1. Tujikumbushe

Hijja Itufunze Kumcha Allah Kikamilifu

Ibada ya Hijja ilimalizika rasmi katika mji Mtakatifu wa Makka na kisha mahujaji wakaelekea mjini Madina kwa ajili ya kuzuru maeneo mbalimbali ya kihistoria ukiwemo msikiti wa Mtume [Masjid Nnabawiy]. Naam! hii ni safari muhimu inayopaswa kuendewa na kila muislamu mwenye wasaa, kwani Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] amesema:

“Isifungwe safari ndefu [kwa ajili ya ibada] isipokuwa kwenda katika Misikiti mitatu; Masjidul Haraam [Makka], na Msikiti wangu huu [Madina], na Msikiti wa Ilyaa [Baytul Maqdis-Palestina],” [Imepokewa na Bukhari, Muslim, Tirmidhi na wengineo].

Siyo lengo letu kuzungumzia ziara ya Madina bali tunataka kuonesha umuhimu na utukufu wa ibada ya Hijja na athari zake katika maisha yetu ya kila siku. Inafahamika kuwa, moja ya nidhamu aliyoiweka Mwenyezi Mungu kwa waumini ni kutekeleza ibada ya Hijja ambayo katika malengo yake ni kumuandaa mja kumpenda Allah kuliko kitu kingine chochote.

Lengo hili huifanya Hijja kuwa na umuhimu mkubwa kwa waumini wa dini ya Kiislamu. Ni uchache wa fikra kudhani eti, faida ya Hijja inaishia katika kutekeleza matendo ya kutufu na kussai(kuzunguka milima miwili ya swafa na Marwa), kusimama Arafa, kulala Muzdalifa pamoja na kupiga mawe Jamaraat. Tunasema hivyo kwa maana, Hijja ni zaidi ya kutufu, kussai na matendo mengineyo. Lakini swali la kujiuliza ni je, baada ya kumalizika Hijja, Mahujaji wanawezaje kudumu na fikra ya kuitumikia akhera kuliko dunia.

Bila shaka msingi wa swali hili unarejea katika kuifahamu dhana ya ibada ambayo ndio lengo kuu la kuwepo kwetu ulimwenguni. Si jambo la kutilia shaka kwamba, wapo wenye uelewa finyu katika kuifahamu dhana ya ibada. Hawa ni wale wanaoinasibisha ibada na matendo ya kusimamisha swala tano, kufunga Ramadhani, kutoa zaka na kwenda Hijja.

Hii ni dhana duni ambayo kamwe haiwezi kumfikisha muislamu katika lengo kusudiwa. Hivyo basi ili kulinda hadhi na ubora wetu mbele ya Mwenyezi Mungu, ni lazima tudumu katika kutekeleza ipasavyo ibada zote zilizoainishwa na dini.

Kutazama haramu ni miongoni mwa madhambi ambayo wengi wetu huyaona kuwa ni madogo mno. Hii ni dalili ya kuwepo kwa kundi kubwa la watu wanaodharau makosa wanayomfanyia Mwenyezi Mungu. Sisi Waislamu, tunalazimika kujiepusha na maovu ya utapeli, shirki, kiburi, matusi, pamoja na kula riba na mali za haramu ili kujinusuru na adhabu ya Allah Ta’ala Siku ya Kiyama.

Pia katika kuhakikisha hatupotezi wakati wetu bure, ni vema tukaacha kufuatilia mambo yanayotupelekea kupata madhambi mfano wa muziki, mpira na mengineyo. Hatuna sababu ya kuhoji ikiwa ipo faida ama laa kwa wale wanaotumia muda wao mwingi huko, lakini ni lazima tujiulize, ni kwa nini hatutengi muda wa kuisoma Qur’an japo kwa robo saa kila siku.

Tutosheke na kauli ya Allah Ta’ala isemayo :“…Hakika masikio, na macho, na moyo hivyo vyote vitaulizwa [Siku ya Kiyama].” [Qur’an, 17:36].

Lililo muhimu kwa Muislamu ni kutahadhari na kudharau makosa anayomfanyia Mwenyezi Mungu kwani kufanya hivyo ni kujifedhehesha na kujikosesha thamani mbele ya Muumba. Pia, wanazuoni wa Kiislamu wanasema:“Usitazame udogo wa dhambi bali tazama ukubwa wa Yule unayemuasi.”

Pamoja na yote hayo, bado hatujachelewa kwani kupitia nguzo ya Hijja, tunayo nafasi kubwa ya kufanya mageuzi kutoka katika Uislamu, uumini hadi UchaMungu. Wakati umefika wa kuzilazimisha nyoyo kumtumikia Muumba wetu. Na kwa kuwa tunafanya biashara na Allah Ta’ala hatuna budi kuyafanya maisha yetu kuwa bidhaa pendwa kwake. Ili tuwe watiifu mbele ya Allah Ta’ala, hatuna budi kuelekeza juhudi zetu katika kumtii kwa moyo wa ikhlaswi na ndani ya mipaka ya tabia njema, na hapo ndio tutakopata chakula cha furaha katika maisha baada ya kufa

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close