5. Ramadhan

Utaratibu na muongozo wa kufunga mwezi wa Ramadhan

Neno swaumu, kwa lugha ya Kiarabu linamaanisha kujizuia au kunyamaza kama ilivyokuja katika Aya: “Hakika mimi (Maryam bint Imran) nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.” [Qur’an, 19:26].

Katika muktadha wa sharia ya Kiislamu, swaumu ni kujizuia kula, kunywa na kutangamana na mke au mume kwa tendo la ndoa. Zaidi ya kujizuia na kula, kunywa na tendo la ndoa, swaumu katika Uislamu humtaka mwenye kufunga kujizuia na kauli au matendo yote yaliyokatazwa na Allah.

Sharia ya funga ya Ramadhan
Katika sharia ya Kiislamu, funga ya Ramadhan ni lazima (wajibu). Na wajibu huo umethibiti katika Qur’an, Sunna (Hadithi za Mtume) na katika makubaliano ya Wanazuoni (Ijmaai). Ibada ya swaumu ilifaradhishwa mwaka wa pili baada ya Mtume kuhama Makka kwenda Madina.

Allah Mtukufu anasema: “Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga swaumu kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate
kumcha Mungu,” [Qur’an, 2:183].

Kwa faida ya msomaji, swaumu za faradhi yaani lazima katika Uislamu ni pamoja na swaumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, swaumu ya nadhiri, swaumu ya kuomba kufutiwa dhambi (kafara), kwa dhambi aliyoitenda mtu kama ilivyoelezwa katika vitabu vya Fiq–hi.

Hapana shaka kwamba ibada ya swaumu ilikuwapo katika umma zilizotangulia kwa ushahidi wa Aya ya 183 Suratul Baqara tuliyoinukuu hapo juu. Ibada ya swaumu imekuwa sehemu ya matendo makuu ya ibada katika dini zote zenye kujinasibisha na Allah, maarufu kama ‘Adyaan as–samaawiyyah’ au dini ambazo mafundisho yake yalishuka kutoka mbinguni.

Malengo ya swaumu
Lengo kuu la swaumu ya Ramadhan ni kama lilivyoelezwa katika Suratul–Baqara [2:183], ili kuupata uchamungu. Maana ya uchamungu ni kumkumbuka Allah kila wakati, kumtii kwa kuacha makatazo yake na kutekeleza maamrisho yake na kuwatendea wema viumbe wa Allah kwa kutafuta radhi zake tu.

Lengo la pili la swaumu ni kumuwezesha mfungaji kuelewa hali ya dhiki ya njaa, kiu na tabu za umasikini zinazowakabili wale wasiokuwa nacho na hivyo kumsukuma mfungaji kuwahurumia, kuwatendea wema na kushukuru neema za Allah alizopewa.

Hapo awali, Uislamu uliwaharamishia watu waliofunga kula, kunywa na kufanya tendo la ndoa na wake zao wakati wa usiku. Ni kwamba mtu aliyefunga mchana wa Ramadhan kisha akawa hajafuturu wakati wa Magharibi, mtu huyu hakurusuhusiwa kunywa, kula na kufanya tendo la ndoa na mkewe wakati wa usiku. Hata hivyo, sharia hiyo ilifutwa na mambo hayo matatu yakahalalishwa katika usiku wa Ramadhan.

Al–Barrau (Allah amridhie) amehadithia: “Ilikuwa mmoja wao anapofunga, muda wa kufungua (swaumu) ukawadia, na akalala kabla ya kufungua, haruhusiwi kula usiku huo wala mchana wake hadi ifike jioni.”

Katika kisa kimoja, Qais bin Swirmah al–Answari alikuwa amefunga na ulipofika muda wa kufungua alimwendea mkewe na kumuuliza: “Je, kuna chakula?” Mkewe akajibu: “Hapana lakini naenda kukuchukulia.” Mchana wa siku hiyo Qais alikuwa amefanya kazi ngumu sana, hivyo akalala. Mkewe alipofika aligundua kuwa amelala hivyo akamuambia: “Umekula hasara! Huwezi tena kula chakula hiki.” [Bukhari].


Allah anasema: “Na (katika mwezi wa Ramadhan) mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.” [Qur’an, 2:185].

