetu itaingia mara Trilioni 445 na Bilioni 900. Na wanasema hivi karibuni imegundulika sayari kubwa sana inaitwa Kansio ni kubwa kuliko jua mara Bilion 9 na Milioni 261, ikilinganishwa na ardhi ni kubwa mara Trilioni 12,039 Bilioni 300.

Allah anasema katika Quran (51:47) “Na mbingu tumezifanya kwa nguvu…” Na nguvu iliyotajwa na Allah ni tofauti na nguvu tunayoifikiria sisi wanadamu, yeye anakiri ukubwa wa nguvu zake. Na watu wakiutaja utukufu wa Allah na wakimsifu wanatekeleza moja katika ibada anazozipenda ana Allah, Malaika walio karibu sana na Allah walijifakhari na ibada hiyo pale walipomwambia Allah kwenye Quran (2:30) “…Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utukufu wako…”, kwa muktadha huu kumsifu na kumtukuza Allah ni ibada mpaka kubwa mpaka Malaika wakajifakharisha nayo kwa Allah.

Allah anasema katika Quran (56:75) “Basi naapa kwa maanguko ya nyota”, Dk. Muhammad Raatib anasema Allah hakuapa kwa nyota ila ameapa kwa vituo vya nyota kutokana na umbali wa nyota na masafa ya spidi ya mwanga mpaka  kufika hapa duniani basi nyota unayoina leo si kwamba inapita muda huu ila ni kuwa imeshapita siku nyingi. Lau kama ayah ii anaisoma mtaalamu wa elimu ya Falaki (Nyota) basi angesujudu hali ya kuwa amedhalilika kama tambara lenye unyevunyevu.

Ukitazama umbali wa masafa haya utashangaa ni kwa vipi Allah alimpeleka Mtume Muhammad mpaka mbingu ya saba ambako ni mbali zaidi ya umbali huu kwa sehemu tu ya usiku.

Ulamaa wanakadiria kwamba nyota hizi katika anga zipo katika system ya njia ambazo zinaitwa Galaxy (Majarrat) ambazo idadi yake ni matrilioni, na katika kila Majarra kuna matrilioni ya nyota. Dk Annablus anasema idadi iliyofikia sasa ni zaidi ya nyota Trilioni Milioni moja.

Je ni nani anayashikilia haya matufe katika anga ili yasidondoke, Allah akasema katika Quran (35:41) “Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anayezizuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizoea isipokuwa Yeye, Hakika Yeye ni mpole Mwenye kusamehe”   

Sababu kubwa ya Allah kutupigia mfano wa haya yote, ni kututaka sisi tujue ukubwa wake ili tumuabudu, kama alivyosema katika Quran (17:22) “Usimfanye Mungu  mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliyetupika”

Pia Allah anasema katika Quran (22:73) “Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapokuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa”

Quran (13:16) inasema “…Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walioumba kama alivyoumba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye Kushinda.”

Sheikh alimaliza kwa kutunasihi kuhusu umuhimu wa ibada, alisemaAllah anatutaka sisi tumuabudu, na ametuumba kwa ajili ibada, unaweza kuikimbia ibada lakini hauwezi kuyakimbia matokeo ya ibada. Mwisho alimaliza kwa kumuomba Allah atujaalie kuwa ni wenye kuyasikiliza maneno na kuyafuata yaliyo mema.

Hayo ndiyo kwa mukhtasari, yaliyoweza kuwasilishwa na Sheikh Ally Jumanne katika Misk ya Roho 2018 (Unaweza kutazama muhadhara huu kupitia kiungo hiki https://youtu.be/fNR4-a0AKZE ), wakati tukijiandaa kuipokea Misk ya Roho 2019 ungana nasi katika matoleo yajayo upate ufupisho wa mada zilizowasilishwa na wahadhiri wengine.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close