1. Tujikumbushe

Itambue misimu ya kheri na kuithamini

Hakika umekujieni mwezi wa  Ramadhan, mwezi wenye baraka. Allah amefaradhisha ndani yake funga, inafunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto, na wanafungwa mashetani, ndani yake kuna usiku bora zaidi ya miezi elfu, atakayeikosa heri hiyo basi huyo atakuwa amepoteza.” [Ahmad na Nasai].

Naam! Mwezi wa Ramadhan ni neema kubwa kutoka kwa Allah kwa sababu ndani yake kunapatikana fursa ya pekee ya kuvuna neema na baraka tele kutoka kwa Allah Mtukufu. Jambo la kutafakari na kujiuliza ni kwa kiasi gani tunafaidika kwa kheri za Ramadhan.

Yapo mambo mengi yanayopelekea Waislamu wengi kutofaidika na Ramadhan. Moja ya mambo hayo ni Waislamu kutotambua misimu ya kheri na nafasi yake katika maisha yao ya dunia na Akhera.

Allah ametuletea mwezi wa Ramadhan na ameutofautisha na miezi mingine ili waja wafaidike na neema zake. Allah ametakasika na kila kasoro na upungufu, ameumba viumbe kisha akawaamrisha baadhi ya mambo na kuwakataza mengine, na ametofautisha ubora wa siku na miezi.

Hakufanya hayo kwa mchezo bali kudhihirisha utukufu na uwezo wake kwa waja. Allah anatuambia: “Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? Ametukuka Allah, Mfalme wa Haki, hapana mola wa haki ila Yeye, Mola Mlezi wa A’rshi tukufu.” [Qur’an, 23:115– 116].

Ni muhimu Muislamu kuitambua misimu ya kheri na kujifunza hukumu za kisharia zinazofungamana na ibada zinazopatikana katika msimu husika. Si sahihi kwa Muislamu kuzungumzia au kufanya ibada asiyokuwa na elimu nayo kwani akiifanya atakosa faida ya ibada hiyo kwa sababu ya kutofuata sharia na taratibu.

Kwa hiyo, kwa kuzingatia hili, Muislamu huyu atakuwa amepoteza msimu wa kheri ambao haupatikani isipokuwa mara moja kwa mwaka.

Siku 10 za mwazo za Dhul-Hijja
Katika kila msimu, kuna ibada za kipekee ambazo hutofautiana na ibada za misimu mingine. Siku kumi za mwanzo katika mwezi wa Dhu–Hijja ni miongoni mwa misimu bora kabisa kwa Waumini kutekeleza ibada mbalimbali. Allah Mtukufu ameziapia siku hizi 10 ndani ya kitabu chake kitukufu cha Qur’an pale aliposema: “Naapa kwa Alfajiri. Na kwa siku 10.” [Qur’an, 89:1–2]. Wanazuoni wengi wa tafsiri ya Qur’an wamesema kilichoapiwa katika Aya hii ni siku 10 za mwanzo wa Dhul–Hijja, yaani Mfungo Tatu.

Siku 10 hizi zinajumuisha fadhila na baraka mbalimbali. Kutenda amali njema katika siku hizi ni bora kuliko amali njema katika siku nyingine za mwaka, kama alivyotuambia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Hakuna siku amali inakuwa bora zaidi kushinda siku hizi 10 za Dhul–Hijja (Mfungu Tatu).” Maswahaba wakasema: “Hata amali ya Jihad?” Akasema: “Hata Jihad, ila mtu aliyetoka Jihad akaiweka rehani nafsi yake na mali yake, na kurejea bila ya chochote.” [Bukhari]. Wanazuoni wameitaja Hadithi hii kama ushahidi juu ya ubora wa funga ya siku 10 za Dhul-Hijja.

Kufunga Sunna mwezi Shaaban
Vile vile, kukithirisha kufunga Sunna katika mwezi wa Shaaban ni mojawapo ya ibada muhimuambazoMuislamu hapaswi kuzipuuza. Imethibiti katika Sunna, kupitia Hadithi ya Aisha (Allah amridhie), akisema: “Sijamuona Mtume akifunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyokuwa akifunga katika Shaaban.” [Bukhari na Muslim].

Msimu wa Ramadhan
Kadhalika, katika msimu huu wa Ramadhan, Waumini wa kweli wanaojitambua hujipinda usiku na mchana ili kufikia yale yaliyoyakusudiwa ya kheri. Ndani ya Ramadhan, ipo funga ya faradhi ambayo haipatikani katika miezi mingine wowote ila huu. Katika mwezi huu, kila jema analofanya mja hulipwa maradufu kuliko ambavyo analipwa katika siku za kawaida.

Pia, ndani ya kumi la mwisho la Ramadhan kunapatikana usiku wenye heshima kubwa au cheo, yaani Laylatul Qadri. Malipo ya amali anayoifanya mja ndani ya usiku huu ni zaidi ya amali iliyofanywa katika miezi elfu (miaka 84), kama anavyobainisha Mwenyezi Mungu:

“Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu.” [Qur’an, 97:3].

Hivyo, ni vema kila Muislamu apanie kuupata usiku huu kwa kufanya ibada mbalimbali kama alivyofanya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ambapo alikuwa akikaa itikafu msikitini ili usiku huu wa cheo umkute akiwa katika ibada. Jambo bora na muhimu zaidi kwa Muislamu ni kuzitambua ibada muhimu zinazopasa kufanywa katika misimu ya kheri na kujua fadhila zake ili kupata tija na faida kutokana na ibada hizo.

Ni muhimu kufanya hivyo ili kujua ni ibada gani ipewe kipaumbele katika msimu husika. Kujua ukubwa wa malipo yanayopatikana katika ibada fulani husaidia kuipa nafsi hamasa, umakini na nguvu ya kufanya ibada. Pia, humpa mja mtendaji uchangamfu kwa sababu anajua kuna thawabu nyingi atakazozipata kupitia ibada hiyo.

Kwa mfano, wapo watu wanaotekeleza ibada za sunna na kuacha za faradhi, au kutanguliza ibada yenye ubora unaozidiwa na ibada nyingine. Katika mazingira kama haya, mtu anaweza kupoteza nguvu na muda mwingi kufanya ibada zenye daraja ya chini na kuziacha zile zenye thawabu kedekede.

Epuka mijadala ya kimadhehebu
Moja kati ya mambo yanayofanya Waislamu wengi wasinufaike na misimu ya kheri ni kupoteza muda kwenye mijadala ya kimadhehebu isiyo na tija. Ubaya ni kwamba, mijadala hii imejikita katika kuendeleza mabishano na siyo kuelimishana na kuibadilisha jamii ya Kiislamu.

Jambo muhimu hapa ni kujifunza hukumu za kisharia kutoka
kwa wanazuoni wanaoaminika na wenye nia nzuri ya kuielimisha jamii bila kuiyumbisha.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close