1. Tujikumbushe

Khiyana, tabia inayodumaza umma!

A llah ‘ Azza Wajallah’anatuambia: “Enyi walioamini! Msimfanyie khiyana Allah na Mtume, wala msikhini amana zenu hali ya kuwa mnajua.” [Qur’an, 8: 27].

Pamoja na tahadhari hiyo, Waislamu wengi wamekuwa wakiwekeza nguvu kubwa katika kuinua kiwango cha maendeleo yao binafsi na kupuuza mambo muhimu ya dini.

Katika zama zetu hizi, dhana ya ukombozi wa kiuchumi na elimu ya dini imekuwa haipewi kipaumbele cha pekee na baadhi ya Waislamu. Hivyo basi, juhudi kubwa ielekezwe katika kuweka mipango madhubuti itakayowakwamua Waislamu kielimu na kiuchumi.

 Kujikwamua kiuchumi kunaafikiana na mafundisho ya Uislamu ambayo moja ya malengo yake ni kuwafanya watu waishi maisha mazuri.

Lakini ili tuwe na maisha mazuri hatuna budi kuishi kwa mujibu wa sheria, misingi, maadili na itikadi sahihi ya dini ya Kiislamu. Wakati tufikiria ni namna gani tutaweza kuishi maisha mazuri, ni lazima kuwe na mipango thabiti ya kuiinua jamii ya Kiislamu kielimu na kiuchumi.

Ukweli, uaminifu na kuamiliana na watu vizuri, ndivyo vinavyomfanya mtu apige hatua kiuchumi. Hivyo, tunapaswa kuwa wakweli na wenye imani thabiti, isiyotikisika na yenye kuzalisha mtazamo chanya. Kauli zinazoendana na matendo na mipango inayolenga kuuimarisha umma wa Kiislamu kiimani na kitabia ni katika mambo yanayochagiza mafanikio katika nyanja za kiuchumi na kielimu.

Hii ina maana kwamba kitendo hakiwezi kuwa kizuri kama mtendaji wake hajasalimika na tabia mbaya. Nafsi isipotakasika na maovu haiwezi kuacha starehe za ulimwengu na mapambo yake.

Kwa msingi huo, ni wajibu wetu kubainisha tabia zinazopelekea umma kudumaa. Uongo, dhuluma na husda ni baadhi tu ya tabia zinazowakwamisha Waislamu katika kufikia mustakbali ulio bora.

Tabia ya khiyana

Miongoni mwa tabia zinazodumaza umma na kuharibu maisha ya watu ni khiyana. Allah ameteremsha aya nyingi zinazozungumzia ubaya wa khiyana na kueleza wazi kuwa hawapendi wenye kufanya khiyana. Miongoni mwa aya hizo ni ile inayosema:

“Na ukichelea khiyana kwa watu fulani basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kufanya khiyana.” [Qur’an, 8:58].

Na katika yale yanayoonesha ubaya wa khiyana ni neno lake Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie):

“Rudisha amana kwa aliyekuaminisha na wala usimfanyie khiyana aliyekukhini.” [Sahihi Abu Daudi].

Maana halisi ya neno khiyana na sura zake

Neno khiyana katika mtazamo wa sharia ya Uislamu lina maana ya kuvunja uaminifu kwa kufanya kitendo kinachopingana na kipimo sahihi cha tabia na maadili mema, au kuvunja ahadi iliyowekwa. Neno khiyana pia lina maana ya kwenda kinyume na haki kwa kuvunja ahadi kwa siri, kuharibu kile ulichoaminiwa kwacho iwe ni mali au heshimaa. Katika maana ya jumla, khiyana ni tabia ya udanganyifu, kukosa uaminifu na kuvunja ahadi.

Aina nne za khiyana

Allah anatuambia: “Enyi mlioamini! Msimfanyie khiyana Allah na Mtume, wala msikhini amana zenu hali ya kuwa mnajua.” [Qur’an 8:27]. Na katika aya nyingine, Allah anaonya: “Wala usiwatetee wanaokhini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye na khiyana, mwenye dhambi.” [Qur’an, 4:107]

Tukizitama aya hizi mbili tunapata sampuli nne za khiyana ambazo ni, kumfanyia khiyana Allah, kumfanyia khiyana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), kukhini amana za watu na kuzifanyia khiyana nafsi zetu wenyewe.

Kumfanyia khiyana Mtume wa Allah (rehema na amani ya Allah zimshukie) ni kuacha kutekeleza amri zake, kutoacha makatazo yake, kutofuata mwenendo (Sunna) wake na kumzulia uongo.

Wajibu wa pamoja na mahsusi

Tukumbuke kuwa matendo yote ya mwanadamu ni amana nzito ambayo viumbe wengine waliikataa. Matendo ya mwanadamu yamejikita katika kufuata amri za Allah na kuacha makatazo yake. Kwa hiyo, kumkufuru Allah, kumshirikisha, kufanya jambo kwa ajili ya kutaka kusifiwa au kujionesha (ria), kutotekeleza ahadi na kupuuza maamrisho ya Allah – yote hayo ni khiyana. Na umma utaendelea kudumaa endapo utashindwa kuacha khiyana.

Khiyana kubwa

Ama khiyana kubwa zaidi ni mtu kumkhini Allah na Mtume wake. Mwenye kuwakhini wawili hao, huyo ameinyima nafsi yake haki na muongozo sahihi aliopangiwa na Allah.

Uharibifu mkubwa umetokea kwa sababu ya watu kufanya khiyana katika kila nyanja ya maisha yao. Na maana hasa ya khiyana ni mtu kufanya maasi na mambo yenye madhara duniani na Akhera.

Mtu asiyejipamba kwa tabia njema wala kunufaika kupitia akili yake, huyo ameifanyia khiyana nafsi yake. Vivyo hivyo, mtu yeyote atakayewekeza muda na nguvu kubwa katika kufanya starehe na anasa za kidunia, kutafuta mali, cheo na kufanya uharibifu, huyo amefanya khiyana.

Kufanya khiyana kwa njia yoyote ile ni katika madhambi makubwa. Lakini licha ya kuwa ni katika madhambi makubwa, bado mlango wa toba upo wazi.

“Sema, Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Allah. Hakika Allah husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 39:53].

Na imekuja katika hadith iliyopokewa na Abu Huraira (Allah amridhie) akieleza: Mtume (rehema na amani ya Allah na amani zimshukie) amesema:

“Mtu yeyote anayeleta toba kabla ya Juakuchomoza kutoka magharibi, Allah atamkubalia toba yake.” [Muslim].

Na toba ya kweli hasa ni mtu kufanya haraka kutubu, na kujuta kutenda madhambi hayo, na kuazimia kutorudia tena. Na iwapo amefanya khiyana katika haki za watu, hapo ataleta toba na kisha inabidi airudishe haki ya watu kwa wenyewe au aombe msamaha.

Imepokewa Hadith na Abu Huraira (Allah amridhie) akieleza kwamba, Mtume (rehema na amani ya Allah na amani zimshukie) amesema:

“Aliyekuwa na kitu cha dhuluma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham (Kwa maana ya Siku ya Kiyama). Ikiwa ana amali njema, basi zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe.” [Bukhari].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close