5. Ramadhan

Tupambane kudhibiti tatizo la usahaulifu wa Ramadhan

Usahaulifu’ wa Ramadhan ni maradhi yanayowaathiri mamilioni ya Waislamu nchini Tanzania na ulimwenguni kote, lakini rasilimali zilizowekezwa kwenye uchunguzi wa matibabu ya maradhi haya ni chache. Maradhi haya yanasambaa kwa haraka na yanaweza kuambukizwa kupitia hotuba, vitendo na hata fikra.

Chanzo cha mlipuko huu wa maradhi kwa kawaida ni sherehe za kupitiliza za Idd, ambazo zinamfanya muathirika asahau kila funzo muhimu alilopata ndani ya Ramadhan.

Maradhi haya ya ‘usahaulifu’ yanaweza yakadumu kwa miezi 11 mpaka Ramadhan ijayo, ambapo muathirika atafurahia nafuu ya muda kutokana na dalili za maradhi haya, na kisha kuambukizwa tena ugonjwa huu mwishoni mwa Ramadhan.

Kwa hiyo, duara la miezi 11 ya kuteseka na mwezi mmoja wa nafuu linaendelea mwaka baada ya mwaka, huku waathirika wakiishi kwa kukataa hali yao hii. Nadhani bado tunaweza kukumbuka wazi mandhari, hususan katika usiku wa siku kumi za mwisho za Ramadhan, ambapo Waislamu wanakusanyika kwa maelfu katika nyumba za Allah kwa ajili ya kusimama, kurukuu na kusujudu nyuma ya imamu mmoja.

Nadhani tunaweza kukumbuka Qunut za hisia zilizoombwa wakati wa Sala za Witri, karibu tufumue mapaa ya misikiti kwa sauti, tukimlilia Mwenyezi Mungu aunganishe nyoyo zetu, ainue daraja zetu na aondoe vinyongo tulivyowekeana katika nyoyo zetu.

Nadhani bado tunaweza kukumbuka sauti za vilio vya Waislamu wakiomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwa sauti kama ile iliyosimuliwa katika ‘Riyadh al-Salihin’ kuhusu kulia kwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) wakati wa sala za usiku.

Lakini ni jambo la kushangaza sana jioni ile ile ambayo Ramadhan inakaribia kukamilika, ambapo tulipaswa kumuomba Allah ‘Azza wa Jalla’ akubali funga, sala na sadaka zetu, sisi tunaleta malumbano makali kuhusu siku sahihi ya Idd. Hapo utaona Waislamu tukishutumiana vikali saa chache baada ya kwisha tu Ramadhan badala ya kumlilia Allah Ta’ala aunganishe nyoyo zetu!

Hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) inayozungumzia kuanza na kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan inasema: “Fungeni kwa kuonekana kwake (mwezi mwandamo) na fungueni kwa kuonekana kwake, na kama umejificha kutokana na mawingu kamilisheni siku 30. “[Bukhari na Muslim].

Hata wakati wa zama za Maswahaba, walikuwa wakisherehekea Idd siku tofauti katika maeneo tofauti ya dunia, ambapo Maswahaba waliokuwa Sham (Syria) wakianza Ramadhan katika siku tofauti na wale waliokuwa Madina. Ni jambo la kawaida linalotokana na Idd kutambuliwa kwa kuonekana mwezi mwandamo, ambao unaweza kuonekana kwa watu wa upande mmoja na usionekane kwa wengine na mawasiliano wakati ule yalikuwa duni.

Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka elfu moja ya histora ya Kiislamu, haijawahi kutokea Waislamu wa eneo moja au mji mmoja kusherehekea Idd katika siku mbili tofauti. Ndugu zangu katika Imani, huu ni mzaha kwa dini yetu na inazuia tunu za Uislamu zisionekane wazi kwa vitendo, hususan katika nchi ambazo si za Waislamu.

Mtume (rehema za Allah na
amani zimshukie) amesema: “Funga yenu ni siku mnayofunga, na kufungua kwenu ni siku mnayofungua, na siku ya kuchinja kwenu ni siku mnayochinja. “ [Tirmidhiy].

Al-Tirmidhi amesema: “Baadhi ya wanazuoni wamefafanua Hadithi hii kumaanisha kwamba kufunga swaumu na kufungua kunapaswa kufanywa na Waislamu kama umma (jama’ah).”

Kwa hiyo, mwezi wa Ramadhan unaanza wakati umma wa Waislamu unapokubali na unamalizika wakati umma huo unapokubali, na viongozi wa jamii wanawajibika kufuata mwandamo wa mwezi au kukamilisha siku 30 kama ilivyoelekezwa kwenye Hadithi.

Nimeshawahi kuwaona Waislamu katika baadhi ya nchi wakiwa na laptops, ‘astronomical charts’, ‘calculators’ na timu zao wakijaribu kuthibitisha au kukanusha iwapo siku fulani ya Idd ni ‘sahihi’ au la. Kama umma wa Waislamu umeanza na kumaliza mwezi pamoja, na viongozi wao wamefuata utaratibu halali wa kutangaza mwanzo wa kuanza kufunga na mwisho, yaani kuandama kwa mwezi au kukamilisha siku 30, basi kukokotoa, kutabiri na chati za wanajimu hakuna ulazima.

Kiukweli, vitabu vya sharia ya Kiislamu vinanukuu makubaliano kuhusu mtazamo wa kutofikiria unajimu au ukokotozi kama nyenzo ya kuthibitisha mwanzo wa Ramadhan au Idd. [Rejea: al-Jassas al Hanafi, al-Baji al-Maliki, Ibn Rushdal Maliki, al-Subki al-Shafi’i, Ibn Taymiya, Ibn ‘Abidin al-Hanafi].

Matatizo matatu yanayoibuka
1) Mawasiliano ya hapo kwa hapo – Hivi sasa, tunaweza kuona taswira za satellite zikionesha duniani kote ndani ya nusu sekunde tu tangazo la Ramadhan na Idd kule Makka, Morroco, Mauritania na hata Maldives. Tufuate wapi? au tujaribu wenyewe kuangalia mwezi hapa Tanzania, hata kama kuna mawingu mazito?

2) Viongozi wetu ni akina nani?- Nani tumuamini na jukumu la kutangaza Ramadhan na Idd? Misikiti yetu Wanazuoni? Wanajimu? Kamati za taasisi za kutangaza mwezi mwandamo?

3) Kila kundi la Waislamu ndani ya eneo moja, mji mmoja au nchi moja kutangaza kuanza kwa Ramadhan au Idd kwa misingi yao wenyewe, kunaturudisha kwenye tatizo lile lile la watu wa mji mmoja kusherehekea Idd katika siku tofauti. Tufuate wapi kama kwetu mwezi mwandamo haukuonekana? Kila mwaka inaonekana tunakuwa na makundi mawili kuhusu kuadhimisha sikukuu ya Idd. Wale wanaofuata mwandamo wa kimataifa na wale wanaofuata mwandamo wa eneo lao. Wakati mjadala ukiendelea, kipaumbele ni kuwa na siku moja ya kuanza Ramadhan na kusherehekea Idd.

Ndugu zangu katika Imani, licha ya kukwepa mjadala huu muhimu kwa sababu ya kulinda kile kinachodhaniwa kuwa ni umoja; lakini kwa hakika ni aibu na fedheha kwa
Waislamu wa mji mmoja kufunga au kufungua siku tofauti mwezi mtukufu wa Ramadhan!

Show More

Related Articles

Back to top button
Close