1. Tujikumbushe

Juhudi ziongezwe kudhibiti wizi mitandaoni

Kwa muda mrefu, kumekuwepo na matukio mengi ya wizi wa mitandaoni hapa nchini na kwingineko ulimwenguni, jambo linaloibua hofu kwa watumiaji wa simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki.

Ripoti ya shirika linalotoa huduma za kudhibiti programu hasidi la Kaspersky Security Network (IT Threat Evolution Quarter Two 2019) imefichua kuwa, zaidi ya visa milioni 26.6 vya matukio ya wizi kupitia mitandao viliripotiwa duniani kote katika kipindi cha takriban miezi mitatu (kuanzia Aprili hadi Juni) mwaka 2019.

Kwa hapa Tanzania, wapo walioibiwa kwa hadaa ya kuulizwa maswali na kujikuta wakitoa namba zao za siri kwa matapeli waliovaa joho la watoa huduma za mawasiliano ya simu husika na kuibiwa.

Mbali na hao, kuna wanaojifanya ndugu au jamaa wanaotuma ujumbe mfupi wa maandishi wakiomba msaada wa haraka kwa madai wapo mbali na wana dharura.

Lakini pia wapo wengine ambao wamekuwa wakijifanya wametuma ujumbe kimakosa, lakini ndani yake ukiwa na maneno ambayo kama mpokeaji asipokuwa makini, anaweza kujikuta ‘ameingizwa mjini’. Kwa sababu hiyo, tunashauri kwamba ni vema wananchi wakachukua tahadhari muhimu kabla ya kufanya aina yoyote ya muamala.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Akikujieni (mpotovu) na habari yoyote, ichunguzeni (kwanza), msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyoyatenda.” [Qur’an, 49:6].

Hivyo, isitokee hata siku moja ukatuma fedha kwa mtu hata kama mlikuwa na ahadi ya kufanya hivyo kabla ya kuwasiliana naye kwa kuzungumza na kuwa mwangalifu wakati wa kukamilisha muamala.

Lakini pia aina za ujumbe zinazotumika kutapeli zitupe funzo kwamba hakuna mafanikio katika maisha kwa njia za mkato.

Kutokana na kuendelea kuwapo kwa tatizo la wizi wa mitandaoni na kusababisha hasara ambazo zinaweza kuzuilika, tunadhani huu ni wakati sahihi wa kuunganisha nguvu za Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), kampuni za simu na wananchi mmoja mmoja ili kupambana na uhalifu wa mitandaoni.

Sanjari na hilo, tunashauri mamlaka husika zifuatilie kuongezeka kwa wimbi hili la utapeli na kuchukua hatua ama ya kutoa elimu ili wananchi wasiumizwe, lakini pia kuwabaini wahalifu na kuwachukulia hatua stahiki.

Tunaamini lengo zuri la serikali la kukabiliana na matukio ya wizi wa mitandaoni litaongezwa kasi endapo mamlaka husika zitaendelea kuchukua hatua kwa watu wanaotekeleza vitendo hivyo viovu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close