1. Tujikumbushe

Baada ya Imani, hapewi mtu kingine bora kuliko afya

Allah ameturuzuku wanadamu neema zisizohesabika, kama alivyosema Mwenyewe katika kitabu chake kitukufu, [Qur’an, 16:18]:

“Na mkizihesabu neema za Allah hamtozidhibiti! Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu.”

Moja kati ya neema kubwa za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwetu ni afya. Ni nini afya? Ni viwango tofauti vya utimamu wa mwili ambao Mwenyezi Mungu ametupatia katika vipindi tofauti vya maisha yetu. Mwenye afya hakika ni miongoni mwa waliopewa neema kubwa kwani ustawi wa mwanadamu unategemea hali ya mwili.

Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) wakati fulani alipanda juu ya Mimbari kisha akalia na kusema:

“Muombeni Mwenyezi Mungu msamaha na afya, kwani baada ya kupewa Imani yenye yakini, mtu hapewi kingine kilichobora zaidi ya afya.”

Viwiliwili ni amana tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa muda uliokwishakadiriwa na hakika Mwenyezi Mungu atatuuliza jinsi tulivyoitunza na kuitumia.

Bahati nzuri ni kuwa Afya njema imefungamana na mafundisho ya Uislamu ambapo Qur’an na Sunna zina maelekezo lukuki juu ya namna ya kutunza afya, aidha kwa kinga au tiba kwa kuishi maisha ya utwaharifu na utakaso. Katika makala ya leo ya afya tutaangalia baadhi ya maelekzo hayo.

Usafi

Uislamu umehimiza sana usafi. Imeandikwa katika Qur’an: “Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha…” (2:222). Katika Hadith, Mtume amesema: “Uislamu ni usafi, basi jisafisheni kwani haingii Peponi ila aliye safi.”

Uislamu umefanya usafi (tohara) kuwa sharti la ibada nyingi, mathalan sala. Mtume amesema: “Haikubaliwi sala yoyote pasi na tohara.” Udhu kabla ya sala ni sharti la kiibada. Udhu hujumuisha kunawa vitanga vya mikono, kusukutua mdomo, kusafishaji tundu za pua, kunawa uso kisha mikono, kuosha kichwa, kisha masikio, kisha miguu.

Vitendo hivyo hufanywa kwa utaratibu huo ambao ni hakikisho la kudumu la kiafya kwa Waislamu. Mtu anaweza kuona namna kila kitendo kilivyochukua nafasi yake ya kiafya kabla ya kingine. Kwanza, vianze viganja kuwa safi kisha ndipo viteke maji kupeleka mdomoni. Baada ya maji kutiwa mdomoni ndipo yatiwe puani. Mikono ingeanza puani na kisha kuja mdomoni usingekuwa usafi. Kwa ujumla, zoezi zima la udhu limekaa kiafya.

Ni aibu na haifai jamii ya Kiislamu kufundishwa kanuni za usafi ambazo ni matokeo ya magonjwa ya milipuko kama kipindupindu. Kwenye suala hilo hilo la usafi, Aisha (Allah amridhie) alimsikia Mjumbe wa Allah akisema:

“Mambo kumi ni katika Sunna, kukata mustachi, kufuga ndevu, kutumia mswaki, kutia maji puani ( kusafisha ) , kukata kucha, kusafisha maungio ya vidole, kutoa nywele z a kwapani, kunyoa sehemu za siri, kusafisha sehemu za siri.” Msimulizi anasema amesahau jambo la kumi lakini inaweza kuwa kusukutua mdomo.” [Sahih Muslim].

Ukiangalia mambo haya yote yanalenga katika usafi wa mtu. Kwa ujumla, ni aibu na haifai jamii ya Kiislamu kufundishwa kanuni za usafi ambazo husaidia kuzuia magonjwa ya milipuko kama kipindupindu.

Lishe na adabu za ulaji Kuna aya kadhaa wa kadhaa katika Qur’an zinazohimiza ulaji wa kiafya na kula kwa kiwango. Mwenyezi M u n g u anasema:

“Enyi mlio amini! Kuleni vizuri t u l i v y o kuruzu – kuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.”[Qur’an 2:172].

