1. Tujikumbushe

Hakika sisi ni wa Allah, na kwake tutarejea

Allah Mtukufu anatuambia: “Na tutakutieni katika msukosuko wa hofu na njaa na upungufu wa mali na kufiwa na wa matunda. Na wabashirie wanaosubiri. Wale ambao ukiwasibu msiba husema, ‘Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tutarejea’. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.” [Qur’ an, 2:155-157].

Maana halisi ya Aya hiyo ni kwamba kila tulichonacho hapa duniani, kwa hakika si chetu. Vitu vyote vinavyokuzunguka, kila unachokiona, kila ulichonacho na kila kilichopo, vyote ni Miliki ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Ni Allah Ta’ala ndiye aliyekupa mali na vitu vyote unavyomiliki, na kwamba Yeye Ndiye Mmiliki wa kweli wa vitu vyote hivyo. Kwa hiyo, magari unayomiliki, nyumba unazoishi, biashara unazomiliki – vyote ni mali ya Mwenyezi Mungu. Watoto aliokujaalia, afya aliyokuneemesha na muda aliyokuachia, vyote ni mali ya Allah Ta’ala.

Hata uhai tulionao ni miliki ya Mwenyezi Mungu peke yake, kama mwenyewe anavyosema ndani ya Qur’an:

“Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye Ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo. Naye ni Muweza wa kila kitu.” [Qur’an, 5:120]. “Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu…” [Qur’an, 2:142].

 Kwa kuwa kila kitu ni miliki ya Allah Ta’ala, basi tunapaswa kuingiza hata roho zetu kwenye orodha hiyo ndefu.

Vifo vya Masheikh wakubwa na wanasiasa mashuhuri vilivyotokea hivi karibuni nchini Kenya na hapa Tanzania ni ushahidi kuwa roho zetu ambazo tunaziita nafsi ni mali ya Mwenyezi Mungu, siyo zetu.

Uislamu umefafanua kuwa mtu yeyote hawezi kufa ila kwa matakwa na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hivyo, sababu inayopelekea kifo ni moja tu, nayo ni kumalizika kwa umri wa mwanadamu. Muislamu lazima aitakidi kuwa afishaye (anayetoa uhai) si mwingine bali ni Mwenyezi Mungu pekee.

Pindi muda uliowekwa kwa ajili yetu unapokamilika, maisha hukoma kwa kupitia sababu zinazoonekana kwa nje kuwa ndio chanzo hasa. Ajabu ni kwamba kundi kubwa la watu wakiwamo Waislamu, wameigeuza dunia kuwa sehemu ya kwanza na ya mwisho ya maisha, wakiamini hakuna kitakachofuata baada ya kufa kwao.

Lakini Allah Mtukufu anasema: “Ama yule atakayekiuka amri ya Mwenyezi Mungu. Na akapendelea maisha ya dunia (kuliko ya Akhera). Hapana shaka mafikio yake ni motoni.” [Qur’an, 79:37-39].

Kwingineko, Waswahili husema: “Ponda mali kufa kwaja”. Mantiki ya msemo huu imekuwa ndiyo hoja ya watu wanaoamini kifo ni adui wa starehe hivyo kujipa fursa ya kustarehe kabla mauti hayajawafika.

Hawa ni wale ambao huzidhulumu nafsi zao kwa kujitenga mbali na suala la kumkumbuka Allah, ili hatimaye wasilazimike kuitumia neema ya uhai katika kumuabudu. Kwa sababu hii, Mwenyezi Mungu anatuonya kwa kutuambia:

“Hakika hayo mauti mnayoyakimbia bila ya shaka yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana. Hapo atakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.” [Qur’an, 62:8].

Tahadhari na kuipenda sana dunia

Kuishughulikia dunia na kuisahau Akhera ni sawa na kuijenga nyumba moja na kuharibu nyingine. Kwa msingi huo, haifai Muislamu kuipenda zaidi dunia na kuipuuza Akhera kwa kuwa hakuna awezaye kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Hii ina maana, mja hawezi kuitumikia Akhera ipasavyo na wakati huohuo akaitumikia dunia. Ama mwenye kuvitumikia vyote viwili, dunia na akhera, kwa nguvu sawa basi kuna uwezakano mkubwa wa kukichukia kimoja na kukipenda kingine.

Ikiwa unamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho basi jilazimishe kuifanyia kazi Akhera yako. Lia juu ya wasiwasi wa nafsi yako, na uwe ni mwenye hofu ya kuiogopa Siku ya Hesabu (Kiyama). Ewe Muislamu, kumbuka uhai ni amana, hivyo unapaswa kuutumia kwa uadilifu na utii wa kufuata maamrisho ya Muumba wako.

Allah ametuumba kwa lengo kubwa moja, nalo ni kumuabudu yeye pasina kumshirikisha na chochote. Hivyo, wanadamu tutambue kuwa tupo kwenye mtihani wa kutekeleza ibada za Mwenyezi Mungu ili kufikia lengo la kupata mafanikio bora Siku ya Kiyama.

Kadri mwanadamu anavyozidi kutenda wema na kutekeleza ibada za Mwenyezi Mungu, ndivyo anavyozidi kupata mafanikio kwenye mitihani ya dunia.

Tuchukue mafunzo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu wakati alipofiwa na mtoto wake, Ibrahim. Mtume alisema:

“Macho yetu yamejaa machozi, mioyo yetu imejaa huzuni, lakini hatusemi kwa midomo yetu, isipokuwa lile linalompendeza Allah. Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.” [Bukhari].

Hiyo ndiyo imani inayotakiwa kuambatana na kauli ya Mwenyezi Mungu “Inna lillaahi wa inna ilayhi Rajuun.” Hatamki maneno haya ila yule anayemuamini Allah na Siku ya mwisho.

Kwa hakika kifo kipo karibu sana, hivyo mwanadamu hana sababu ya kuchelewa kufanya matendo mema kwa nia thabiti na Ikhlas huku akitumia fursa ya uhai kufanya toba kwa Mwenyezi Mungu.

Nasema haya kwa sababu, Mwenyezi Mungu hatakubali toba inayotokana na hofu ya mauti katika dakika ya mwisho kama anavyobainisha ndani ya Qur’an:

“Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema, ‘Hakika mimi sasa nimetubia.’ Wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.” [Qur’ an, 4:18].

Kuna faida nyingi za kukikumbuka kifo, na miongoni mwa hizo ni: Mosi: Mwenye kukitafakari na kukikumbuka kifo, daima hujibidiisha kufanya matendo mema, kuepuka maovu na kuridhika na kichache. Na mwenye kukisahau kifo hughafilika na maisha ya dunia na kuvuka mipaka ya Allah kwa kufanya maasi mbalimbali.

Pili: Mwenye kukikumbuka kifo hufanya toba ya kweli kwani hukumbuka madhambi yake na kumuomba msamaha Allah kwa sababu anajua siku na muda wowote anaweza kuiaga dunia. Kwa hiyo, ni wajibu Muislamu kujiweka mbali na anasa za ulimwengu na vitu visivyokuwa na faida. Na katika sifa za waumini wa kweli ni kujiepusha na mambo machafu, maovu na yenye kutia shaka (Shubuhaat). Kwa kufanya hivyo, utaisalimisha nafsi yako na hatari ya kufanya dhambi.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close