1. Tujikumbushe2. Deen

Kila Mtu Hutoa Harufu, ni Khiyari Yako Kuifanya Ya Kufurahisha Au Kukirihisha.

Kiasili, mwanadamu ni kiumbe dhaifu mwenye mapungufu mengi mno. Kwenye mwili wake kuna harufu nyingi, na aghalabu harufu hizo si nzuri. Mwanadamu hutoa jasho, harufu mdomoni na nyenginezo, na hakuna moja ipendezayo.

Lakini, mafanikio baadhi ya nyakati maishani huwafikia wale wanaopambana na udhaifu wao wa asili. Kuna udhaifu wa kusahau, na wale wapambanao na usahaulifu hufuzu. Kuna udhaifu wa kulala, na wale wapambanao na usingizi hufuzu mno.

Turudi kwenye hoja yetu ya harufu. Wale wanaoamua kwa makusudi kupambana na harufu za kukirihisha, kwa kujitia unyunyu na uturi, kujifukiza manukato na kujinadhifisha muda wote, aghalabu juhudi hizo huleta matokeo mazuri. Ndiyo, JUHUDI. Ni juhudi na si chengine. Kwa hakika unapojibidiisha na kufanya juhudi, mafanikio ni dhahiri.

وَلَّذِینَ جَاھَدُوا فِینَا لَنَھدِیَنَّھُم سُبُلَنَا
(Wale wanaofanya juhudi tutawaongoza katika njia yetu)

Kwa upande mwingine pia, kama miili yetu ya nyama itoavyo harufu, ndivyo mioyo, nafsi na roho zetu zitoavyo harufu pia. Mara nyingi, nafsi zetu hutuvutia katika mambo maovu, na maovu hunuka mno. Ni nafsi chache mno zilizorehemewa na mola zisizoshawishi uovu, na wengi si katika hizo chache.

Kama tufanyavyo juhudi kuondosha harufu ya jasho, ndivyo tutakiwavyo kupambana na harufu za nafsi na mioyo yetu zitokanazo na matendo yetu. Nidokeze nukta moja: Moyo unapojisahau, uturi wake wa kuufukiza ni Adhkaar.
Okay, tunazifahamu adhkari nyingi, lakini hakuna adhkari bora zaidi ya zile alizotufundisha Allaah mwenyewe kwa maneno yake ndani ya Qur’an, na hiko ndio KITABU CHANGU!

Lipo jambo moja na sehemu moja inayotukutanisha kwa ajili ya jambo hili. Sehemu yenye lengo la kuzifanya roho zetu zinukie. Sehemu inayolenga kutuelezea kinagaubaga kuhusu kitabu chetu, kitabu ambacho kila mmoja ana milki ya kukiita KITABU CHANGU.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close