1. Tujikumbushe2. Deen

Anayetambua kuwa ataulizwa, aandae majibu

Fudhwail bin Iyadh (Allah amrehemu) alikutana na mtu mmoja akamuuliza: “Umefikisha umri wa miaka mingapi?” Yule mtu akajibu: “Miaka sitini.” Fudhwail akasema: “Tangu miaka sitini iliyopita unaelekea kwa Mola wako, sasa umekaribia kufika.” Mtu yule akasema: “Innaa lillahi wainnaa ilayhi raajiun.” Fudhwail akamuuliza: “Unajua unachokisema?” Akamuambia: “Nimesema, ‘Inna lillahi wainnaa ilayhi raajiun.’ Akasema: “Unaijua tafsiri yake?” Akasema: “Ewe Abu Ali! Basi nitafsirie.”

Akamuambia: “Unaposema hivyo, maana yake unakiri kuwa wewe ni mja wa Allah na kwake utarejea. Anayetambua kuwa yeye ni mja wa Allah na kwake atarejea basi ajue kuwa atasimamishwa na ataulizwa (kwa yale aliyokuwa akiyafanya); na anayetambua kuwa ataulizwa basi na aandae majibu ya kila swali.”

 Mtu yule akasema: “Sasa nitumie njia gani?” Fudhwail akamjibu: “Njia ni nyepesi tu.” Akauliza: “Ni ipi hiyo, nifahamishe.” Akamuambia: “Fanya mema katika umri wako uliobaki; na Allah atakusamehe yale uliyofanya katika umri uliopita na uliobaki kwani ukifanya maovu katika umri uliobakia utaadhibiwa kwa yaliyopita na yajayo.” [Taz: ‘Hilyatul – Auliyaa’].

Katika tukio hili yapo mengi ya kujifunza, na miongoni mwa hayo ni:

  • Kupupia mambo ya kheri Kila ifikapo mwezi wa Muharram, huwa tunahesabu kumalizika kwa mwaka wa Kiislamu na kuuanza mwaka mwingine. Si hivyo tu, pia wapo wengi wanaosherehekea siku zao za kuzaliwa huku wakisahau kuwa siku zao za kuishi hapa ulimwenguni zinapungua na hivyo kulikaribia kaburi.

Kuna umuhimu wa kufikiria tunayoyafanya na tuliyoyafanya kwa sababu moja kubwa ya kiimani, nayo ni: kujiandaa kuulizwa Siku ya Kiyama kuhusu matendo yote tuyafanyayo hapa ulimwenguni.

Katika tukio hili, Fudhwail (Allah amrehemu) anamkumbusha mtu aliyekutana naye kuwa anakaribia kumaliza safari ya maisha ya dunia. Hii ina maana, safari yake ya kuelekea Akhera ambayo aliianza tangu akiwa mchanga inakaribia. Kwa sababu hiyo, mtu huyo anapaswa kujipinda na ibada, kutubia makosa na kumuomba Allah msamaha ili asamehewe madhambi yake yaliyopita.

Mwanzo wa mwaka wa Hijra ni muda muafaka wa kutafakari katika nafasi ya mtu mmoja, familia na Waislamu kwa ujumla tumetekeleza vipi ibada za Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo yake.

Kubadilika kwa siku, miezi na miaka kunamaanisha kuwa umri nao unabadilika. Hii ni kwa sababu usiku na mchana ndiyo vituo vya umri wa mwanadamu. Kila unapobadilika usiku kwenda mchana, mwanadamu anahama kituo kimoja na kuingia kingine katika mchakato wa kuifikia safari yake ya Akhera.

Yapasa tuzingatie na kutambua kuwa, maisha ya dunia ni ya mpito. Qur’an yasema: “Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye kuona.” [Qur’an, 24:44]. Swali la kujiuliza ni je, tumejiandaa vipi kwa maisha yajayo?

Watu werevu wanatambua kuwa kila dakika na sekunde katika maisha yao ina thamani na ndiyo maana hawapotezi muda kwa kufanya mambo ya hovyo kwa kuelewa kuwa miaka hairudi nyuma, na ikishapita hakuna namna ya kuirejesha.

  • Fanya mema muda wote Ni jambo muhimu kwa kila Muislamu kuwa na matumaini mazuri yenye kuambatana na matendo mema. Imethibiti katika Hadithi sahihi kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akichukizwa na watu wenye matumaini mabaya (nuksi) kama ilivyokuja katika Hadithi ya Aisha (Allah amuwie radhie) ambaye amesema: “Mtume (rehema na amani zimshukie) alikuwa anapenda mategemeo mazuri na anachukizwa na nuksi (twiyara).” [Ibn Majah].Maazimio ya ukweli Tuwe na azma ya kweli ya kutumia uhai wetu katika mambo yanayomridhisha Allah na Mtume wake. Pia, tuondoshe udhaifu uliotawala katika nafsi zetu sanjari na kutenda kheri kwa ajili ya kufikia kilele cha mafanikio.
  • Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani imshukie) alikuwa anamuomba Allah ampe uimara na azma ya kutekeleza majukumu aliyopewa. Aidha, Mtume aliwahamasisha Maswahaba (Allah awaridhie) kufuata haki na kuusiana (kushikamana) na subira (kustahamiliana).

Miongoni mwa dua ambazo Mtume alikuwa akiwaombea Maswahaba zake ni ile inayosema: “Ewe Mola ninakuomba uimara (uthabiti) katika mambo na maazimio katika uongofu. Ninakuomba niwe mwenye kushukuru neema zako na kutekeleza vema ibada zako. Ninakuomba unipe ulimi wenye ukweli na moyo uliosalimika, na ninajilinda kwako kwa shari unazozijua, hakika wewe ndiye Mjuzi wa yale yaliyofichikana.” [Ahmad, Tirmidhiy na Nasai].

  • Tujifunze kwa Jarir (Allah amridhie) Amesema Jarir bin Abdillah Albajaliy (Allah amridhie): “Nilimwendea Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akawa anawapa watu ahadi ya utii (Bay’ah). Nikamuambia, “Ewe mjumbe wa Allah, nyoosha mkono wako nikupe bay’ah na uniwekee sharti kwa sababu wewe ndiye unayejua zaidi.” Mtume akasema: “Nakubaliana nawe kuwa utamuabudu Allah, na utasimamisha sala, na utatoa zaka, na utawanasihi Waislamu na utafarikiana na washirikina.” [Nasai].
  • Kumtii Allah na kutekeleza maamrisho yake Mwaka mpya wa 1441 Hijriya ni kipindi muhimu kwa Waislamu kuhuisha imani yao, kutenda yaliyo mema, kusimamisha haki na kufanya subira ili kubakia katika haki. Wapo watu wengi waliobadilika kitabia, wakazihuisha imani zao na Allah akawafanyia wepesi katika mabadiliko hayo.

Hata hivyo, ifahamike kuwa mabadiliko hayaji kama kimbunga au mafuriko, kwamba yakipita mara moja unaona mabadiliko. Mabadiliko yanaanzia kwa mtu mwenyewe kubadilika. Bila kuwa na ari, moyo na dhati ya mabadiliko; hakuna mabadiliko yatakayotokea.

 Qur’an yasema: “Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi neema alizowaneemesha watu mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” [Qur’an, 8:53].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close