Katika aya nyingine, Mwenyezi Mungu anasema: Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.” [2:168]. Aidha, katika Uislamu, tunafndishwa kula kwa wastani: “Kuleni vitu vizuri lakini msipite kiasi.” [Qur’an, 20:81].

Naye Bwana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Sisi ni watu hatuli mpaka tusikie njaa na tukila basi hatushibi (kupita kiasi).”

Katika ufafanuzi zaidi, Mtume amesema katika hadith nyingine:

“Hakuna chombo chenye shari ambacho mwanadamu amepata kukijaza kama anavyolijaza tumbo lake. Mwanadamu hahitaji ila matonge machache ya chakula ili kubakia na nguvu. Ikibidi kula agawe theluthi moja ya tumbo lake kwa ajili ya chakula, theluthi kwa ajili ya maji, na theluthi kwa ajili ya pumzi.’ [Ibn Majah].

Kuna mengi mengine yamaeelekezwa katika adabu za kula ikiwemo kusema Bismillah kunawa kabla na baada ya kula, kula sehemu iliyokuelekea katika sahani, kupoza chakula, kutafuna vema, kunywa maji kwa vituo vitatu na kadhalika. Hata vyakula vilivyokatazwa pia ni kwa faida yetu. Tafiti ngapi za kisayansi, kwa mfano, zimethibitisha madhara ya nyama ya nguruwe na nyinginezo zilizokatazwa katka Uislamu? Ni nyingi mno.

Sala za kila siku na funga

Ingawa faida ya kwanza ya sala na funga ni utii wa kutimiza amri ya Mwenyezi Mungu, sala pia faradhi huleta tija muhimu katika kusaidia mzunguko wa damu, kupumua pumzi vizuri (breathing) na kulainisha maungio yote ya mwili, ikiwemo shingo, kiuno, magoti, vifundo vya miguu, viwiko, viganja, vidole yote hushughulishwa pale mtu anaposwali.

Mazoezi ya sala ni mazuri kwa sababu ni ya wastani (yaani hayachoshi) na endelevu. Waislamu tunafanya mazoezi ya sala, faradhi na Sunna, katika maisha yao yote.

Kwa upande wa swaumu, tunapofunga Ramadhan au swaumu nyingine za Sunna, miili yetu huweza kuondosha sumu inayotokana na vyakula vingi vya kuchakatwa viwandani, vyenye kemikali, ambavyo ndivyo tunavyokula kwa wingi. Pia, kwa kufunga, mfumo wa umeng’enyaji hupata mapumziko na pia husaidia wenye miili mikubwa na presha ya kupanda.

Kuharamishwa kwa vilevi

Uislamu unakataza kabisa vilezi ikiwemo pombe na mihadarati, ikiwemo sigara kwa sababu husababisha madhara makubwa na ya muda mrefu katika akili, mwili na kwa maisha ya jamii.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Bila shaka, ulevi na kamari na kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kupiga ramli ni najisi, na ni kazi za shetani, Basi jiepusheni navyo ili mpate kufaulu. Hakika shetani anataka kukutieni katika uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari na anataka kukuzuilieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi, je, mtaacha? [Qur’an, 5:90-91].

Ulalaji mzuri

Kuna mambo kadhaa yameelekezwa katika adabu za ulalaji ambayo nayo kimsingi yanasaidia kulinda afya zetu. Baadhi ya mambo ambayo yameelekezwa kuhusu ulalaji ni pamoja na kutochelewa kulala baada ya sala ya Isha ila kwa dharura, kukung’uta kitanda, kulala na udhu, kuanza kulalia upande wa kulia. Pia, haifai kulala kifudifudi kwani ulalaji huo umeitwa kuwa ni wa watu motoni.

Kwa ujumla kuna maelekezo mengi ya kidini ambayo ukiacha kuwa ni utii kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie) pia yana faida kiafya ni mengi mno. Wajibu wetu ni kushikamana nayo, kadri ya uwezo wetu, ili tulinde afya zetu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close