1. Tujikumbushe

Kifo hakina umri, epuka neno ‘Nitafanya’, jiandae sasa!

Ni jambo la kushtua inapotoka habari kuwa mtu wa karibu, ndugu, rafiki au mtu mashuhuri ambaye ulishirikiana naye katika mambo kadha wa kadha amefariki ghafla.

Lakini kimsingi, hilo si jambo la ajabu kwa sababu siku zote maisha ya mwanadamu yanafuata mpango aliouweka Allah, ambao hata hivyo unakwenda tofauti na fikra na mitazamo ya baadhi ya vijana wanaodhani kuwa katika ngazi ya umri wao huo wamefika walipokuwa wanapataka.

Vijana wanahamasishana kuutumia ujana wao na wengine wanadiriki kuwabeza wale wanaojitahidi katika masuala ya ibada na kujiepusha na mambo ya kipuuzi katika ulimwengu.

Yamkini, wengi wetu tunaishi maisha ya kughafilika na kujisahau hasa katika upande wa kumtii na kumcha Allah. Tunasahau kuwa kila kukicha siku zinasonga mbele, umri unaongezeka na siku zetu za kuishi ulimwenguni zinazidi kupungua.


“Hakika mwanadamu yumo ndani ya hasara. Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana [kufuata] haki na wakausiana [kushikamana] na subira [kustahamiliana].”
[Qur’ an, 103:2–3]

Labda tumtazame huyu mtu mwenye mgongo uliopinda, nywele nyeupe, mwendo wa taratibu, hana nguvu katika utendaji wake, hata meno yake yameanza kung’oka, anasimama kwa shida, anakaa kwa mashaka, anasali na kufunga kwa tabu na hata kula kwake na kunywa pia ni kwa shida.

Umewahi kufikiria hatua aliyopitia mtu huyu? Hivi hakuwa kijana kama wewe? Aliishi maisha ya ujana na alipitia hatua mbalimbali akicheza kama wewe na kupumbazika, akidhani kuwa maisha ya ujana yatabakia hivyo, akidanganyika na nguvu za ujana akazembea katika kutekeleza wajibu wake katika kuyatengeneza maisha ya dunia na Akhera.

Baada ya ujana kumtupa mkono, hivi leo amezeeka, udhaifu wa kila namna umeuzunguka mwili wake, maradhi ya aina mbalimbali yanamwandama, sasa analilia fursa ya ujana aliyoipoteza katika mambo ya kipuuzi, na anatamani ujana ungerudi ili atumie nguvu zake katika kufanya ibada.

Maneno Matukufu ya Allah yamemthibitikia pale aliposema: “Allah ndiye aliyekuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.” [Qur’an, 54:30].

Jambo hili la kurudi ujana ni muhali kwani kila kukicha udhaifu unazidi na siku za kubaki ulimwenguni zinapungua. Huu ndiyo utaratibu wa Allah kwa viumbe wake, utaratibu ambao haubadiliki.

Matumaini ya uongo
Mara nyingi vijana wanakuwa na tamaa nyingi zikiambatana na matumaini yasiyokuwa na ukweli ndani yake. Kijana hutumai kuwa atakapofika katika umri wa utu uzima, miaka 40, atajipinda na ibada pamoja na kutubia kwa Mola wake.

Vijana husema miaka 40 ndiyo umri mzuri kwani nitakuwa nimekamilika kiakili na kimwili, nitakuwa nimeshamaliza anasa za ujana, Allah ni Mwema na Msamehavu kwa waja wake. Husema ni bora nikasubiri kidogo nimalizie mambo ya ujana kwa sababu kwa sasa ninaweza kutubia kisha baada ya muda mchache nikarejea tena katika maasi. Hii ni sehemu ya mipango na matumaini wanayojiwekea vijana kana kwamba dhamana ya umri wao ipo mikononi mwao. Wanayoyapanga si mambo ya kesho tu bali hata ya miaka kadhaa ijayo wakiwa na fikra zile zile kuwa wao bado ni vijana na wataishi umri mrefu.

Labda tuulizane ni nani mwenye dhamana kuwa atafikia umri wa miaka 30, 40 au 50? Nani mwenye dhamana ya kufika hata kesho? Nani mwenye dhamana kuwa atanyanyuka hapo alipokaa au atafika huko anakokwenda? Umauti hauna taarifa bali huja ghafla kwa kijana, mzee hata mtoto – na sisi wote ni mashahidi kwa wale wenzetu wenye umri kama wetu waliotangulia hali ya kuwa walikuwa na matumaini ya kuishi muda mrefu.

Tujifunze kwa wenzetu. Tujiulize, je waliweza kutubia kabla ya kuondoka kwao? Je katika makaburi yao wameweza kufaidika na yale waliyoyatanguliza katika maisha yao? Kule kupoteza wakati na kujishughulisha na mambo ya kipuuzi kumewanufaisha nini katika hali waliyokuwa nayo hivi sasa? Hawakuweza kuufikia umri waliokuwa wamejipangia wenyewe kwa sabubu jambo hilo halipo katika dhima ya mtu bali mtendaji wa hilo ni Allah peke yake ambaye hahitaji ushauri wa yeyote pindi anapoamua jambo.

Epuka neno, ‘Nitafanya’
Jambo lingine ambalo ni kikwazo kikubwa kwa vijana katika kubadilisha mwelekeo wa maisha yao kuwa mzuri ni kitendo cha kutochukua hatua ya mabadiliko papo kwa papo wakawa ni watu wa kusema, “Nitafanya”. Wengi wanasema nitatubu, nitasali, hawasemi nitabadilika. Kauli hii ya kusema nitafanya kadha kwa hakika ni bahari isiyokuwa na mwisho. Waliozama katika bahari hii ni wengi mno. Walikuwa wakisema, nitafanya mpaka wakajikuta wapo ndani ya makaburi.

Walipofikisha miaka 30 walisema nitatubu nikifikisha 40, walipofikia 40 wakasema ikifika 50 na kila kukicha walikuwa wakiyakaribia makaburi, hatimaye wakayaingia huku wakisema, “Nitafanya”. Kuwa na tamaa na matumaini ya kuishi muda mrefu kumewafanya wazidishe maasi na kuchelewesha toba. Zinduka. Ujana unatoweka, umauti hauchagui na uzee ni udhaifu.

Muda unaoupoteza kwa sasa ni vigumu kuudiriki baadaye. Vifo vya ghafla vitokanavyo na maradhi ya moyo, figo, mapafu, ubongo, mfumo wa upumuaji na mengineyo; kadhalika matukio ya mara kwa mara ya ajali za ndege, magari na zile za baharini na katika maziwa ni ishara kuwa maisha yetu hapa ulimwenguni ni ya mpito.

Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika mwanadamu yumo ndani ya hasara. Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana [kufuata] haki na wakausiana [kushikamana] na subira [kustahamiliana].”
[Qur’ an, 103:2–3]. Je, ndugu yangu Muislamu hutamani kuwa miongoni mwa watu watakaofaulu Siku ya Kiyama?

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close