1. Tujikumbushe

Mimbari Zetu: Kifo ni lazima, umejiandaaje?

Uhuru ambao Allah Aliyetukuka ametupatia hapa ulimwenguni, hautakiwi kutafsiriwa katika lugha ya ‘kupata’, bali iwe lugha ya tahadhari na maandalizi.


Daima tunasisitizwa kuishi kwa hofu kana kwamba tutakufa kesho. Wengi wetu tunajisahau na kuishi kama tutabaki milele. Kifo ndiyo mwisho wa yote yanayohusu ulimwengu huu, lakini ndiyo mwanzo wa safari nyengine ambayo ni kubwa na ngumu au laini kutokana na namna ulivyojiandaa.


Allah Aliyetukuka anasema: “Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.”
(Qur’an, 50:19).


Na hiki kifo kina hamkani yake na hakuna uchochoro wa kukikwepa. Pia ijulikane kuwa, ulichokichuma hapa duniani huleta athari hadi katika namna ya utolewaji wa roho yako. Uchungu ni mkali hasa ikiwa maandalizi yako ni mabovu. Ninapohoji tumejiandaaje na kifo, siyo maandalizi ya suti na moka ngapi, au gari aina gani na pesa kiasi gani katika akaunti yako ya benki. Hivyo vyote utaviacha hapa hapa. Allah Aliyetukuka anasema katika Qur’an (11:14):

Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza wa kila kitu.”

Kule utaulizwa ujana wako umeutumiaje? Mali zako umezitumiaje? Vichunga vyako vinavyokuzunguka umevichungaje? Allah atakuhoji kwa kila neema aliyokubariki na utatakiwa kutoa majawabu yaliyonyooka. Hakuna kuvunga vunga, kudanganya wala habari za kumuhonga jaji.


Kuna mshairi anasema: “Ndani ya shimo kumbuka, huna hapo mtetezi. Majuto yanakufika, na ukiwa na simanzi, ubaki kuhangaika, hakuna cha usingizi, Tunakumbuka mauti, tunapoona jeneza.”
Ni kweli, wapo wanaokumbuka mauti wakiliona jeneza, hizo ndiyo nafsi laini zinapokumbana na mawaidha. Kwa mujibu wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), kinachoondoa kutu katika moyo ni kuyakumbuka mauti na kusoma Qur’an. Bahati mbaya wengi tuna mioyo migumu kiasi kwamba hata jeneza
halitushtui tukumbuki. Huu ni mtihani
ndugu zangu Waislamu. Mtu asiyekumbuka kwamba kuna kifo na kufufuliwa, atakuwa na muda wa kufanya maandalizi ya huko aendako?


Allah Aliyetukuka anakumbusha katika Qur’an: “Wanaotaka maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa humo vitendo vyao kamili. Na wao humo hawatopunjwa. Hawa ndiyo ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyoyafanya, na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda.” (Qur’an, 11:15-16).


Kuwa na gari na mali nyingi au nyumba nzuri siyo mwisho wa hadithi. Kumbuka kuwa ukiendekeza vitu hivyo, Allah atakuacha tu, lakini atakutia mkononi pumzi zako zikikata. Maadamu upo duniani, kila ulichopewa, ni sharti ukitumie kwa ajili ya maandalizi ya maisha baada ya kufa kwako. Hilo halina hiari ikiwa unataka makao mema huko twendako. La, kama una uwezo wa kupambana na moto, basi endelea na mikogo ya kilimwengu hadi pumzi ikate.


Tusijipumbaze na kuzidanganya nafsi zetu. Hakuna mwenye uwezo wa kupambana na moto wala kukwepa kifo. Kufa kwa kiongozi wetu wa umma ni kielelezo tosha kwamba hakuna wa kukwepa. Allah Aliyetukuka anasema:

Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwishapita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Naatakayegeuka akarudi nyuma, huyo hatamdhuru Allah kitu. Na Allah atawalipa wanaomshukuru.” (Qur’an, 3:144)

Ulipofika muda wake, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliondoka. Habari njema ni kuwa yeye alijiandaa vyema kukutana na Muumba wake. Kisanga kipo kwetu mimi na wewe tunayeabudu uzinzi, riba, dhulma, utapeli na kila maovu.


Allah Aliyetukuka anasema: “Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao watakuwa pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii na Wakweli na Mashahidi na watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!” (Qur’an, 4:69). Hayo hayatokuja bure bure. Juhudi na taqwa ya moyo vinahitajika. Allah Aliyetukuka mwenyewe anasema pepo haipatikani hivi hivi tu. Huwezi kutenda maovu, kisha utegemee pepo. Akili gani hizo?

Sisi ni kama wanafunzi katika chumba cha mtihani. Juhudi zako za kabla ndiyo zitakazokuwezesha kufeli au kupasi. Hakuna muujiza wala longolongo katika hilo. Maandalizi yako mazuri ndiyo yatakayokuokoa. Allah Aliyetukuka anasema:


“Wale walioamini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo mazuri.” (Qur’an, 93:29).


Maisha haya ni mafupi mno, yasituhadae wala kutupumbaza. Tuwaache wale wanaoifanya dunia kuwa ndiyo pepo yao, ambao hawajajifunza kwa waliopita waliofanya hivyo hatimae wakamezwa na udongo. Hilo linapaswa kuwa somo kwetu. Watu wamekufa maelfu na mamilioni ya miaka, kwa sasa wameshasahaulika. Wapo walioutumia muda wao duniani vizuri na wapo walioutumia vibaya. Malipo yote yapo kwa mwenyewe Allah Aliyetukuka. Ukiwa unaendelea kupumua maana yake bado nafasi unayo. Allah Aliyetukuka anatupenda ndiyo maana anatupa hiyo
nafasi. Tusiwe wajinga wa nafsi zetu ndugu zangu Waislamu.

Ghururi za kilimwengu zitatuumiza wenyewe siku ya mwisho, siku ambayo mtoto hatomjua mzazi wala mke hatomjua mume. Kila mmoja anapambania hali yake. Siku hiyo, sote tutakuwa uchi lakini hakuna mwenye muda wa kumshangaa mwenzake. Ni siku ngumu mno, ambapo utasimamishwa mbele ya Allah Aliyetukuka uulizwe juu ya kila tendo lako. Ili kuwa na jawabu nzuri maana yake unahitaji maandalizi mazuri ya hapa duniani.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close