1. Tujikumbushe

Huenda unapata riziki kwa sababu yake

Anas bin Malik [Allah amridhie] amesema: “Kulikuwa na ndugu wawili katika zama za Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie]. Mmoja alikuwa akimwendea Mtume mara kwa mara kutafuta elimu na hekima, na mwingine akifanya kazi kwa ajili ya kumsaidia nduguye. Mmoja wao [yule mfanyakazi] akamshitaki ndugu yake kwa Mtume. Mtume akamwambia: “Huenda unapata riziki kwa sababu yake.” [Tirmidhiy].

Mafundisho ya tukio

Tukio hili, kwanza linatufunza umuhimu wa kujitolea katika mambo ya kheri hususan katika zama hizi ambazo baadhi yetu Waislamu tumekuwa tukitumia rasilimali fedha katika mambo ya haramu kama vile muziki, soka na mambo mengine ya anasa.

Tukio hili pia linatoa picha tofauti ya namna walivyoishi waja wema waliopita, ukilinganisha na maisha tunayoishi Waislamu wengi wa zama hizi

Katika ibada ambazo huchukua nafasi kubwa katika maisha ya kila ya Muislamu ni kutoa ufadhili wa masomo hususan ya dini, kusadia maskini, yatima na wale wanaojitolea kuwalingania watu Uislamu

Umuhimu wa kutafuta elimu

Kutafuta elimu ni jambo lenye manufaa kwa mtu binafsi, dini na jamii nzima na ndiyo maana Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] alibariki uamuzi wa kijana yule wa kutafuta elimu na kumuusia nduguye anayefanya kazi kumsaidia mwenzie kwa sababu anafanya jambo kubwa lenye manufaa kwa jamii.

Mtume alimfahamisha na akamtaka awe pamoja naye kwa sababu lile analolifanya ndugu yake, yaani kutafuta elimu huenda ndiyo chanzo cha yeye kupata riziki kwa wepesi. Kupitia elimu, watu hufundishwa kuchunga mipaka ya Allah, kutenganisha halali na haramu, kufanya uadilifu, kuishi kwa kuzingatia misingi na maadili ya dini, na kadhalika. Hivyo, kutafuta elimu ni jambo kubwa linalostahiki kuungwa mkono na kila mwenye kumuamini Allah na Siku ya Mwisho.

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, wapo baadhi ya ndugu zetu wanaoona uzito kutafuta elimu kwa kisingizio cha kubanwa na shughuli nyingi za utafutaji riziki.

Tumeona katika tukio hili kwamba mtu anayetafuta elimu, Allah humfanyia wepesi katika shughuli zake za kila siku. Hata hivyo, wakati tukitupiana lawama kwa kushindwa kusaidia ipasavyo sekta ya elimu, swali la kujiuliza ni; kwa kiasi gani Waislamu tunafanya jitihada binafsi au za pamoja kuwasaidia vijana wetu kielimu? Hebu kwa mfano, tujiulize mimi na wewe tunafanya nini kuhakikisha vijana wa Kiislamu wanafanya vizuri kitaaluma?

Tuwekeze katika mambo ya kheri

Moja kati ya malengo ya Uislamu ni kuilea nafsi kupenda mambo yenye manufaa kwa mtu binafsi na jamii nzima. Jambo moja la hakika ni kwamba, mja anayeshikamana na tabia njema ya kusaidia mambo yenye manufaa kwa jamii hupata daraja (malipo) kama ile anayoipata mtu anayefunga swaumu au kusimama usiku kwa ajili ya sala.

Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] amesema: “Hakika Muumini hupata kwa tabia yake njema daraja za aliyefunga na anayesimama usiku kwa ajili ya ibada.”

Kuwanufaisha wengine ni sehemu ya ibada

Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] amesema: “Mtu anayependwa zaidi kwa Allah Aliyetukuka ni yule mwenye kuwanufaisha watu, na matendo yanayopendeza sana kwa Allah ni furaha unayoiingiza kwa Muislamu au kumuondoshea tatizo, au kumlipia deni.” [Twabraniy]. Jukumu la kuilinda dini na jamii dhidi ya mmomonyoko wa maadili ni la watu wote na si mtu mmoja au kikundi fulani cha watu. Kila mmoja wetu kwa nafasi yake ana wajibu wa kulinda dini kwa kutumia elimu, mali au mamalaka aliyonayo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close