1. Tujikumbushe

Fatwa ni dhamana na amana, tuwaachie wanazuoni

Kuna udhaifu mkubwa wa uelewa miongoni mwa Waislamu katika mambo ya kisheria. Ipo mifano mingi ya watu wanaotoa majibu mepesi katika hoja nzito na maswali ya msingi wanayoulizwa na watu kwenye mitaa wanayoishi kuhusu hukumu mbalimbali za Uislamu.

Hali hii imepelekea kujitokeza kwa kada ya watu wanaotanguliza akili na rai zao katika kutoa ufafanuzi (fatwa) katika masuala ya kidini. Mtindo huu umeibuliwa na makundi ya vijana ambao kwa hakika uwezo wao kielimu ni mdogo.

Hili ni jambo zito na kubwa ambalo nimekuwa nikijiuliza mara kwa mara hasa ninapofanya tafakuri ya kina juu ya masuala yanayojitokeza katika dini yetu na jamii kwa ujumla.

Mtindo huu wa kutoa majibu mepesi au ya jumla jumla unaweza kuwa hatari katika dini na jamii kuliko kitu kingine chochote. Huu ni ugonjwa ambao unaweza kuwa umejificha au unaonekana waziwazi lakini kwa tabia yetu sisi Waislamu tunaupuuza na kujipa moyo kuwa Uislamu ni mwepesi. Jambo hili likipuuzwa linaweza kuwa na madhara makubwa hasa katika suala la utoaji haki.

Wasichokijua watu wengi ni kuwa, kutoa fatwa ni dhamana na ni amana, hivyo haijuzu kwa yeyote kutoa ufafanuzi wa masuala ya kidini ila kwa yule aliyefikia daraja ya kutoa fatwa kwa ujuzi na elimu aliyopewa na Allah ‘Azza Wajallah’.

Katika kitabu chake alichokiita; ‘I’laamul – muwaqqiiyn An Rabbil Aalamiyn’, Imam Ibn Qayyim (Allah amrehemu) amesema: “Wale wenye kutoa fatwa wanaandika kwa niaba ya Allah. Fatwa sio jambo rahisi. Hatoi fatwa isipokuwa yule aliye na elimu iliyozama kabisa. Ama yule mwenye kufikiri tu, au anasema yale aliyoyasikia kwa watu hapaswi kutoa fatwa.”

Kauli hii ya Ibn Qayyim inasadifu hali halisi iliyopo katika jamii yetu. Kwa sababu hii, Muislamu hapaswi kutoa fatwa bila elimu sahihi. Kutoa fatwa pasina elimu kunaweza kusababisha mkanganyiko mkubwa hasahasa katika jamii ambazo hazitambui mamlaka ya Wanazuoni.

Hatuwezi kumlaumu mtu mwingine kwa sababu kuwapo kwa tatizo hili kunatokana na kukosekana mifumo ya utendaji kazi na uwajibikaji kwa viongozi wetu wa kidini hasa linapokuja suala la ufafanuzi wa masuala muhimu ya kidini.

Hatuyasemi haya kwa nia mbaya bali tunataka kuonesha umuhimu wa Waislamu kujifunza elimu ya sharia kwa sababu mtu hapaswi kuzungumza jambo ambalo hana elimu nalo.

Allah anasema ndani ya Qur’ an: “Na wala usifuatilie usiyo na elimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo – vyote hivyo vitaulizwa (siku ya kiyama).” [Qur’an, 17: 36].

Muislamu anatakiwa apatiwe majibu sahihi kuhusu mambo ya dini yake na siyo kujibiwa kijuujuu.

Katika kulisisitiza hilo, Imam Ibn Qayyim (Allah amrehemu) amesema:“Mtu anayetenda bila elimu ni sawa na anayesafiri bila muongozaji, na inajulikana kuwa mtu kama huyu ni rahisi sana kuangamia kuliko kuokoka.” (Taz: ‘Miftaahu Daar As-Sa’aadah,’ 1/182–83).

Kwa hakika, kutoa fatwa ni jambo lililokuwepo tangu enzi na enzi na litaendelea kuwa kipengele muhimu na cha msingi katika kuleta ustawi na mafanikio ya Uislamu na Waislamu.

Lakini ili mtu afikie daraja au kiwango cha kutoa fatwa ni lazima asome elimu ya sharia ya Kiislamu (Fiqhi) na kanuni zake, kufahamu saikolojia na tabia ya muulizaji swali na kujifunza kujibu maswali kwa adabu na kuchunga uwezo wa kiakili wa muulizaji.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close