1. Tujikumbushe

Hakika shirk ni dhuluma kubwa!

K atika maisha yake hapa duniani, mwanadamu hujikuta njia panda anapofikwa na matatizo. Kwa bahati mbaya, wapo baadhi yetu ambao hukata tamaa wakati wa matatazo na kuwaendea wachawi au waganga wa kienyeji wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi kwa lengo la kutafuta suluhu ya matatizo yao.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, tabia hii ya kuwaendea wachawi na wapiga ramli chonganishi haipo kwa watu waaminio ushirikina pekee bali hata baadhi ya Waislamu wanaotekeleza ibada ya sala. Ni Waislamu hawa ambao ndani ya sala zao husema:

“Wewe (Allah) ndiye tunayekuabudu na wewe tu ndiye tunayekutaka msaada.” [Qur’an, 1:5].

Hali hii inadhihirisha wazi upungufu na udhaifu wa imani kwa baadhi ya Waislamu katika suala zima la kumtegemea Allah. Muislamu mwenye imani ya kweli hufuata utaratibu wa kisharia katika kutafuta suluhu ya matatizo yanayomkabili.

Hii ni kwa sababu, Muumini siku zote humtumainia Allah na kumshukuru kwa kila jambo na wala hatumii njia za kishirikina kwa sababu hajui sekunde, dakika, saa, siku na wakati wa kufa kwake.

Muislamu anayeamini ufufuo na Siku ya Kiyama huwa na yakini moyoni mwake juu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu mmoja, Mwenye nguvu, Muweza wa kila kitu, asiye na mwana, msaidizi wala mshirika.

Shirk ni kinyume cha Tawhid

Shirk ni kumwekea Allah mshirika katika Uungu wake au ibada yake au sifa zake. Mshirikina ameitwa mshirika kwa sababu amemshirikisha Allah na viumbe wake katika Kuabudiwa, Ufalme na Uungu wake. Na shirk ndiyo dhambi kubwa zaidi ambayo haisamehewi ila kwa toba maalumu.

Hilo limeelezwa ndani ya Qur’an pale Allah Aliyetukuka aliposema: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi (dhambi ya) kushirikishwa. Lakini yeye (Allah) husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, basi huyo amepotea upotovu wa mbali.” [Qur’an, 4:116].

Naye Mtume (rehema za Allah amani imshukie) amesema: “Atakayekufa katika hali ya kumuomba asiyekuwa Allah ataingia motoni.” [Bukhari].

Kwa hivyo, tunapaswa kumpwekesha Allah kwa kumuabudu Yeye peke yake pasina kumshirikisha na chochote. Tumeusiwa tusimshirikishe Allah kwa sababu shirk ni dhambi inayotafuna matendo mema ya mja.

Madhara makubwa ya kumshirikisha Allah yatashuhudiwa Siku ya Kiyama pale Allah Mtukufu atakapowaambia Malaika:

“Mtupeni katika Jehannam kila kafiri muasi. Akatazaye kheri, arukaye mipaka, aliyekuwa akijipa shaka (zisizokuwa na sababu). Aliyeweka mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, basi mtupeni katika adhabu kali.” [Qur’an, 50:24– 26].

Kuwa na subira na uvumilivu

Kufanya subira si jambo jepesi. Ni jambo linalohitaji juhudi na azma ya kweli kama Qur’an inavyotuambia.

“Na anayesubiri na kusamehe (atalipwa wema wake). Bila shaka hilo ni katika mambo makubwa ya kuazimiwa kufanywa (na kila Muislamu).” [Qur’an, 42:43].

Kwa hiyo, Muislamu anatakiwa awe mwenye kusubiri baada ya kupata shida au matatizo. Na kwa kuwa matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, Allah Aliyetukuka ameandaa malipo makubwa kwa watu wafanyao subira katika matatizo.

Ni uduni wa maarifa kudhani eti matatizo yanatokana na hasira za Mwenyezi Mungu kwa viumbe. Jambo hili halina ukweli wala usahihi, kwani Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtihani mkubwa, na hakika Allah anapowapenda watu huwapa mtihani, Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allah) na atakayechukia atapata ghadhabu,” [Tirmidhiy].

Nao, baadhi ya Wema waliopita (Salaf) wamesema, lau isingelikuwa ni kwa sababu ya matatizo ya duniani, basi tungelikuwa ni wenye kufilisika Siku ya Kiyama. Kwa muktadha huu, ni wazi kama kusingekuwa na matatizo, watu wangeishi kwa majivuno, kiburi, kujiona, dhuluma na moyo msusuwavu.

Hivyo, ndugu yangu Muislamu, kuwa mwenye subra na uvumilivu na kamwe usikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Tambua matatizo yanayokusibu ni sehemu tu ya mipango [Qadar] ya Mola wako Mlezi.

Shikamana na subira kwani subira ni ukarimu usiokwisha, ulinzi usioshindwa na ngome isiyovunjika. Kumbuka subira ndiyo silaha yako ya mapambano dhidi ya mitihani ya ulimwengu. Ali bin Abi Twalib (Allah amridhie) amesema:

“Mwenye kuipa nyongo dunia, matatizo (misiba) huwa ni mepesi kwake, na mwenye kuona kifo kiko karibu basi hukimbilia kufanya matendo ya kheri.”

Hii ni kwa sababu, mja huwa mwepesi zaidi wa kusubiri pale anapoyatazama malipo makubwa ya Akhera. Kwa minajili hiyo, hatuna budi kuikabili mitihani ya Mwenyezi Mungu kwa upole na ikhlas. Mwenyezi Mungu anataka tukwee na kufikia daraja ya uchamungu, ndiyo maana anatujaribu kwa kutupitisha katika mitihani kadha wa kadha.

Vyovyote iwavyo, furaha tunayoipata hapa duniani ni yenye kufunikwa na matatizo. Ibnu Abbas (Allah amridhie) amesema:

“Kila furaha ina huzuni. Hakuna nyumba iliyojaa furaha isipokuwa hujaa huzuni.”

Kauli hii inathibitisha wazi kuwa, Muumini ndiye mlengwa mkuu wa mitihani pamoja na majaribu, na kwa ajili hiyo baadhi yao hupewa mitihani migumu huku wengine wakipewa mepesi kulingana na udogo wa imani yao.

Hii ndiyo sura halisi ya maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni. Kwa hiyo, wale wanaodhani kuwa dunia ni mahala pa starehe na kufurahia maisha wanajidanganya wao wenyewe!

Ukweli ni kwamba, dunia hii tunayoishi ni shamba la kupandia mazao ya Akhera, na bila shaka shamba hili litastawi na kumpatia mazao bora yule aliyeishi kwa kufuata taratibu na kanuni alizoweka Mwenyezi Mungu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close