Ulipowadia mchana wa siku iliyofuata Qais alipoteza fahamu. Punde, baada ya Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) kujuzwa mkasa huo, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii: “Mmehalalishiwa usiku wa swaumu kuingiliana na wake zenu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku.” [Qur’an, 2:187].

Imeandikwa kwenye vitabu vya historia (Tareikh) kuwa, katika uhai wake, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) aliwahi kufunga swaumu ya Ramadhan misimu tisa (kuanzia mwaka wa pili Hijriya hadi wa kumi).

Fadhila na utukufu wa mwezi wa Ramadhan
Zifuatazo ni baadhi ya fadhila zinazopatikana ndani ya mwezi wa Ramadhan: Allah Aliyetukuka amejaalia Ramadhan kuwa ndiyo mwezi ilipoteremshwa Qur’an. Allah anasema: “Mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa humo Qur’an kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizowazi za uongofu na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hesabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hesabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.” [Qur’an, 2:185–186]. Hii ilikuwa katika kumi la mwisho la Ramadhan kama ilivyokuja katika Aya: “Hakika Sisi tumeiteremsha Qur’ an katika Laylatul Qadri, usiku wa cheo.” [Qur’an, 97:1].

Kila uingiapo mwezi wa Ramadhan, Allah Mtukufu hufungua milango ya pepo na kuifunga ile ya moto. Mashetani na majini hudhibitiwa na kufungwa pingu. Allah hufungua milango ya rehema na baraka kwa waja wake. Katika Hadithi iliyopokewa na Imamu Bukhari na Muslim, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mwezi wa Ramadhan unapoingia, milango ya peponi hufunguliwa na milango ya motoni hufungwa, na mashetani hutiwa pingu.”

Ndani ya mwezi wa Ramadhan, Allah hukubali maombi ya waja wake kwa haraka. Watu humshukuru Allah kwa wingi na kumdhukuru. Allah anasema: “Na (katika mwezi wa Ramadhan) mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.” [Qur’an, 2:185].

Swaumu ya Ramadhan hufuta dhambi ndogo ndogo. Imepokewa kutoka kwa Abuu Huraira (Allah amridhie) kuwa, Mtume (rehema na amani zimfikie) amesema: “Sala tano, na sala ya Ijumaa hadi Ijumaa nyingine, na swaumu ya Ramadhan, hufuta dhambi zinazojitokeza katikati yake, kama mtu atajiepusha na dhambi kubwa.” [Bukhari na Muslim].

Ramadhan ni fursa kwa waja kufutiwa dhambi zao. Imesimuliwa kwamba: “Siku moja Mtume alipokuwa juu ya mimbari aliitikia ‘Amiin, Amiin, Amiin.’ Akaambiwa, ‘Hujawahi kufanya ulivyo fanya leo?’ Mtume akasema, ‘Malaika Jibril alinijia akaniambia amekula hasara mtu ambaye amekutwa na Ramadhan na asisamehewe dhambi zake.’”

Mwenye kufunga mwezi wa Ramadhan atakuwa pamoja na Mitume na wasema kweli Siku ya Kiyama. Mwenye kusimama usiku wa Ramadhan anafutiwa dhambi zake zilizopita.

Ramadhan ndiyo mwezi pekee ambao ndani ya waumini husali sala ya Tarawehe kwa jamaa. Kutekeleza ibada ya Umra katika mwezi wa Ramadhan ni sawa na kuhiji pamoja na Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie).

Hakika Ramadhan ni mwezi wa kuzidisha ukarimu. Hilo linatokana na mambo makuu matatu: Mosi, Ramadhan ni mwezi wa funga, ibada ambayo humfanya mtu awe mkarimu na mwenye kufanya matendo ya kheri. Pili, Ramadhan ni mwezi ambao huzidishwa thawabu ndani yake. Amali njema ndani ya Ramadhan hulipwa maradufu, ukilinganisha na miezi mingine. Tatu, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akikithirisha kusoma Qur’an ndani ya mwezi wa Ramadhan. Qur’an humshajiisha mtu kutoa na kusaidia watu wengine, kama anavyosema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Na toeni katika alivyokufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake,” [Qur’an, 57:7].

Ramadhan ni fursa adhimu ya kujipinda na ibada za usiku (Qiyaamu Llyal). Imethibiti kutoka kwa Aisha (Allah amridhie) kwamba, katika kumi la mwisho la Ramadhan, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akihamia msikitini kwa ajili ya itikafu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close